UDHAIFU

UDHAIFU

UDHAIFU

(1)

Ilikuwa ni saa saba adhuhuri pale Joji alipowasili hotelini na kuamua kwenda chumbani kwake kwa ajili ya kuoga na kubadilisha nguo zake ili arudi kwa mara nyingine kula chakula cha mchana katika Kafeteria ya pale hotelini. Na alipoanza kushuka chini mara simu iliita ghafla ilikuwa ni Katarina anampigia:

Hallo..mpenzi wangu.

Habari yako Joji, na vipi huko ugenini nchi ya maajabu?

Ni nzuri na mimi mzima wa afya hapa, na hakika nimemaliza kazi yangu na zimebaki siku mbili tu ili kujua zaidi kuhusiana na mji huu mzuri.

Vizuri, na vipi maswali ya dokta?

Hahaha, wakati mwingine nahisi Tom yupo sahihi, pindi aliposema ukijiweka karibu na dini utaziacha zote, na nahisi mambo yameanza kujitokeza na kuwa wazi kwa kiasi fulani.

Kila unapoukaribia Ukatoliki utafurahishwa nao, kadhalika roho mtakatifu atakufurahisha.

Achana na suala hili, Maiko mwenye kuonekana mfuasi mzuri wa Ukiristo ndio mwenye kuniletea wasichana wa kustarehe nao, na wote hao kwa pamoja Maiko, Kakhi na Tom sijapata kumuamini yoyote kati yao.

Kuwepo kwa mfano mbaya hakumaanisha ubaya wa fikra ya asili, bali huenda ni uthibitisho kuwa asili si mbaya, na hata kama kutakuwa na mfano mbaya, basi elewa kuna makumi ya mifano mizuri!

Umesema kweli, cha muhimu kwanza ni hali za watoto wetu. Vipi hali ya Maiko na Sali?

Wapo katika hali nzuri, na sote sisi tunahamu ya kukuona hivi karibuni.

Na mimi pia nina hamu nanyi ya kukuoneni karibuni.

Katika Kafeteria ya pale hotelini chakula kiliandaliwa vizuri, na watalii wengi kutoka sehemu mbali mbali za nchi walikuwepo hapo. Wakati huo Joji alikaa pembezoni akiwa katika meza ndogo akipata chakula peke yake. Jicho lake likaangukia kwa msichana mzuri wa Kihindi wa miaka ishirini na kitu hivi, mwenye nywele nyingi nyeusi, mwenye macho yenye wanja, na mwenye mwanya wa kutabasamu na kung’aa, alikuwa akiwaangalia watalii wenye kuangaza macho yao, na wakati mwingine akitabasamu nao huku akiwarembeshea macho na vitimbi mbalimbali vya kuwavutia.
Haijulikani nini kilimvutia Joji kwa uzuri wake na mvuto wake pale aliporudiarudia kumtazama yule msichana, na aliamua kushughulika nae kwa chakula na fikra badala ya kushughulika na kazi za intaneti alizotakiwa kuzimaliza na kujikuta akishughulika na yule msichana aliyekaa ghafla katika meza yake.

Kwa jina naitwa Omela, natokea Delhi au kwa jina lingine nafahamika Mrembo wa kufitini. Nimevutiwa nawe pindi nilipokuona macho yako yananivuta ulipokuwa umekaa peke yako, je ungependelea nikuondolee upweke wako?

Joji aliinua macho yake kumwangalia yule msichana aliyekuwa nusu uchi, tumbo lake lilikuwa wazi, na kivazi chake kilikuwa kifupi sana kisichofunika chochote, uso wake ni kama kipande cha mwezi, na nywele zake za hariri na mwenye tabasamu la kuvutia, na haijulikani nini alifurahishwa nacho sana pale alipomujia na kukaa nae katika meza yake.

Jina langu ni Joji, nimetokea Uingereza, nakushukuru kwa utu wako, kisha alikaa kimya kidogo akajaribu kushindana na nafsi yake na kuishinda huku akitamani kuwa nae, lakini inavyoelekea kufanya hivyo kutasababisha mambo mengine kutokea… Samahani nasikitika nipo na kazi sana, na hii ndio mara yangu ya kwanza tangu kufika kwangu India kukaa peke yangu hapa.

Upole wako, vazi lako na muonekano wako ni mzuri, je utapendelea tustarehe pamoja?

Utulivu wako ni mzuri na mimi nafurahishwa na maneno yako, ila baada ya muda mfupi nitakuwa na kazi.

Samahani….unaonekana mpole mwenye tabia nzuri, mimi nina vyeti ambavyo vinaonyesha sina ukimwi.

Alinyoosha mkono wake na kumpa mkononi mwake huku akiukandamiza mkono wa Joji. Joji alihisi ni kama umeme umepenya katika moyo wake, lakini pamoja na yote hayo aliushinda moyo wake na nafsi yake na kurudisha mkono wake kwa upole.

Nimekuelewa – asante sana, mimi nina mke.

Je mke wako unae hapa India?

Hapana yupo Uingereza.

Wengi wanaokuja kutokea Ulaya, Marekani pamoja na dini zao mbali mbali bado wanapenda maisha ya starehe hapa….na uzuri wa India upo katika maeneo mengi.

Nakushukuru na kwa kweli wewe ni mzuri unaovutia sana lakini pamoja na hayo nakushukuru.

Wewe ni mgeni lakini ni mgumu, na wewe ni mtu wa kwanza katika maisha yangu kukutamkia na kukupa moyo wangu halafu unanikataa…

Omela aliondoka kwa haraka, pale pale Joji alijiuliza moyoni mwake kwa mshangao….je mtu huitwa mgumu ambae anasita kumfanyia hiana mke wake na mwenye kuheshimu misingi yake, Hahaha huenda ikawa ni hivyo….. haya ndio maisha yanavyoonekana machoni mwetu kila siku hupita mambo ya ajabu, tusiyoweza kuyatafsiri au huenda yanafasirika kwa njia zetu. Laiti Kakhi angekuwa katika nafasi yangu angefurahi sana usiku huu wa leo akiwa na mwanamke mzuri kabisa!!

(2)

Pindi Joji alipomaliza kula chakula chake, aliangalia saa yake, na kukuta ni saa kumi na nusu kwa majira ya India, sawa na saa za tano asubuhi Uingereza. Na akakumbuka kuwa Katarina alimpigia simu kabla ya masaa manne, yaani saa moja asubuhi na sio kawaida yake kuamka mapema hivyo!
Alipanda ngazi kuelekea chumbani kwake na kuchukua komputa yake ili amalizie kazi zake, alifungua email yake katika sehemu yake ya Face book alimtumia Kakhi akimpa habari nzuri ya kwamba ameingia mikataba na kampuni mbili, kisha akafungua barua hizo zilizopo katika email, baada ya hapo alifungua face book ambayo hakuiangalia kwa muda wa siku tatu na kukuta idadi kubwa ya makala, picha na marafiki wapya, akakuta dokta Tom amemtumia ujumbe wa kutaka urafiki, alimkaribisha na baada kufungua alikuta picha nyingi na kwa mshangao wa ghafla wamepiga picha na Katarina! wakicheka na kula chakula kwa pamoja huku ameandika chini yake ‘pamoja na Katarina’ aliangalia tarehe yake na kukuta inakuwa saa kumi na mbili kwa majira ya London na baadhi ziliandikwa saa kumi na moja na dakika ishirini na tano sawa na tarehe hiyo 15/7….
Wasiwasi ulimshika, kumbe pale Katarina alipompigia simu mapema asubuhi alikuwa pamoja na Tom mpaka saa kumi na moja na nusu, kwa maana hajalala bado! Damu ilichemka katika mishipa yake na kuinua simu akimpigia Katarina na kukuta simu yake imefungwa, alimpigia Tom ambaye alipokea kwa sauti ya uchovu:

Ndio Joji, Katarina amenijulisha kwamba umeanza kujitenga na kila dini.

Wakati gani amekwambia?!!

Alipokupigia tulikuwa pamoja nae, kisha nikampeleka nyumbani, nakupongeza kwa hakika ni mzuri.

Mlikuwa mkifanya nini?

Tulikuwa na sherehe Kanisani, je sijakujulisha kwamba mimi nafanya utafiti kuhusu wanadini?

Joji alifunga simu na kujitupa kitandani kwa mshangao wa tukio hilo, na kujikuta yupo mapokezi akimtafuta Omela, na hakumkuta, alimuuliza muhudumu wa hoteli wapi alipo, alitabasamu na kumjulisha kwamba leo ana oda nyingi, na yeye ameelekea muda mfupi chumbani kwa mtalii wa Kichina.
Joji alimuliza kwa sauti ya kufoka!

Nini wanafanya?!

Alijibu Hahahaa, nitajuaje mimi?

Joji alijihisi vibaya kwa swali lake, na kujikuta mwenye wasi wasi sana, hajui la kufanya…alipanda kwenda chumbani kwake…Nia yake kubwa kwa muda huo ni kutaka kumuonyesha Katarina kwa njia yoyote ya malipizo kutokana na hiyana yake, aliamua kuwasiliana na Maiko ili amletee wasichana wawili wazuri aliowaona pale Kafeteria, lakini alisema na nafsi yake ya kwamba: Achana na mambo hayo hayatakunufaisha shikamana na misingi ya tabia yako na usiwe kama Kakhi au Tom, na fikra nyingine ikimwambia, ‘Hii misingi ya tabia yako imekupa faida gani…..hakuna kitu?

Hallo…Maiko

Hallo Joji, umenishtua, sio kawaida yako kunipigia simu muda huu.

Joji alizinduka na kuangalia saa na kukuta ni saa saba na nusu.

Samahani, sikutanabahi kama muda umekwenda hivi bali nimetamani kukujulia hali tu na huenda nitakupigia kesho, asante Maiko.

Nashukuru kwa simu, tutawasiliana kesho.

Joji aliendelea kuwaza kwa hasira pale chumbani kwake na baadhi ya matusi na laana zikimtoka hajui la kufanya, shaka na wasiwasi kwa mke wake zimedhoofisha haiba yake….Alitaka kulipizia kwa Omela, bahati mbaya hakumpata, mwishowe mtu mwingine alifaulu kumpata Omela. Mtu asie na kasumba kama yeye na asiye mkakamavu na misingi ya tabia ambayo inatufanya turejee nyuma na kufikiri mara nyingi, na wanakuja wengine na kupatiliza fursa kwa anasa na uzuri.
Na kwa wakati huo Joji akakumbuka siku za nyuma Katarina na Tom walipokesha, na kufungua intaneti na kutafuta ukurasa wenye picha za Tom za zamani na kukuta ameweka picha za mkesha wa ukurasa wake na picha hizo zinaonyesha kufanana na hafla ya hivi karibuni; zinazojulisha sehemu ile ile, ambayo huenda ikawa ni kanisani, kisha akajiuliza: Ni kanisa gani hili lenye kuruhusu upuuzi huu!!
Kisha akakumbuka alivyoishi na mkesha huo uliopita. Na ni kwa namna gani Baraad alipotaka kumfanya ‘teja’, hapo alikumbuka maneno ya Adam, “Laiti ungeshinda mambo yako ya msingi na kutatua matatizo yako kwa njia bora, nafsi ingekuwa ni imara zaidi kutatua mazito” na kauli yake ni kuwa, “Usiweke shaka yako ndio dalili ya kumtia hatiani pengine kuwa kwake na Tom ni kwa ajili ya kumlingania kwenye Ukristo”. Na usia wake mwingine kwake ni “Angalia au zingatia mambo muhimu ili nafsi yako na maisha yako yawe ndio jibu la matatizo yako kwa urahisi, na wakati huo utapata furaha na kumaliza yanayokusibu.” Na kauli yake ni: “Jaribu kutangamana na Katarina pamoja na Tom kwa njia ya kawaida, kwani wewe hivi karibuni utakuwa ni mwenye kusafiri kuelekea India na kurudi kwako utahadithia kila tukio, na hakikisha unayachukulia mambo kama yalivyo (kama kawaida) bila huzuni, na kwa furaha bila hasira.” Joji alijiuliza mwenyewe: Hivi Adam yupo pamoja na Katarina, au anamtetea kwa vile ni mtu wa dini kama yeye? Nitawasiliana nae ili niangalie nini anachonificha mtu huyu!!

Hallo, nani mwenzangu?

Ni mimi Joji kutoka India.

Naam karibu mmagharibi kutoka mashariki, vipi hali zenu?

Ni katika hali mbaya, Katarina amekesha usiku wote mpaka asubuhi ya leo pamoja na Tom.

Umethibitishaje hilo?

Kupitia Tom mwenyewe, kwa sababu ameweka picha yake katika mtandao wake unaweza kufungua na utaona picha ya Katarina.

Ni nini kigeni? Je ulihakikisha kuwa alikesha nae mara iliyopita?

Naam, lakini…..

Ok, muhimu utafanya nini? Usiwe dhaifu mbele ya shaka na kuchanganyikiwa, angalia malengo yako ya safari, iwe malengo ya kikazi au malengo ya kutatua maswali yanayo kuzunguka.

Natamani nilipize kisasi kwa Katarina kwa njia yoyote ile.

Nimekueleza tangu mwanzo, usiachie mtu akuchezee pindi unapokuwa katika hali ya udhaifu na kuchanganyikiwa kwako, narudia tena kukueleza, tukiwa katika hali zetu za udhaifu, tunashindwa kushikamana na msingi yetu. Na pale tunaposhikamana na misingi yetu tunazidi kuwa na nguvu.

Nitastarehe na msichana wa Kihindi na zaidi yake, na nitamtumia picha hizo ili kuumiza moyo wake kama alivyoniumiza mimi.

Wewe kwa hili utakuwa unaunguza moyo wako tu, na kisasi cha aina hii ni pigo kwa watu dhaifu, na utaidhuru nafsi yako na utu wako zaidi kuliko utakavyo muumiza Katarina, na inawezekana asidhurike kwa hilo. Yeye amekusaliti na Tom ni nani mwenye madhara zaidi yeye au wewe?

Ni mimi.

Hapana bali yeye ndie alieharibu dini yake na heshima yake, na wewe haikudhuru chochote. Lakini kwa upande wangu pengine isiwe kama unavyofikiria.

Kwa nini unamtetea? Au ni kwa vile ni mwana dini kama wewe?

Sifikirii kama ana maadili ya dini kama ana kusaliti kama unavyosema, na hata kama itatokea hivyo, na kama hajakusaliti hilo suala jingine, kisha kwanini mimi nimtetee hali mimi simjui kabisa? Na sikujua kama ana dini ila kupitia kwako sasa hivi, na wewe ulikuwa unasema anakunywa pombe na kukesha tu, na hukuniambia kwani mwanadini, kisha nina maslahi gani katika hilo? Pia wewe ndio ulioniambia na sio mimi niliekupigia simu!

Samahani Adam, sio nia yangu kukuudhi, ila nimefedheheshwa sana, na nimeamua kumuonyesha Katarina kwa kutembea na Omela.

Najua sio lengo lako kunidhalilisha ila mashinikizo yasituhamishe katika misingi yetu, na ni nani huyo Omela?

Ni msichana mrembo alienitaka nikamkataa na sasa namtafuta sana ili niwe nae kwa sasa.

Na kwa nini ulimkataa?

Si kutaka kuchafua utu wangu kwa matamanio… au kwa kuwa mjinga na mpumbavu!

Kwa hiyo sasa unajiandaa kudhalilisha utu wako?!

Nifanyaje sasa?

Rudi katika utu wako, na tafuta majibu kwa matatizo yako makubwa, tembea katika njia ya furaha, na utafika na kushinda mitihani yako.

Mimi nitarudi London baada ya siku mbili na ni muhimu kukutana nawe.

Nakusubiri:

Joji alimaliza maongezi kwa kukata simu hali ya kutojua nini anakifanya, alifungua kompyuta yake ili afungue ukurasa wa face book wa Adam, na hapo alikuta katika hali ya kawaida kabisa, makala zake ni ndefu, naye Joji akiwa katika hali mbaya ya kinafsi isiyomruhusu kusoma makala kama hizi, mara ghafla macho yake yakageukia makala yenye kichwa cha habari: “Somo kwa ajili ya rafiki yangu anaefuata furaha.” Aliandika Adam makala hayo kabla ya siku nne…

Somo kwa rafiki yangu mwenye kutafuta furaha: Nimefahamiana hivi karibuni na mtu mwenye misingi bora anaetafuta faraja kwa yale yaliyompata, naamini ni mkweli katika utafiti wake, lakini msongo wake ni mkubwa, nimemfahamu kupitia kisa chake hicho na nimependelea nikushirikisheni kwa faida zifuatavyo: Mwenye kutafuta furaha ni juu yake kufuata njia yake; na haiwezi kufikiwa furaha hiyo kwa mali, cheo au kurithiwa, na ili afikie furaha hiyo hakuna budi kujituma na kudumu ili kuifikia. Hatafurahi kabisa au kuwa mwenye furaha mtu ambaye hatajibu maswali makubwa: Nani katuumba? Kwa nini ametuumba? Kwanini tunaishi? Na mwisho uko wapi? Na mtu ambaye hatayapatia ufumbuzi maswali haya, hatapata katu furaha ya milele. Baadhi ya watu wanatia uzito na ugumu njia ya furaha, halafu wanasema: hatutavuka vikwazo hivi, na laiti wangerahisisha mambo wangefikia katika furaha kwa wepesi zaidi. Baadhi ya watu wanasahau malengo yao kwa matatizo madogo na malengo madogo ya karibuni, na wakati huo wanaishia kati kati ya njia bila kufikia kabisa malengo ya furaha. Haifai kukatisha misingi yetu njiani, kwani misingi ndio minara yetu kuu ambayo hatupaswi kuivuka, na mwenye kutaka kuivunja atavunjika mwenyewe, na minara itabaki bila kubadilika. Mtafiti anapokuwa mkweli na nafsi yake, akajituma na akadumu na kusubiri, basi atapata uwepesi katika mambo yatakayomfungulia njia. Somo bado ni kubwa na nitaendelea na makala hayo kipindi kijacho pengine itakuwa karibuni. Ni mimi: Adam.

(3)

Baada ya Joji kusoma makala ya Adamu alikuwa mbali huku akijiuliza kwa mshangao: Kwa nini Adam ameandika habari zake na hakumfahamisha jambo hilo, wala hata hakuashiria jina lake? Na Adam hajaenda kinyume juu ya yale aliyoniambia, alikuwa muwazi kwangu lakini hakujali hisia zangu wala hali yangu ya nafsi! Katika hali hii nikipata kidonge cha Heroin au nikipata wasaa wa kumpata Omela nitasahau yote niliyokuwa nayo, na kusahau ni njia ya kuelekea katika furaha…ah, je ni kweli njia hizi ni kimbilio la matatizo au ni suluhisho sahihi wanalotumia watu wapevu ambao hawapotezi fursa yoyote? Ama kweli nipo katika mtanziko!
Simu iliita chumbani, alinyanyua mkono wa kujibia, upande wa pili wa simu alikuwa mhudumu katika mapokezi, akimjulisha kuja kwa Omela…

Je una muhitajia aje kwako?

Joji alitulia kitambo kirefu hajui la kumwambia…

Sijui!

Nini?

Nashuka kuja kumuona sasa hivi.

Alishuka mapokezi huku akijiuliza: Je kushuka kwake ni kumlipizia Katarina au kujimaliza mwenyewe, kama anavyodai Adam? Je awatii Kakhi na Tom? Au amtii Adam? Wakati akiwa katika lindi la maswali hayo yasiyokuwa na majibu, ghafla lifti ikawa imesimama mkabala na mapokezi, na alipofungua mlango ghafla Omela amemsimamia mbele yake na mara tu alipomuona alitabasamu kwa furaha kubwa lililofanya uso wake mzuri kuzidi kung’aa na kuzidi kupendeza.

Karibu Omela, unaonaje tukakaa pale kwenye kiti kile?

Haa haa, hamna neno.

Mara baada ya kukaa tu Omela alianza kutabasamu..

Nimejihisi mwenye furaha kubwa pale mhudumu aliponileza unanihitaji.

Kwa nini?

Kwa sababu nilihisi umenidhalilisha pale uliponikataa, na sikuwa mwenye mvuto kwako.

Sijakudharau bali nilikushukuru, na sikukuambia wewe sio mzuri, bali wewe ni mzuri sana kama jina lako lilivyo.

Kwa nini hatukai chumbani tukastarehe pamoja ikiwa ….kisha alimkonyeza.

Nataka tuongee kwanza.

Juu ya nini? Au tuongee nini?

Je inawezekana nikuulize maswali mepesi lakini yenye maana kubwa kwangu? Na naomba uwe mkweli na muwazi sana kwangu.

Usijali nitakuwa mkweli kwako, ila sijajua kwa nini unanipelekea huko?

Je wewe ni mwenye furaha na maisha yako?

Kimya kilitanda kwa Omela huku akitafakari na kutazama chini….

Nimekuahidi kuwa mkweli na sitokuficha kitu na kwenda kinyume na ahadi yangu, japokuwa sikutegemea kukutana na swali hili, ikiwa furaha hiyo unayoizungumza ni kwa maana ya kucheka, kutabasamu, kucheza, kuwa na mali pamoja na uzuri, basi kwa hayo mimi ni mwenye furaha kubwa.

Nakusudia ndani ya moyo wako je unajisikia furaha? Kwani baadhi ya watu wanacheka lakini ndani ya mioyo yao kumejaa huzuni kubwa.

Nimekuahidi ukweli kana kwamba umeingia moyoni mwangu kabisa, na mimi najiepusha na huzuni za ndani kwa kutafuta mali, kucheka, kucheza na kufanya mapenzi ili niepukane na huzuni iliyo ndani ya moyo wangu.

Ni zipi sababu za matatizo na huzuni hizi pamoja na uzuri ulionao, mali na afya njema bali na hata kustarehe pia?

Sijui, huenda ni maisha ya hovyo ninayoishi, kwani maisha yangu hayana thamani kabisa.

Je unatafuta maana ya maisha yako? Au maongezi haya hayakuhusu?

Hapana, kwa hakika ni vigumu kupata majibu, majibu maana yake ni kupata furaha, nami sistahiki.

Kwa nini hustahiki?

Kwa sababu mimi ni mdoli watalii wananichezea, na mimi nawachezea kwa ajili ya starehe ya mpito tu.

Na kwa nini umefurahi pale uliposikia nakutafuta?

Kwa sababu mchezo wangu wa kukutega umeshindwa, nami sijazoea kupoteza na kupata hasara maishani mwangu milele.

Unajua kwa nini nilikuwa nakutafuta?

Hapana kisha akatabasamu na kusema: Usiniambie ulikuwa unanitafuta ili uniulize maswali haya?!

Hapana sio kwa ajili hiyo, bali ni kwa ajili ya kushuku kuwa mke wangu ananisaliti na nikaamua nimlipizie kwa kustarehe na wewe.

Haa haa alicheka kidogo kwani sijakwambia kuwa mimi ni mdoli tu wa kuchezewa tu kwa muda, unamlipizia mkeo kwa hila zangu za mpito, kweli mimi ni duni?!

Nisamehe, bali wewe ni mzuri wa kupindukia, lakini kwa upande wangu, utu wangu ulikuwa unanizuia kufanya mambo kinyume na heshima yangu.

Na kwa sasa ni penzi la kisasi umesahau utu wako! Mimi ni rahisi kiasi gani katika macho ya watu!

Samahani, sina nia ya kukudhalilisha ila hii ndio kazi yako unayoifanya.

Wewe hujasema ila ukweli tu! Wakati mwingine mwanadamu hajijui mwenyewe na kwa hakika nimebakisha wiki mbili kutimiza miaka miwili nafanya kazi hii, na hakuna mtu alienirudisha nilipomsogezea nafsi yangu, na mara ngapi nilijihisi mzuri machoni mwao. Na baada ya kumaliza haja zetu naondoka, na wewe ndio mtu wa mwanzo kuniweka wazi kwa hili, akanifanya kupambana na nafsi yangu.

Samahani. Narudia kusema, sio nia yangu kukudhalilisha au kukutia kasoro.

Huenda…lakini ukweli ndio huo!!

Una maana gani?

Mara nyingi tunakimbia nafsi zetu na tunaogopa kuona uhakika wake.

Sijafahamu!

Joji alinyoosha mkono wake na kushika mkono wa Omela na kumvuta upande wake, lakini Omela aliondoa mkono wake kwa upole huko macho yake yakitoa machozi na kusema:

Kucheza na kukimbia maisha ni uovu kwa vyovyote utakavyo onyesha ushupavu.

Achana na hayo nisamehe kwa yale niliyotamka.

HaaHaa. Je utaachana na mipango yako ya kumlipizia mkeo.? Sina thamani kiasi hiki!

Nini unataka? Je unakusudia kukataa kupanda juu kwa ajili ya kustarehe mimi na wewe ili tuondokane na huzuni zetu?

Ndio, mara hii mimi ndio sitaki.

Ni ipi dini yako?

Sina dini mimi, na je kuna mwenye dini ya kweli anaefanya mambo mfano wangu?

Mke wangu ni mwanadini, lakini ananisaliti na mtu mwingine!

Ama dhana na shaka yako si kweli, au yeye anasema uongo na unafiki hali ya kuwa hana dini, au anajinasibisha na dini mbaya, hivi inaingia akilini niwe na Mola ananiona na kunihesabu halafu niwe nawinda wanaume? Jua ya kwamba baba na mama yangu ni mabudha, lakini mimi nimeachana na ubudha kwa utata wake na ugumu wake wenye kuchukiza kwa hiyo nikawa bila dini.

Vipi unaishutumu dini ya wazazi wako?

Hiyo ni dini yetu tuliyoianzisha na kuibadilisha kama tutakavyo. Kwa hivyo ukitaka unaweza ukasema hakuna dini ya Budha kwa sababu hiyo ya kubadili badili! Bali sheria zote zilizobadilishwa zinatokana na sheria za dini zilizopita kwa hiyo mabadiliko na uzushi huo hata kama ni mbaya hauna kikomo…nitaondoka hapa hotelini na huenda nisirudi tena.

Kwa nini usirudi?

Sitarudi mpaka nione sababu inayonipa maana ya maisha yangu na kunifanya niheshimu nafsi yangu, nakushukuru sana kwa mara nyingine tena.

Wapi unaenda sasa?

Omela alisimama na kutoka bila kujibu swali lake.

(4)

Joji aliamka hali ya kuwa amechelewa kuwasiliana na Maiko… alimuitikia kwa sauti nzito yenye mikwaruzo iliyochoka..

Je bado umelala? Una nini? Umelala na kuamka umechelewa, je hayo umejifunza kwa Kakhi?

Achana nae nina siku na nusu hapa India nimebakisha, kwa kitu gani utaniusia?

Kuna bustani nyingi, makanisa, nyumba za ibada, makumbusho na masoko….katika hayo unataka kutembea wapi?

Bora makanisa na nyumba za ibada.

Usisahau kutembelea kanisa la Saint James kwani zuri na maarufu.

Na vingine? Je kuna sehemu za ibada za Waislamu, Wahindu na wengineo?

Ijapokuwa sipendi, ila msikiti mkubwa uliopo Delhi umejengwa kwa miaka sita ni mzuri na wenye mandhari nzuri ya kuvutia.

Nakushukuru nitapata kwanza kifungua kinywa kisha nitatembelea sehemu mbili hizi.

Kabla hujamaliza chai nitakuwa nimeshafika hapo hotelini.

Usisumbuke, nitachukua taxi.

Haa Haa, sio hongo hii, tumeshamaliza kutiliana sahihi mkataba, nitakuwa hapo baada ya nusu saa.

Kabla Joji hajamaliza chai yake na huku akijaribu kusahau kusalitiwa na mke wake, pamoja na maongezi yake na Omela na kuhusu kumuhadithia shaka yake kwa mkewe, ghafla alipigiwa simu na Maiko akimjulisha yupo mapokezi, alimalizia chai yake na kwenda kuonana na Maiko…walisalimiana na walichukua gari kuelekea kanisani.

Jana nilikukumbuka nilipokuwa ninaongea na mhudumu wa kihindu wa hoteli.

Nini wamekuambia kuhusiana na mimi?

HaaHaa, nilikumbuka maneno yako kuhusu Jiyostana mbudha, siku hiyo ulinieleza kuwa lau nitakaa nae muda mrefu sitotamani tena kurudi India karibuni!

Haa haa, kweli…kweli dini hizi zilizoanzishwa na watu katika zama za ujinga, kila moja ikija kutatua shida za wafuasi wao, au kuleta haki na usawa katika tabaka fulani kwao, lakini kwa mtazamo wa leo zimekosa thamani…Achana na dini hizi ili nikufahamishe kuhusiana na kanisa la Saint James ambalo tutalifikia muda sio mrefu, kanisa hilo lilijengwa na James Skinner mwaka 1836 C.E. ni kanisa kongwe katika sehemu hii, lina mandhari ya kipekee na uwanja wake ni katika viwanja vizuri kabisa.

Umesema ni kanisa kongwe katika sehemu hii?

Ndio, ni karibu miaka 200 hadi 300 hivi.

Na kabla ya miaka 300 hakukuwepo na Ukristo India ?!

Ukristo nchini India umekuja kwa njia mbili: Njia ya kwanza ni: njia ya Mtume Tom katika Injili ya Yohana naye ni mmoja katika mitume kumi na mbili wa Masiya katika karne ya kwanza ya A.D Na njia ya pili ni: njia ya kimishionari wa Kimagharibi kati ya mwaka 1500 mpaka 1975 A.D ni dini ya tatu India baada ya Uhindu na Uislamu, na idadi yao inafikia 24 milioni.

Tu, ni idadi ndogo ukilinganisha na wakazi wake.

Ndio idadi yao ni kama asilimia 2.3 na kwa idadi hii tu kuna maandamano ya hasira yanayofanyika mara kwa mara kuhusu kuongezeka idadi ya wakristo, wahindu wanahisi kuwa ukristo unapewa nguvu sana kwa mali inayotoka nje.

Na je ni sahihi watu kuingizwa kwenye dini kwa mali?

HaaHaa kwa kiasi fulani mpaka watu waondokane na itikadi mbaya za Kihindu.

Joji na Maiko walifika kanisani na kushuka ndani ya Kanisa wakiangalia kwa mazingatio; uzuri wa jengo, picha, pamoja na masanamu na minara yake, kweli ni nzuri, wala hakukuwa na alama ya Ibada hapo ni kana kwamba ilikuwa ni alama kuu ya Kihistoria tu. Maiko alikuwa akilisifia kanisa hilo kwa Joji kwa sifa nyingi mpaka walipomaliza ziara yao, wakapanda gari, hapo akamwambia:

Nini rai yako?

Linavutia kweli.

Je sijakueleza hivyo? Sasa tunakwenda wapi?

Tumekubaliana tunakwenda Msikiti wa Delhi sasa.

Vizuri! Japo sehemu hiyo Siipendi lakini twende kwa ajili yako.

Kwa nini huipendi?

Waislamu sio watu wazuri ni wabaya sana.

Vipi? Je wamewalazimisha watu kuingia katika dini hiyo kwa nguvu?

Ukweli, hawajawalazimisha watu kuingia katika dini yao ya watu ambao hawajastaarabika.

Kwani wamewarubuni kwa kuwaingiza kama Wakristo?!

Najua lengo lako lakini hili pia sio.

Watu wameikubali vipi dini hii?

Oh, watu wameikubali dini hii kwa njia ya wafanya biashara wa Kiarabu waliokuja India kufanya biashara.

Yaani watu waliingia katika Uislamu kwa maingiliano na wafanya biashara wa Kiarabu, kwa mapenzi yao tu, na sio kulazimishwa!.

Ni kweli kwa bahati mbaya, ni rahisi kuwadanganya watu na kuwachezea, kwa ajili ya kukikimbia tabaka la chini la wahindu lenye chuki watu wakaingia katika Uislamu walipoingiliana kwa mara ya kwanza na wafanyabiashara wa Kiarabu, kisha baada ya hapo wakaja tena kwa njia ya vita.

Vita?!

Ndio, vita vya kwanza vililetwa na mtu anayeitwa Muhammad bin Qaasim Athaqafii katika mwaka 700 hivi A.D.

Takriban ni kati ya miaka 1500 hivi!

Waliongezeka mpaka ikawa ni dini ya pili nchini India.

Ni ngapi idadi yao?

Ni zaidi ya watu 180,000,000 ni sawa na asilimia 14.5 ya wakazi wake.

Ni idadi kubwa! Na hii inamaanisha kama Pakistani na Bangaladesh hawakujitenga pengine wengi wao wangekuwa ni Waislamu.

Ndio, lakini walihisi kudhulumiwa na Wahindu na kuanza mapinduzi yaliyopelekea Pakistani kujitenga, hapo alitabasamu na kusema: Hii ni bora kwetu, kwa hakika Waislamu walitawala India kuanzia mwaka 1001 A.D na utawala wao ulidumu kwa miaka 300 hivi.

Je waliwalazimisha watu kuingia Uislamu kwa muda huo?

Hapana, ila walikuwa ni madhalimu, walijenga majumba makubwa ya kifahari kati kati ya watu maskini na wanyonge.

Aliniambia hayo Mutwi Rahman tulipokuwa katika ziara ya TajMahal!

Hayo ni katika uadilifu wa Mutwi Rahman, waliwadhulumu watu riziki zao ijapokuwa hawakulazimisha watu kuingia katika dini yao, kwa kifupi kila tawala zilizotawala India zilidhulumu na huenda Uislamu ulikuwa na uadilifu kidogo nchini India kuliko ushirika wa Wahindu na Waingereza waliouita Ushirika wa Wahindi wa Mashariki na uharamia wa wazungu. Waislamu na wahindu walikuja juu sana na kuwa kinyume nao.

Kwa maana hiyo Wahindu walipenda hukumu ya Kiislamu?

HaaHaa, kwa masikitiko ndio, walikubali na hawakuwa wote ni madhalimu, isipokuwa dhulma ilitokea mwishoni mwa utawala wao, kama walivyokuwa watawala wa Kiislamu (pamoja na dhulma yao) walikuwa ni bora kuliko shirikisho la Wahindi wa Mashariki na Waingereza ni mategemeo yangu halitakuudhi hilo.

Historia inaandikwa kama ilivyo, na sio kama tunavyotaka.

Mapinduzi ya Waingereza yaliendelea mpaka walimteka mtawala wa Kiislamu na kuua wanae, na wakavileta vichwa vyao juu ya meza ya chakula, halafu wakaupiga vita Uislamu na kutupilia mbali mafundisho yake na kupora utajiri wa Wahindi.

Unyama ulioje huu…ziko wapi haki za binaadamu?

Haki za binadamu huenda tukazisikia tu katika mikutano na vikao. Ama uhalisia wake ni kitu kingine. Muhimu tumekaribia msikiti ambao ulikuwa ni makao ya mikutano ya Kimapinduzi dhidi ya Waingereza, na sehemu hii palitolewa wito wa jihadi kutoka kwa wanachuoni wa Kiislamu, na kwa wito huo watu walijiandaa baada ya hapo…na unaitwa msikiti wa Jihan Nama au msikiti wa Jamah, na ujenzi wake ulichukua muda mrefu na kukamilika mwaka 1656 A.D Mfalme wa Munguli ‘Shah Jihaan aliamrishwa ujengwe, ni katika misikiti mikubwa barani Asia unatosha watu 25,000 wenye kusali.

Basi ni Msikiti mkongwe!

Huenda, ni jengo zuri limejengwa kwa staili ya kiManguli lenye minara mitatu na ni hilo hapo mbele yako tumeshalifikia.

Walishuka wakaangalia uzuri wa jengo lake. Na Maiko alikuwa sio mwenye kufurahia usifiaji wa Joji. Joji alifanya haraka haraka kuliangalia jengo ili kuheshimu hisia za Maiko ambaye alikuwa mpole pamoja nae.

Je ungependelea kwenda sehemu nyingine.

Nashukuru, huenda muda umekwenda sana.

Lakini bado hujafanya uadilifu!

Kwa nini?

Umetembelea kanisa na msikiti, na hujatembelea sehemu ya ibada ya Wahindu!

Nilikuwa nataka kufika huko, ila nahisi kama nakusumbua.

Sehemu hiyo ipo karibu na njia yetu, je utapenda kuona sehemu hiyo?

Bila shaka, ikiwa haitakuchelewesha shughuli zako, ila mimi safari yangu ni kesho na nitakuwa na faragha kwa ajili ya kufunga mabegi yangu na sitatoka sana..

Jina la hekalu la Wahindu ni Akshardam, hutembelewa kila siku na maelfu ya wakazi na watalii wa kimataifa, nalo ni hekalu kubwa kabisa la Wahindu katika Delhi, ujenzi wake ulianza mwaka 2000 A.D na kukamilika mwaka 2500 A.D, nalo ni hekalu la kisasa lenye kupendeza, wameweka nakishi ya miungu yao kwenye kuta.

Je wamenakishi wanyama na wengine?

Haahaa, ndio, walichorwa miungu yao, mfano wa wanyama na wanawake wachezaji dansi, bali kuna zaidi ya masanamu 20,000, kwani sikukuambia kuwa dini hizi za watu zinachekesha, inavyoonekana kila walipokuwa wakipendezwa na kitu wanakifanya Mungu. Wewe upo katika nchi ya maajabu, kuna waoabudu panya na wana sehemu zao za ibada na kuna wanaoabudu nyoka na wana sehemu zao za hata hivyo tumeshawasili katika jengo lenyewe la Wahindu.

Yaelekea ni jengo la kuvutia sana.

Sahihi, hakika imejengwa kwa mawe, hawakutumia matofali au kokoto na limepambwa kwa mapambo ya thamani kubwa tushuke tuangalie kwa haraka ili tusichelewe hotelini.

Joji alipendezwa sana na jengo hilo, lakini alijihisi kuchefukwa kwa kuona masanamu mengi, walizunguka lile jengo kwa haraka, na katika njia ya kurudi..

Jengo zuri, lakini wingi wa masanamu ni kitu kinachochefua!

Ndio, umesema kweli.

Cha ajabu hata kanisani kuna masanamu, ama msikitini hakuna masanamu ndani yake!

Lakini sanamu la kanisani ni la Yesu na sio la wanyama.

HaaHaa, umesema kweli, pamoja na yote hayo na kushukuru, safari yetu ya leo ilikuwa nzuri sana.

Kutokana na kuzama na safari yake ya leo, Joji alisahau kidogo maudhui yake na Katarina pamoja na Tom kidogo, na alijihisi utulivu na raha, inaonekana kama vile alichoambiwa na Adam kilikuwa sahihi: Kwamba: “Zingatia mambo yako muhimu….” Safari yake hii ilikuwa ni hatua mojawapo mbele kufikia furaha, kwa hakika dini zilizoanzishwa duniani haziwezi kujibu maswali yake; vipi litajibu wakati chenyewe kinakikosa, yenyewe inajibadilisha mara kwa mara kulingana na mazingira, ili kufikia utulivu wa kidini unaotarajiwa na watu.
Ilimjia fikra kumuandika Adam ujumbe, alifungua kompyuta yake na kumwambia:

“Rafiki yangu Adam… Nakushukuru kwa nasaha zako, pia nisamehe kwa mazungumzo yangu mabaya. Umesema kweli: Kwa hakika nimefaidika kwa nasaha zako sana. Nimeshinda jaribio langu la kutaka kulipiza kisasi lililonitawala. Kwani nimejishugulisha zaidi na mambo muhimu na kuachana na mambo madogo madogo, kwa hakika nimeendelea kujishughulisha kwa siku yote nzima, na ninaweza kujibu swali lako na la dokta pia kwa uwazi zaidi. Dini za duniani hazijibu swali lolote; hizo ni rai tu za watu ambao hawakutuumba, basi vipi watajua kwa nini tumeumbwa?.....Narudia shukrani zangu kwako na mimi kesho narudi, nitafurahi kukutana nawe nakushukuru kwa mara nyingine. Ni mimi rafiki yako Joji.

Kisha baada ya hapo alijilaza kitandani akifurahia siku yake kwa kushughulikia malengo yake makubwa..

(5)

Joji aliamka mapema akaoga… aliangalia saa na kukuta bado masaa manne kuelekea uwanja wa ndege, akajisemeza ‘nitaangalia nini ninachoweza kufanya katika masaa haya’, lakini kwanza nipate chai…
wakati akiwa amekaa katika meza ya chai, mara akamuona yule mhudumu wa KihinduKapoor aliyeongea nae jana na kumuita…..

Kapoor akaseme, Karibu Mheshimiwa.

Na wewe karibu, nilikuchelewesha muda uliopita, lakini nina maswali nataka kukuuuliza kama una muda kama utakubali (kama hutajali)?

Hakuna tatizo, inaonekana una hamu ya kuwajua Wahindu… na huu ni mtindo mpya wa watu wa magharibi.

Na je Uhindu ni mtindo?!

Naam, Uhindu na Ubudha ni model huko kwenu Ulaya na Marekani, wanakuja huko kukimbia maisha mabaya ya kimaada yenye kumfanya mtu ni chombo au mashine ya kulimbikiza na kukusanya, wanakuja huku wakitafuta maisha ya kiroho na tabia na hawajui zaidi ya hapo.

Vizuri sana. Lakini nataka nikuulize swali; Je wewe na Wahindu wengine mnayo furaha kwa ujumla?

Huenda Mabrahma ambao wanawakandamiza watu ndio wenye furaha, hata hivyo sidhani kama ni sahihi. Ama kwa upande wangu mimi ni Shudhra ni mtumishi tu, huu ni katika upande wa kitabaka, ama kwa upande wa imani, sisi tunaikimbia imani yetu na wingi wa miungu wetu kushughulika na mambo ya kiroho na kitabia zaidi na kujivua na dunia na Mungu pia, kwani hujasikia kuhusu Ghandi?

Ndio, alikuwa mtu safi.

Alitaka kuasi Uhindu kwa hivyo wahindu wenye kasumba wakamuuwa.

Na kwa nini alitaka kuasi dini yake?

Kwa sababu alisema haiwezekani kuishi sawa sawa kwa imani yetu kamili, samahani huenda ni kwa (kulingana na mtindo huu) umevutiwa na Uhindu na mimi nakuharibia hilo.

Na kwa nini usibadili dini yako?

Mimi nimezaliwa na wazazi wa Kihindu…kisha alitabasamu akasema: Sitaki kuwa Ghandi mwingine.

Je utachukua zawadi hii ya pesa kwa sababu nimekupotezea muda wako mwingi?

Asante, nakushukuru.

Joji alienda chumbani kwake akaanza kukusanya mabegi yake, wakati anajiandaa simu iliita, upande wa pili alikuwa Karimullah….

Oh! Joji, mimi ni Karimullah.

Oh! Karibu, Karimullah.

Nimekuja jana sijakukuta nilitaka kukusalimia, niliacha mkataba wenye muhuri pale mapokezi kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini India, kama tulivyo kubaliana una safiri lini?

Asante sana,. Nilitaka kuusahau nitauomba sasa hivi, safari yangu ni baada ya masaa mawili…

Je ungependa nikupeleke au nikusindikize mpaka uwanjani?

Nashukuru, ila nimekubaliana na Hoteli wanitafutie gari.

Ok, sawa, nasubiri kopi ya mkataba kutoka Ubalozi wa India London wenye muhuri. Kwa heri.

Joji alirudisha mkono wa simu, na akawasiliana moja kwa moja na mapokezi akitaka kuletewa nyaraka zake…aliweka simu na kufikiri: Kwa nini hafurahishwi na Karimullah ijapokuwa hakuwa na kasoro anayoiona kutoka kwake, je ni kutokana na kufanana na bin Laden? Au ni kwa sababu ya umahiri wake katika kupatana? Au kwa ajili ya maneno kuhusu Mkurugenzi wake Kakhi? Au ni kwa jambo lingine asio lijua? Ni fikra za ajabu….au ni kwa vile sijasahau ulipuaji wa Treni mjini London Au ni kwa ajili labda ya athari ya vyombo vya habari? Cha msingi ni kuwa sifurahishwi na nae wala sijui ni kwa nini.
Aliacha kuwaza pale nyaraka zake zilipoletwa kutoka mapokezi…alizigeuza geuza na kuziangalia na zote zilikuwa sawa bila upungufu kama anavyotaka. Na hakuna kilichobakia isipokuwa muhuri wa Ubalozi wa India London. Aliangalia saa yake akakuta wakati wa kuondoka kwenda uwanjani umekaribia.
Aliwasiliana na mapokezi kwa ajili ya kujiandaa kutoka, na akawataka wawahishe gari nusu saa kabla ikiwezekana, ili kuepukana na foleni njiani au jambo lolote lisilotarajiwa.
Joji alikuwa akiangalia barabara za India kupitia dirishani, njia nzima imejaa masanamu, na alikuwa akijiuliza: Siwezi kuabudu au kutafuta ufumbuzi wa maswali yangu kupitia mawe na watu…naishukuru India iliyoniongoza katika njia ya kwanza ya safari yangu kuelekea kwenye furaha, ilikuwa safari yenye vivutio na starehe pamoja na yote niliyoyapitia.