NI KIPINDI CHA UGAIDI NA MISUKOSUKO

NI KIPINDI CHA UGAIDI NA MISUKOSUKO

NI KIPINDI CHA UGAIDI NA MISUKOSUKO

(1)

Joji alirejea kutoka India, ni safari iliyokuwa nzuri sana, iliyojaa mafunzo, majadiliano na maswali, na haikuwa ni safari yake ya kwanza kikazi, lakini pamoja na hivyo ni safari iliyokuwa na mafanikio makubwa, ndio safari iliyofunga mikataba mikubwa kwa haraka zaidi.. na India ni miji ya kuvutia. Alipokuwa kwenye ndege aliitafakari sana safari yake kwa kina, kwa mapenzi yake na nchi ya India pamoja na watu wake, ila alichukizwa na kuwepo kwa itikadi mbaya za dini, huku akijiuliza: Hivi kupenda India ndio suluhisho la maswali yake? Au ni kwa ajili ya Katarina mwenye asili ya India? Lakini haijapita muda alirudi katika hali yake ya kawaida, na jeraha lake kwa Katarina bado halijafutika katika moyo wake.
Ndege iliwasili London na kukusanya mizigo yake, na kuelekea katika ukumbi wa mapokezi, na ghafla akaonana na Katarina pamoja na watoto wake waliokuja kumpokea, alijisikia ni mwenye furaha kupita kiasi huku akicheka na kucheza cheza na familia yake njiani…..

Hujatueleza..mpenzi wangu, vipi India?

Ni mji mzuri pamoja na watu wake ni wazuri pia.

Huu ni uzuri wa macho yako.

Kweli, ilikuwa ni safari nzuri maishani mwangu.

Vizuri, nini umekipenda kupitia safari hii?

Kila kitu kilikuwa kizuri, na cha ajabu hakuna hata kitu kimoja nimekiweka kichwani katika safari hii, na kwa nini? labda huenda kwa wema wa watu wake, au huenda ni kwa ajili yako mpenzi wangu…au labda ni kwa ajili ya kutiliana saini na kampuni kwa haraka zaidi sijui kwa kifupi tu nimevutiwa sana na safari hii

Alimgeukia mwanae Maiko…

Unajua? Unanikumbusha Maiko wa India unafafana nae sana, halafu akatabasamu na kusema: lakini wewe mwanangu ni zaidi yake kwa uzuri…Ila wewe Sali, unanikumbusha uzuri wako sawa na uzuri wa Omela.

Muda ulikwenda sana mpaka walipofika nyumbani kwao, na hapo watoto walienda kulala vyumbani mwao, baada ya baba yao kuwaahidi kuwasimulia safari yake kesho yake. Na Joji alienda chumbani kwake na kumkuta Katarina amejipamba kwa nguo nzuri akimsubiri….

Omela uliosema ana fanana na Sali ni mzuri sana.

Ndio kweli.

Umejuaje? Je umesikia nasaha za Tom na Kakhi?

Wewe ndio unatakiwa kunihabarisha kwanza, lini umeonana na Tom?

Sijaonana nae, ila tulikutana katika hafla kanisani kabla ya siku mbili, kwa nini unalikwepa swali langu, ni nani Omela?

Omela ni msichana tuliekutana nae hotelini ghafla tu, ni mzuri sana, amesema kuwa maana ya jina lake ni uzuri uliopindukia lakini niambie umekesha na Tom mpaka muda gani?

Tumekesha mpaka saa za mwisho, lakini unadhani nitaamini kukutana nae ilikuwa ni kwa ghafla tu, halafu hujalisahau jina lake?

Ndio, ilikuwa ni ghafla tu, na je unafikiria nitaamini mkesha wako kanisani ulikuwa mpaka saa moja asubuhi?

Nani aliyekuambia kuwa tulikesha hadi asubuhi? Je unanishuku? Haikuwa ni bora mimi ndie niliyetakiwa kukufuatilia nyendo zako na wanawake hao wazuri?

Nataka kulala samahani…..

Joji alilala kitandani na kuelekeza mgongo wake kwa Katarina kwa sababu maongezi yao yalichafuka, akaamua kulala….na Katarina nae alifanya hivyo hivyo kama Joji na kwa kumpa mgongo wake huku Joji akijiuliza, Je nilikuwa mkali? Je ni kweli alikuwa katika hafla kanisani? Je nimemvunjia heshima yake? Kisha akasema: Huenda nimemtia adabu na kumuadhibu pia nimemshuku kama alivyonishuku, kisha alijidai kulala mara baada ya muda akapitiwa na usingizi na kulala.
Asubuhi ilipofika aliamka na kukuta tayari Katarina amemuandalia chai na chakula anachokipenda …akasahau hasira za jana na kumfurahia.

Karibu mpenzi wangu.

Asante mpenzi wangu, halafu sijakupa zawadi yako, subiri kidogo nitakupa Rozari uliyoitaka.

Nashukuru mpenzi wangu…ni nzuri sana, nilifikiri umesahau!

Vipi nitasahau maombi yako mpenzi, hichi ndicho kitu muhimu zaidi nilikusudia kukuletea kutoka India.

Roho mtakatifu alikuwa nawe akikulinda kwa kuchukua Rozari hii, vipi kuhusiana na ufumbuzi wa maswali?

Ilikuwa ni safari nzuri iliyopelekea kujua dini, fikra, na mila mbali mbali.

Je umetembelea kanisa la Saint James? Limejengwa vizuri sana!

Ndio, nimetembelea… ni zuri kweli nilifikiria Wakristo ni wengi India, lakini nimeshtushwa kwa idadi yao kuwa ndogo sana.

Ndio umesema kweli, kwa masikitiko, watu hawakubali kubadili dini zao za Kihindu kwa wepesi mpaka kuwe na vitisho vya kigaidi, kwa ujumla Kanisa linafikiria kubadili mikakati yake kukabiliana na hali hii.

Magaidi !! Unakusudia Waislamu?

Ndio, ni wabaya na waovu.

Ijapokuwa katika moja ya mikataba yetu kulikuwa na kampuni ya Waislamu, pamoja na wema wao, muamala wao mzuri, ukweli wao na maadili yao, ila kwa ukweli sijapendezwa nao, na miongoni mwao jina lake ni Karimullah na sijajua kuwa nini imetokea hivyo!

Nafsi yako ni safi na nzuri inapenda mema, ni vigumu kuipenda nafsi yenye kuua na kupenda kuangamiza.

Huenda ikawa hivyo, ijapokuwa walikuwa ni wazuri na wepesi katika kufanya nao kazi, lakini ni watu walioshikamana na maadili yao.

Kwa nini, je hakuna Wakristo uliokutana nao?!

HaaHaa: Ndio, nimekutana na Maiko mwenye dini, na sijui kwa nini nilipendezwa nae ijapokuwa tabia yake ilikuwa si nzuri!

Mwenye dini bila tabia nzuri?!

Ndio, ana dini sana lakini mwenye ubaguzi, pia hana tabia nzuri, kwa masikitiko Kakhi alimuomba anitafutie wanawake wa Kihindi na avuruge mikataba ya wafanya kazi, na yeye akakubali hilo.

Oh!! Mtu wa dini halafu anakuletea wasichana!

Ndio, kisha akaendelea kuelezea mpaka Katarina aliporidhika: Cha ajabu alishangaa kukataa kwangu.

Anapora haki za watu na kunitaka nizini! Huu sio Ukristo ni lazima tupambanue kati ya Ukristo na Wakristo.

Ndio, bila shaka huu ndio ukweli kwa hali zote mbili kwa upande mwingine kama ulivyosema: Ni lazima tutenganishe kati ya fikra za watu na dini, ili tusiinasibishe dini na makosa ya watu. Na kwa upande mwingine: Je hayakuwa matendo ya watu yanatokana na fikra na dini zao? Na kitu chochote kikizidi kupita kiasi ni dalili ya tatizo katika dini na fikra zao pia?

Ndio, lakini rafiki yako Maiko ana tatizo lake kipekee.

Huenda… kila wenye dini husema hivyo.

Na vipi kuhusiana na ufumbuzi wa maswali ya dokta?

Nafikiri majibu ya maswali hayo yako wazi kwa upande wangu.

Kwa hivyo…tumesha maliza tatizo?

Tumemaliza kujibu maswali ya dokta tu, lakini kujibu swali la Mungu ambae ameleta dini za mbinguni bado, kwani tupo njiani ili kufikiria lengo kuu na hapo tutafika katika furaha tunayoitaka.

Endelea na utafika katika lengo mpenzi, na vipi umehakikisha ufumbuzi wakati nakusudia ufumbuzi wa kweli kutokana na dini za mbinguni?

Jibu halikuhitaji kuwa na fikra nyingi, bali nimefahamu kupitia dini nyingi za Kihindi ambazo sio za mbinguni, na hazina tija kwa watu wake, na hata kwa binadamu wote, ni dini zilizowafanya wafuasi wao kwenda kinyume na asili ya mwanadamu sambamba na kupingana na uadilifu na hekima, pia nimegundua hata sisi huku Ulaya tunazo dini hizi na zipo kwa wingi ila hazina tija sana, kwa ujumla hizi ni fikra zangu na nitasikitiza fikra ya Tom nitakapo kutana nae.

Lini utakutana nae?

Baada ya siku nne, kisha akaendelea: Nimechelewa kazini kama nilivyokuchelewesha mpenzi wangu.

Nimewaambia leo nitachelewa, nilidhani na wewe huendi kazini leo.

Hapana, nitaenda japo kwa saa kadhaa ili kukabidhi baadhi ya kazi. Samahani mpenzi naomba idhini yako, tutaonana baadae nikirudi.

(2)

Joji alienda kazini.. na aliingia moja kwa moja kwa mkurugenzi wake Kakhi ambae alimkaribisha kwa hamu kubwa….

Ni mafanikio yalioje makubwa uliyo yapata kupitia safari hii?!

Mikataba ilifanikiwa kama ulivyotaka, lakini umejuaje?

Maiko ametutumia ujumbe wa shukurani, na kutujulisha kuwa mikataba imekamilika… ijapokuwa Maiko ana dini pia anafanya vizuri kazini na anajibu maombi kwa matakwa ya watu…kisha alitabasamu: Ama huyu Mutwi Rahmaan ni mgumu kiutendaji, hebu niambie umefanyaje kutaamali nae?

Tumekubaliana na kuwekeana saini kwa kugongwa mhuri wa Ubalozi wa Uingereza nchini India, na umebaki Muhuri wa Ubalozi wa India London.

Siamini macho yangu! Umekubaliana nae vipi?!

Tumekubaliana nae kwa wepesi sana na kwa maendeleo mazuri, na anafikiria faida kwa wote, ijapokuwa yeye ni asiye na mpangilio wa mambo yake, ila aliniacha nifanye maafikiano na ndugu yake Karimullah, ni kazi iliyokuwa imepangwa vizuri, ijapokuwa sijafurahishwa.

Siamini unayo yasema ijapokuwa mkataba huu hapa mbele yangu nauona, ama kwa upande wangu sio Mutwi Rahmaan au Karimullah wanao nivutia, sijui wanayaangaliaje maisha, kama kwamba wapo vitani daima, huenda ni kwa sababu ya tabia za imani yao kwani wao ni Waislamu. Hebu niambie habari za wasichana wangu? Je huoni haya kulala na wasichana wangu Joji?

Sija lala na wasichana wako wala wengine.

Kwa hivyo…..Maiko atakuwa ni mwenye kulaumiwa na hakuwa mwema kwako kama anavyokuwa kawaida yake na mimi?

Kinyume chake alikuwa ni mkarimu sana kwangu, ila mimi ndio nimewakataa wanawake.

Siamini mwenye akili kupoteza nafasi yake hiyo ya kipekee, nilitamani kusafiri kwa ajili ya kustarehe na wasichana hao, ni wazuri, laiti kama sio kikao cha idara, sijui ni lini utaishi maisha yako na kutumia fursa, na laiti ungemaliza mikataba yote ningesema hutasafiri tena, nini maana ya kusafiri India bila kustarehe na wazuri huko, je uliwapata waliokuwa wazuri zaidi kuliko anaokuletea Maiko na hivyo kuachana na wasichana wangu?

Ndio, Omela alikuja hotelini na kunitaka, ni msichana mzuri sana, Haa Haa alicheka, lakini nilikataa.

Sijajua unavyoyaona maisha na starehe zake?!

Bali ni nini maana ya maisha? Na nini kuishi? Na kwa lipi umeumbwa? Ikiwa tunatumia umri wetu na muda wetu kwa kuzikimbiza nafsi zetu na kupata matamanio?

Ha haa, ni muhadhara mzuri wa kumueleza dokta wako, niache mimi na haya, unapaswa kupanga mambo yetu baada ya mikataba hii, na kampuni inakushukuru sana kwa kupata mafanikio hayo.

Nitaanza kazi ya kupanga na masiku machache nitamaliza, na mimi naishukuru kampuni, kwa kweli ilikuwa ni safari nzuri sana

Pamoja na kuwa mimi sioni uzuri wa safari hiyo kwako, ila napenda kukwambia subiri safari nzuri zaidi kama utataka.

Safari nyingine tena?!

Ndio, kuelekea miji Mitukufu.

Miji gani hiyo?

Japo mimi siamini kama ni mitukufu, ila wenye imani ya dini za mbinguni tatu wanaamini hivyo nayo ni: Yerusalem, jamaa zangu wote wapo huko na wananiita huko mara nyingi sana, lakini nahisi wao wameshikamana na dini kupita kiasi! Mama yangu ni Myahudi, ila mimi bado sijakubaliana na dini zote, kwa hakika shirika la usalama la Yerusalem limekubaliana na kuafiki mbinu zetu tulizowaonyesha baada ya kuwatumia, na ukitaka nenda wewe, na kama huendi nitaenda mimi, ijapokuwa napenda wewe uende, kwani wewe unaonekana una uwezo wa kufanikisha mikataba… unayo wiki moja kufikiria.

Sawa, nitaangalia halafu nitakujulisha.

(3)

Joji alirudi kwake baada tu yakumaliza kazi zake…njiani kulikuwa na msongamano kupita kiasi, hali iliyopelekea kufika nyumbani baada ya masaa mawili na nusu badala ya dakika za kawaida anazotumia….alifika nyumbani akiwa mchovu na Katarina alimkimbilia kumpokea…

Namshukuru Mungu kwa kufika salama, nilikuwa na huzuni juu yako.

Sijui nini kimetokea njiani, leo nimechukua masaa mawili na nusu!

Leo Metro ya chini ya ardhi ilisimamisha kabisa shughuli zake.

Kwa nini?

Kwa shambulizi la kigaidi ndani ya Metro, tunamshukuru Mungu halijatokea katika sehemu za vituo la sivyo wangekufa maelfu ya watu.

Je kuna yeyote aliyeumizwa?

Wameuliwa watu wawili mume na mke walioana kabla ya siku mbili na watu wawili wanaume, mwanamke mmoja na mtoto wamejeruhiwa.

Ni mioyo gani walio nayo hawa Magaidi wa Kiislamu!

Joji alishika rimoti ili afuatilie habari kupitia Televisheni….

Nini kinachokujulisha ni Waislamu? Acha tufuatilie habari katika Televisheni.

Hakuna wengine wasiokuwa na mioyo zaidi yao waliofanya hivyo.

Joji alifuatilia habari katika Televisheni, mlipuko ulitokea kabla ya masaa manne takriban, na kila mchambuzi au mtangazaji waliafikiana kwamba ni magaidi wa Kiislamu waliotekeleza shambulio hilo, lakini bado taarifa kamili haijatolewa mpaka sasa hivi. Na hali ya Usalama ilikuwa tete nchini kote Uingereza. Na watu wote walikuwa wanakimbilia kurudi majumbani mwao, njia zote zikiwa zimefungwa.

Inaonekana rai yako ni sahihi, waliotekeleza shambulio hilo ni magaidi wa Kiislamu, ijapokuwa taarifa rasmi bado haijatolewa mpaka sasa kuhusiana na hilo.

Niamini, hakuna wenye mioyo migumu ila ni wao tu, na wanadai wanapigania dini juu ya hilo.

Wanaua watu kwa jina la dini?!

Ndio, wanadai hiyo ni Jihadi na ni ibada kwao ya kuua watu na kuwaadhibu, we angalia tofauti kati ya dini hii ya nguvu na uzuri na mapenzi ya Ukristo, Kristo anajitolea mwenyewe kufa kwa ajili ya wanadamu, na wafuasi wake hivyo pia. Ama wafuasi wa Muhammad hakuna walijualo isipokuwa kuua tu.

Ninashangazwa sana na Waislamu hawa, na huenda ndio sababu iliyo nipelekea kutokuwa na mapenzi sana kwa Karimullah.

Nashukuru Mungu umetoka salama kwao, hawajakuua wala kukulipua.

Haahaa, fikiria Mutwi Rahmaan ajifungie milipuko halafu aniripue kwa hakika alikuwa ni mpole kwangu na amenipa zawadi ya mafuta mazuri ya Kihindi.

Usiyatumie huenda yakawa na sumu, hakikisha kwanza kama yanatumika kwa ajili hiyo.

Mimi sipendelei manukato, nimemletea Adam aliniomba nimletee, lakini nitahakikisha hayana madhara kwa rafiki yangu Adam.

Hakikisha usalama wake kwanza kabla ya kumpa rafiki yako Adam, Hawa magaidi hawaaminiki katu.

Umenikumbusha, sijamtembelea Adam tangu nimerudi na nilimuahidi kumtembelea baada ya kurudi.

Je yeye ni Mprotestanti au Mkatoliki?

Kumbuka sijui! Sijamuuliza wala hajaniambia, nitajaribu kuonana nae kesho na nitamuuliza…je tutakesha leo au tuna lala moja kwa moja?

Mkesha mzuri na mpenzi mzuri zaidi.

Asubuhi Joji aliamua kutokwenda kazini, aliamua kufanyia kazi zake nyumbani kwa simu na intaneti, na metro haijafanya kazi isipokuwa kidogo tu, na msongamano bado upo. Aliwasiliana sana na Adam lakini simu yake ilikuwa imefungwa. Alifungua Televisheni ili kujua habari za mlipuko na magaidi….Serikali ilifungua au kuziruhusu baadhi ya metro kufanya kazi. Na makundi ya Waislamu walishikiliwa wakiwemo Wahindi, Wapakistani na Waarabu pamoja na Waingereza wanaoishi London, na bado habari zinaashiria Waislamu wapo nyuma ya shambulio la Kigaidi. Na miongoni mwa watu majeruhi ni Muislamu muhindi alikuwa akielekea upande wa Metro hali ya kuwa ni mwenye kutiliwa shaka, pia kumekutwa kitambulisho cha mpakistani katika sehemu hiyo, ila upelelezi bado unaendelea… hata hivyo Serikali imewakumbusha raia wote na wanaoishi humo kukaa au kuchukua hadhari kwa mtu yeyote anayeweka kifurushi katika sehemu yoyote ya raia, au sehemu maalumu na hasa sehemu ikiwa ni Muislamu.
Joji alimalizia kutazama habari, na kuvaa nguo tayari kwa kumtembelea Adam mgahawani…hakumkuta kule na kumuulizia na kufahamishwa na mhudumu mwingine kwamba amepata likizo ya siku tano.

Tangu lini ameanza likizo? Na unajua kwa sababu gani amechukua likizo?

Amechukua kwa madai kuwa anataka kumalizia utafiti wake chuoni, na alipumzika tangu siku tatu zilizopita.

Joji alienda nyumbani kwa Adam na kugonga mlango bila kufunguliwa, na kuweka ujumbe mlangoni unaosema kwamba: ‘Nimekuja lakini bahati mbaya sijakukuta’, kisha akarudi nyumbani kwake…. Alimkuta Katarina akifuatilia habari.

Je kama lolote jipya kuhusiana na shambulio la Metro?

Hakuna jipya, bado wanamtafuta gaidi wa Kipakistani, ila hofu imetanda kwamba London itashambuliwa tena kwa shambulizi jingine.

Natamani wamshike leo ili watu watulie na roho zao, nyoyo gani wanazo hawa?!

Je umekwenda kazini leo?

Hapana, bado njia za Metro zilifungwa kwa muda wa asubuhi, ila nilimtembelea rafiki yangu Adam sijamkuta, yupo katika likizo ya utafiti wake.

Je kesho utakwenda kazini?

Ndio… Bila shaka, nina baadhi ya kazi, halafu nina ahadi ya kukutana na dokta Tom.

Safari hii una majibu maalumu na ya wazi kwa dokta?

Ndio, nahisi uwezo wa majibu ndio ulionisukuma kwa mara ya kwanza na hii ni mara ya pili.

Upo sahihi siku zote, roho mtakatifu yupo nawe na kukupa nguvu.

Najua hata maswali yake mapya yatakavyokuwa.

Unajua?!

Naam, inaelekea sina uchaguzi wa kutosha, na sijui ni mbinu za Tom kutaka kuniingiza au imetokea tu ghafla, au ni uwezo wa roho mtakatifu kama usemavyo?

Vipi ?

Mwanzo majibu yalikuwa wapi tutayapata, na ilikuwa wazi sana kwangu kwamba hakuna pa kuyatoa ila kwa muumba pekee. Na wazo la kupinga ni wazo la fujo na vitu visivyokuwa na tija, je yawezekana kuunda utaratibu unaotokana na fujo na vipi kiumbe aliyeumbwa atajua kwa nini ameumbwa? Ukanaji dini unakwenda kinyume na akili, maumbile na dini hata kama itamchanganya msomi mwenye fikra ya kustaarabika. Ilikuwa ni kujiuliza baadaye nani muumba? Na tumezigawa dini na fikra za watu kuhusu muumba katika makundi mawili: Dini za kidunia na dini za mbinguni. Na ilikuwa wazi kwangu na hasa baada ya safari yangu India ni kwamba dini za kidunia bado hazijafaulu kwenda sambamba na maumbile ya kibinadamu pamoja na wafuasi wao hata kama kuna maendeleo ya wanadamu, bali ni upotevu wa hali ya juu usioendana nao na kwa sasa swali lililopo ni: Je dini za mbinguni zinaweza kutupa majibu muwafaka zinazoendana na maumbile ya mwanadamu kisomi?

Je sijakwambia Ukristo ndio suluhisho la mwanadamu?

Na Vipi kuhusu Uyahudi na Uislamu?

Je mpenzi wangu huenda ukawa Muislamu ukiwa umevalia milipuko katika Metro za chini ya ardhi?

Haa Haa huenda nikawa Myahudi kama Kakhi ambae hashughulishwi na lolote isipokuwa mali na mapenzi.

(4)

Kwa muda huo wote, Joji alijaribu kuwasiliana sana na Adam lakini simu yake ilifungwa hali iliyopelekea kujisikia vibaya, alitaka kukutana nae kabla ya kwenda kwa Dokta… akamtumia ujumbe unaosema: “Nimerudi kutoka India na nimekuletea zawadi, naomba kukuona, je unaweza kunipigia?” Lakini hakupata jibu lake….
Muda wa kukutana na dokta ulifika, Joji alikwenda kliniki, Baraad alikuwa mapokezi, alipomuona Joji alimkaribisha…

Vipi habari za India pamoja na wasichana wao?

Ni mji mzuri sana na maajabu…samahani naomba kumuona Tom muda wangu umefika.

Inaelekea una haraka, au hutaki kuongoe nami..hakuna shida!

Je unaniruhusu kuingia kwa Tom?

Ruhusa karibu..karibu, kumbuka utarudi kwangu siku moja.

Joji aliingia kwa Tom na alikaribishwa kwa mapokezi makubwa kupita kawaida, Tom alifurahi sana kwa kumuona na kumwambia Joji hivi:

Nimefurahi sana kukuona na mara ngapi nilikusubiri kukuona na kupata ushauri wako na majibu yako.

Ulikuwa una subiri maoni yangu na majibu yangu?!

Unaweza kuona mshangao kile ninachokisema lakini huo ndio ukweli wake…ndio inaonekana falsafa yako imeafikiana na utafiti wangu wa kielimu pamoja na utafiti wangu wa kidini, kwa hivyo naenda kanisani kuhudhuria baadhi ya vipindi vya elimu ya dini…kisha alitabasamu na kusema: kwa ujumla achana na hayo. Je umeachana na kila dini kama ulivyo tarajia?

Ndio, bila ya shaka…

Vizuri kama nilivyotarajia.

Acha nikamilishe (samahani) nimeziacha dini zote za duniani.

Una maanisha nini?

Nina maana kuwa lazima tutafute majibu makuu kuhusiana na Mungu muumba, kama zinavyosema dini za mbinguni.

Kwa haki gani kuzithamini dini za mbinguni kuliko za duniani?

Sio mimi niliofanya hivyo, bali wenye dini wenyewe wanajua kuwa dini zao bado hazijakamilika na wanaendelea kuziboresha na kuziendeleza.

Kuziendeleza?!

Ndio, wanaziboresha kwani wanajua ni za watu wenyewe na vipi watajibu maswali mazito ya watu mfano wetu, na pengine sisi tuna wazidi kielimu kuliko wao, na vipi binadamu atajua maisha wanayoishi bila muumba alie waumba, na haiwezekani wajiumbe wenyewe, na hata wanyama tu hawawezi, je huoni dini hizi za duniani ndio chimbuko la ukafiri katika ulimwengu?

Unasema kama vile dini za mbinguni hazina shaka!

Ndio, ni kweli….sijajua swali lako ni katika kuchagua kati ya dini za mbinguni au duniani, na uchaguzi huo sio wa shaka.

Wewe ndio ulioweka chaguzi hizo na sio mimi.

Na wewe umekinaishwa nazo na umerekebisha swali, kwa ujumla sisi tunakwenda njia ya sawa ya kielimu pamoja na kutopendezwa kwangu, na wakati wowote ule tutakuwa tumeacha kufuata dini za mbinguni, na wakati huo tatarejea katika ukafiri wa kupinga dini na Mungu.

Sidhani kama hilo linatimia, ukafiri ni njia ya dhulma yenye kutisha haimfikishi mtu katika furaha ya kweli, na kwa hivyo makafiri wengi maisha yao yameishia kwa kujinyonga.

Haa haa, una maanisha na mimi nitajiua muda sio mrefu?! Ni kwa nini sasa wenye dini nao wanaamua kujiua?

Nategemea wewe unajua giza lililotanda katika ukafiri, na ndio maana umeanza utafiti wako kuhusiana na dini, ama swali kwa nini wenye dini wanajiua? Ni swali ambalo mimi najua jibu lake sio la lazima sana.

Cha msingi kwa sasa hivi ni kufanya utafiti kuhusu dini za mbinguni, ikiwa tutafikia kuona kuwa hazitupi majibu kuhusiana na hilo ni lazima tupate ufumbuzi, ijapokuwa mimi kafiri ila nimetosheka kwa yale unayosema kuhusiana na ukafiri, isipokuwa sina budi na uchaguzi huo na sitoacha uchaguzi wangu moja kwa moja.

Zimebaki dini tatu tu.

Je tutaujadili Uislamu wa vitisho tena?

Sijui, kwa sababu wewe hutaki kuachana na uchaguzi wako?!

Ndio ….umesema kweli, nadhani wewe utafikia hatua ya kujificha katika milima ya Torabora kama bin Laden

Ijapokuwa nauchukia sana ugaidi, na hakika kuwa sio akili wala dini wala moyo, isipokuwa njia ya elimu yenye uadilifu ndio itakayotufikisha huko.

Bila kupoteza wakati, uamuzi ni wako wa kuchagua iliyokuwa bora kati ya dini tatu, napendekeza kuitanguliza ile iliyoridhiwa na wengi.

Dini zote tatu, tumekubaliana.

Nakusudia Uyahudi, kwani Nabii Mussa anakubaliwa na Wayahudi, Wakristo na Waislamu.

Nimeelewa, nadhani ni vizuri kuangalia upande mwingine kabisa.

Vipi tena ewe Mwanafalsafa?

Kwamba Waislamu wanamuamini Musa, Issa pamoja na Muhammad kinyume chake Wakristo hawaamini wengine isipokuwa Musa na Issa na Wayahudi hakuna wanayemkubali isipokuwa Musa tu.

Ni mtazamo sahihi kabisa wa kutofautiana, ila mimi bado nashauri ya kwamba tuanze na Uyahudi kwani ndio dini ya mwanzo ya mbinguni.

Sawa nakubaliana na wewe kabisa.

Ni matarajio yangu uwe na wakati wa kutosha kuangalia kila dini, kwani wewe unazungumzia historia na falsafa, fikra, dini na uhalisia wake kwa wakati mmoja na ukimaliza kutafiti Uyahudi usiuponde au kuunga mkono mpaka utafiti Ukristo na ukimaliza kuutafiti Ukristo, utafiti na Uislamu, halafu alitabasamu na kusema, ikiwa una lengo la kwenda huko Tora bora!

Vizuri, swali langu ni hivi; ni njia ipi utatumia kujua dini hizi?

Kusoma pamoja na utafiti ndio njia kuu isiyoisha, na ikiwa utajuana na wanazuoni wa dini hizi itakusaidiana sana. Natamani ungesafiri kwenda Tel Aviv kama ulivyoenda India ili ujue vizuri Uyahudi kwa ukaribu.

Na cha kushangaza ni kuwa kuna safari fupi ya kuelekea Tel Aviv ila bado sijaamua kwenda mpaka sasa hivi.

Bado sijajua matatizo yako kwani umetoka India ila kama utapata wasaa wa kwenda Tel Aviv itakusaidia sana na ukitaka kuujua Ukristo uende Roma, na Uislamu uende Makka ila magaidi hawatakuruhusu kuingia humo!

Maneno yako yamenitia hamasa ya kusafiri kuelekea Tel Aviv ila nitaangalia kwanza halafu nitakujulisha nilichoamua.

Inaelekea una bahati, kwani wanawake wa Kiyahudi, ni wazuri sana ni wanawake waliochanganya damu zao kwa kila maumbile, baada ya kustarehe na Wahindi na sasa ni zamu yako kustarehe na wanawake wa Kiyahudi, bahati iliyoje kuipata kwako!

Joji hakufurahishwa na maneno ya Tom na aliamua kumtia hasira kwa kumwambia….

Kwa nini usistarehe na wagonjwa tofauti tofauti, na kwa nini usistarehe na wanawake wenye kupenda kukesha kwenye sherehe ili kutimiza au kukamilisha utafiti wako?!

Nimekuelewa sana unacholenga, Katarina ni mzuri na uzuri wake ni kuwa anajitolea kutumikia dini yake, usigeukie kulia wala kushoto.

Au huenda unapenda kustarehe na wanawake wa Kihindi na ndio maana unajilazimisha kufanya utafiti wako usiku kucha mpaka asubuhi.

Pia nimekuelewa sana unachomaanisha, mpaka asubuhi kwa sababu ya moto uliozuka na kuunguza jengo karibu na kanisa. Halafu Tom alimgeukia kwa hasira na kusema: Ijapokuwa nina historia ndefu kuwa na mahusiano na wanawake ila kwa Katarina ni tofauti kabisa hana upuuzi huo zaidi ya kutangaza ukatoliki wake.

Unataka kuniambia katika kukutana kwenu na kukesha kwenu mnatafiti dini, Ukristo na Imani tu?!

Hapana, Kanisa linatumia sherehe ili kuwavuta watu na kuwaelimisha dini.

Na kupitia sherehe hizo ndipo kunazuka visa vya mapenzi.

Ndio umesema kweli, lakini Katarina pamoja na uzuri wake hayupo hivyo lengo lake lipo wazi, nalo ni kulitumikia kanisa na kuwapa elimu zaidi watu kumuamini Kiristo.

Mh mh, Na juu ya hilo mnakunywa pombe pamoja ili imani izidi na kujitolea mhanga kwa ajili ya binadamu?!

Ijapokuwa unatumia kauli sio nzuri zinanichukiza ila mimi nitaeleza uzuri wa Katarina kwangu, hakika ameuvuta moyo wangu kwa mara ya kwanza tangu miaka kumi na tano. Kweli nimekunywa pombe katika sherehe ya kanisa na mimi ni mpingaji ila nimeshangazwa na Katarina kwa kunywa pombe ijapokuwa ni mfuasi wa dini.

Nini kinachotokea pindi imani ilipofika kwenye lengo lake, na kujitoa muhanga kwa ajili ya wanadamu?!

Acha nisema kweli tu, pamoja na Katarina kutaka kuzidisha kunywa na mara tu baada ya kumaliza tatizo la moto jirani, alichoka na kunywa kupita kiasi.

Na wakati huo mkakesha na mkajichanganya pamoja!

Joji, hakukuwa na kitu chochote cha aibu kati yetu, isipokuwa baada ya Katarina kunywa sana alijisikia kizunguzungu hali iliyonipelekea kumchukua mpaka katika gari na kumsubiria mpaka azinduke, na ndio sababu iliyotufanya kuchelewa mpaka asubuhi, na akanishukuru sana na huku akishangazwa na hali hiyo, na ikadhihiri huruma yangu kwake na kumbusu, halafu nikajisikia nimekosea kwa tendo langu hilo na yeye hakufurahishwa kwa hilo pia.

Vizuri ni mapenzi mazuri na ni wajibu wangu kukupongezeni!

Tulikuwa naye muda mrefu rafiki yake na jirani yake Sali, na unaweza kuthibitisha haya nisemayo kutoka kwake, pia na katika mtandao wangu wa facebook; kuna picha zote tulizopiga usiku huo, sikulazimishwa kusema yote hayo, ila nimependelea niwe muwazi kwako ijapokuwa kauli yako sio nzuri na sijajua kwa nini nataamali na wewe kwa njia hii, labda na mimi najihisi nina tatizo kama lako au tofauti na hilo.

Tatizo hilo hilo langu?!

Hakika utashangaa kile ninachokuambia ila nina jambo linanishughulisha moyoni mwangu tangu zamani, na tangu mwaka sasa limezidi na bado sijajua nini sababu, lakini cha kushangaza tangu umerudi na majibu pamoja na utafiti wangu wa dini tatizo hilo limeanza kupungua na sijui ni kwa nini?

Je ni kwa sababu ya kuuliza na kuyajibu au ni kwa sababu nimetembelea kanisa na kuamini au vyote hivyo? Kuhusiana na dhiki na huzuni. Je zinatoka wapi? Na vipi maswali yanakupata ambayo yana kuvunja vunja?

Yameanza kupungua sana, labda ni kwa sababu ya kujishughulisha kutaka kuyapatia ufumbuzi wake kutafuta njia ya furaha na safari zangu kuondokana na matatizo yanayonisumbua moyoni mwangu.

Maelezo haya ni mazuri ya “Katika kufikia kwenye furaha”.

Ndio, njia ile aliyoniambia kikongwe niliyekutana naye njiani, halafu akaitilia uzito yule mpokeaji wageni pale penye mgahawa.

Kila mtu anataka kufuata njia ya furaha na nafsi inaifikiria, ila ukweli utabaki hivyo hivyo.

Nini unakusudia?

Kila mwenye dini au dhehebu au kundi wanadhani wapo katika njia ya kuelekea furahani, na wao tu peke yao wapo katika njia hiyo! Kisha alitabasamu na kusema: Hii ni dharau ya hali ya juu

Lakini bila shaka mimi na wewe hatupo katika njia ya furaha, vinginevyo tusingekuwa katika hamumu hii na ghamu hii ambayo tunaishi nayo!

Lililo muhimu, niache nifanye majumuisho kwa yale tulio simamia kwayo…. Ni kwamba furaha ya kweli ndio itakayojibu maswali makubwa, na kuwa Muumba ndie atakayetupatia majibu ya maswali na sio binadamu; kitu kinachofuta kabisa wazo la kukana dini, na Muumba huyu ndie mwenye dini za mbinguni na sio za duniani, na sisi ndio tuamue ni dini ipi ndio dini sahihi.

La msingi wafuasi wa dini hii ya mbinguni ndio walio katika furaha ya kweli, na naamini mimi naelekea huko kama Katarina alivyo sema tangu mwanzo, ila mimi sitaki kufanya haraka na kufunga mjadala, ukizingatia kwamba na yeye amepunguza kuandamwa na maswali magumu na vizuizi vyake, na ukizingatia nachukua uangalizi wa kina na wepesi juu ya mambo magumu.

Hapana shaka kwamba Katarina mwenye kujitolea muhanga kwa kila kitu katika kufikia njia ya Mola anastahiki kujua ukweli, lakini acha kwanza tutimize malengo yetu, na nasubiri mpaka utakaporudi kutoka Tel Aviv ili tuendelee na hayo.

Tumekubaliana, nimekuchelewesha leo…na kuomba niondoke na kama muda upo tutaonana baada ya wiki mbili kama nitasafiri na ikiwa sijasafiri tutaonana wiki ijayo.

Ila makubaliano yetu ni baada ya wiki mbili ili upate kuwaelewa Wayahudi na jitahidi kwenda miji hiyo mitukufu ili uzidishe ujuzi wako.

Fikra nzuri ya “miji mitukufu”!

Ndio… ni miji mitukufu kwa kila dini za mbinguni na mara nyingi vita na mivutano ya dini hizo zinatokea humo.

Nitajitahidi kwenda, pamoja na kujaribu kupangilia mambo yangu.

Joji aliachana na Tom na nje alimkuta Baraad akimsubiri na usoni mwake akiwa na tabasamu lenye dharau.

Vipi habari ya Katarina? Je utampeleka Torabora?

Tora bora?!!

Usiwe mwepesi wakuchezea maneno!

Nini unakusudia?

Sikusudii chochote, Katarina na Tom wote ni wazuri wenye mvuto wa kupendeza, na unaweza kusafiri, uwe imara na usiwe dhaifu.

Joji hakumjibu na alitoka akiwa na hasira, alikuwa makini kwa maongezi yao kati ya Tom na Baraad. Je unadhani Baraad amesikia maongezi yangu na Tom? Au yeye ni katika wale wanaoitwa telepathia? Au ni nini?!

(5)

Joji aliendelea kuwasiliana na Adam lakini bila majibu yoyote yale, wasiwasi na hofu zilianza kumuingia Joji, alikwenda nyumbani kwa Adam zaidi ya mara moja lakini hakumpata…Katarina aliona wasiwasi aliokuwa nao Joji…

Unaonekana ni mwenye dhiki..kimetokea nini?

Sijamuona rafiki yangu mhudumu Adam, na nimewasiliana nae sana, na nimekwenda kwake mara nyingi!

Ulikuwa unahofia isije ikawa imempata tatizo kutoka kwa magaidi, nilipokuona ghamu nimekuogopea sana, inaelekea unampenda sana Adam?!

Pamoja na upole wake na hali yake ya kawaida lakini amenisaidia sana, na kwa kweli najihisi utulivu sana kwa mazungumzo nae.

Wenzake kazini wanasemaje?

Yupo likizoni kwa ajili ya utafiti wake wa chuoni; kwani yeye ni mwanafunzi anasomea mambo ya dini kama nilivyokujulisha hapo kabla.

Lini likizo yake inakwisha?

Itakwisha kesho kutwa, hata hivyo nina hamu sana ya kukutana nae, ili anishauri baadhi ya mambo..hata hivyo nilitaka kukushauri wewe kuhusu lengo la safari yangu Yerusalem au wanapopaita Tel Aviv.

Aah unakusudia nchi takatifu?!

Ndio; huenda nikaenda kwa ajili ya kutiliana mkataba na shirika la ulinzi la Kiyahudi.

Iweje hivyo nawe sasa hivi unaingia kutoka safarini, nahofia usije ukapata shida na machovu kwa wingi wa safari

Sitopata tabu, hata hivyo nilitamani kukaa nawe na Maiko na Sali kwa muda mrefu, na sikuwa ni mwenye kuhamasika na safari hii hadi nilipokutana na Tom leo hii ambae alinihamasisha sana kusafiri.

Kwa nini?

Anasema: Utaujua Uyahudi kwa ukaribu zaidi.

Katika hili amesema kweli, bali dini zote tatu za mbinguni utazijua; hiyo ni ardhi iliyobarikiwa kwa dini zote za mbinguni.

Nini rai yako wewe?

Sijatanabahi na nukta aliyoizungumza Tom, ukiona utapata faida safari na nitafurahi kwa hilo kwa ajili yako na nitakusubiri mimi na wanangu kurudi kwako.

Alichokisema Tom kinaingia akilini, hata hivyo bado sijahamasika sana, na hata ikiwa hivyo nitaifanya iwe fupi sana.

Wewe ni mwenye bahati sana umesafiri katika nchi ya maajabu, na sasa unataka kusafiri katika nchi muhimu sana ya vyanzo vya vita vingi na mapambano!

Bali mimi ni mwenye bahati ya kuwa na mke mzuri.

Ninapenda kukupa zawadi yako

Zawadi gani hiyo?

Utakaporudi na kupumzika kidogo, tuchukue likizo na tusafiri sote kwenda Roma, ili ukamilishe safari zako zote; yaani baada ya nchi za maajabu na kisha nchi ya mapambano, na baada ya hapo nchi ya makanisa, ili uweze kuufahamu ukatoliki katika makazi yake ya asili, na ili uweze kufikia unayoiita njia ya furaha.

Na baada ya hapo nitakuwa nimeshaujua ukristu kuliko anavyotaka Tom, kisha akaendelea: Inaelekea kuwa kesho nitamjulisha Kakhi kuwafiki kwangu safari hii, natamani nisisafiri hadi ile hali ya hatari inayoikumba nchi itakuwa imekwisha kwani inasumbua sana, na kadhalika kuhakikisha hali zenu ndio nisafiri, au hadi wale magaidi majambazi watakapohukumiwa.

Bado uchunguzi unaendelea kwa yule Mpakistani ambae ndie wanayemdhania kuwa amelipua, wameshawakamata marafiki zake wote na wenye kumzunguka.

Watakwenda wapi? leo au kesho wote watakamatwa, ni kiasi gani nachukizwa na watu hawa magaidi!

Joji alipofika tu alielekea katika ofisi ya Kakhi, ili amjulishe kuwa amewafiki safari ile, na matamanio yake kuwa safari iwe fupi na ikiwezekana isiwe zaidi ya siku nne tu…

Siku nne zinatosha kabisa.

Je majukumu yangu yako wazi yanafahamika?

Ndio, shirika la Yerusalem la ulinzi na usalama ndilo linalotaka kuingia mkataba nasi, nao ni mkataba wa ulinzi wa kielektroni, tumekubalina nao katika kila kitu takriban.

Kwa nini usiwatumie mkataba kisha wakasaini kuliko mtu kusafiri.

Mhusika wao wa teknolojia ana maswali mengi; ni maswali ya ndani yenye kutaka maelezo ya kina, kadhalika kwa ukweli wanahitaji kukinaishwa; hadi sasa dada huyo mhusika ndie pekee aliyegoma mkataba kusaini, maamuzi ya mwisho yanategemea kukubali kwake. Yeye ndie atakayepitisha.

Kama ni hivyo inabidi nijue kadhia zote za teknolojia kwa undani zaidi, na inabidi nisome maelezo yanayohusiana na upinzani wake katika maandikiano yenu naye.

Ndio, hili ni muhimu mno, na mwishowe watasaini mkataba watake au wasitake.

Unaonesha kujiamini kabisa!

Ndio, kwa sababu nyingi; Kwanza: Mayahudi wana Phobia na magaidi wa Hamas, na uwezo wao hata katika teknolojia, na kwa hivyo wataingia mikataba na sisi au hata na wasiokuwa sisi.

Wana haki zote, magaidi hawana mioyo, unaonaje tuliyonayo hapa London?

Lakini Mayahudi ni magaidi zaidi kuliko Hamas na wengineo!

Huenda ikawa hivyo, sijui, ninachokijua ni kuwa magaidi wa London walitamani wafe watu wengi sana kama sio mamia basi maelfu bila ya sababu yoyote ile kutoka katika moyo, au dhamiri au dini!

Achana na ugaidi kwa sasa, ama sababu ya pili: Ni kuwa Levi ndie mhusika wa kitengo cha teknolojia cha shirika la kiyahudi na mkuu wake ni Myahudi vile vile.

Sijafahamu? Kwa nini kuwa kwake myahudi pamoja na mkuu wake ni myahudi ina maana watasaini wote mkataba.

Pamoja na kuwa dini yao ni Uyahudi nawajua walivyo, mkuu wake wa kazi anaitwa Benjamin ambae anataka kuingia mkataba pamoja nasi kwa maslahi maalum, wala huyu dada mhusika wa teknolojia hawezi kumkatalia akitakiwa kufanya hivyo, vinginevyo hatompa mahitaji yake; dada yule anamtii sana bosi wake kwa ajili ya dini.

Kwani na wewe sio Myahudi?!

Ndio, mama yangu ni Myahudi; na kwa hali hiyo mimi vile vile ni Myahudi, na hii ni sababu ya tatu; na kwa hivyo wamewafiki kuingia nami mkataba, hata hivyo mimi ni msekula dini haina maana kwangu ila kama itaniletea maslahi ya mali na starehe, ha ha ha, kwa fikra ni kuwa Levi ni msichana mdogo tu ana umri wa miaka 25 tu, na ni miongoni mwa wasichana wazuri kabisa duniani, na ukitaka kustarehe nae ongea na Benjamin na atakuletea siku hiyo hiyo. Ama Benjamin nimeshakubaliana nae yeye binafsi kiasi cha Dola 100,000 yake binafsi ili awafiki kusaini mkataba.

Je 100,000 Sio nyingi sana?!

Nyingi sana, lakini niliongeza thamani ya mkataba kuwa 150,000 Dola, na akakubali ili muradi apate cha kwake.

Ni mmomonyoko wa kimaadili kiasi gani huu! Hii ni hiana ya shirika na kwa nchi, hii sio biashara!

Mali kwetu ni kitu kingine bwana, sisi mayahudi ni wafanya biashara wa kweli, na ndio unaona tunatamalaki biashara ulimwenguni, hakuna anayeweza kushindana nasi katika mali na biashara yeyote.

Maneno yako yananiogofya kuhusu dini ya Uyahudi, na haiba ya wayahudi.

Ha ha ha, wanasema: Ukimsalimia myahudi rejesha mikono yako baada tu ya salamu, ukiikuta ipo kamili, basi hakikisha kuwa bado unajua kuwesabu sawa sawa, cha msingi ni kuwa mpe Benjamin laki moja na utaona mambo yanavyokwenda kwa wepesi.

Tutamaliza mazungumzo yetu na kuhusu muwafaka na mazingira yake baada ya kuusoma mkataba na maelezo yake.

Vizuri, weka nafasi yako baada ya wiki kutokea sasa, na wiki hii kwa pamoja tutamaliza maafikiano yetu na vikao vyetu.

Joji alijikuta akiendelea kusoma maelezo ya mkataba na vipengele vya maafikiano, kadhalika na yale maelezo ya fani mwisho wa muda wake wa kazi, alitoka hali ya kuchelewa na ilhali bado hajamaliza kazi yake, kwa muda wote huo alijaribu kumpigia simu Adam mara nyingi na kila akipiga simu yake ilikuwa imefungwa. Alirejea nyumbani kwake na akaendelea kufuatilia habari; alikuwa anatamani yule Mpakistani akamatwe kabla ya safari yake.
Alisikia kwenye taarifa ya habari kuwa kuna uwezekano wa mhusika mwingine kabisa wa mlipuko, na kuna watu wengine wapya waliokamatwa, na wote hawahusiki na ugaidi wa Kiislamu, bali wahusika ni harakati za SIITA iliyoparaganyika. Katarina alikaa pembeni yake akiulizia kipya kilichojiri..

Ni kitu cha kushangaza habari hizi za kigaidi kuwa kuna uwezekano wa mhusika mpya wa shambulio hili la ulipuaji!

Haya ni maneno ya kupoteza malengo tu, hawafanyi hivyo isipokuwa Magaidi wa Kiislamu tu.

Harakati za SIITA zinazotaka kujitenga ndie mtuhumiwa mpya..

Huenda ikawa ni mbinu ili magaidi wasogee kisha waanze kuwasiliana; ili waweze kumkamata yule Mpakistani, na ndio maana wakatangaza hivi.

Katika ulimwengu wa siasa kila kitu kinawezekana!

(6)

Joji alishughulishwa katika siku iliyofuata kwa ajili ya safari yake, na kutayarisha mikataba, alikuwa kila mara akiwasiliana na Adam, lakini simu yake ya mkononi ilikuwa mara zote haipatikani, alimtumia barua pepe na barua nyingine katika face book yake. Kulingana na mazungumzo ya mhudumu mwenzake kazini Adam alitarajiwa kuanza kazi leo hii. Alitamani sana kumuona Adam kabla ya wakati huo; kwake ina maana kubwa..
Alipomaliza muda wake wa kazi ofisini …Joji alipitia kwenye mgahawa, na akamuulizia Adam..lakini hakumpata!

Hakufika leo.

Je likizo yake haijesha?

Ndio imekwisha, lakini hakufika kazini, wala hakufanya mawasiliano yoyote, na hii si ada yake kabisa!

Je unatarajia atakuja lini?

Sijui, alitarajiwa kuanza kazi leo, asiyekuwepo huwa ana udhuru.

Asante, akija mjulishe kuwa Joji alipita kumuuliza zaidi ya mara moja.

Vizuri, vizuri.

Joji alirejea nyumbani kwake, lakini akiwa na hofu kuhusu Adam, kutoweka kwake ghafla kumemtia wasiwasi, hakuna njia iliyobaki ya kuwasiliana nae isipokuwa ameitumia: simu, barua pepe, face book, kumfuata kazini, hata nyumbani kwake mara nyingi, lakini zote hakukuwa na athari yake!

Karibu mpenzi wangu, je, umeonana na sahibu yako Adam?

Sijampata, wala hakwenda leo kazini pamoja na kuwa likizo yake imekwisha!

Nataraji isiwe imempata ajali ya ugaidi.

Nami nataraji hivyo, je kuna mpya? Je, wamemkamata aliyelipua?

Kwa bahati mbaya..habari zilizopita hivi punde zinazungumzia kuachiwa huru watuhumiwa wote Waislamu leo hii!

Wamewaachia maharamia!

Wanasema kuwa uchunguzi umebaini kuwa mlipuaji ni miongoni mwa wanaharakati wa SIITA waliojitenga.

Ha ha ha, umenikumbusha aliyoniambia Karimulah mtu ambae sikupendezwa nae: “Gaidi ni yule ambae hakubaliani nanyi, lakini akikubaliana nanyi huwa ni shujaa” huenda akawa ni mkweli..!

Bado sijakinaishwa, na naamini ya kuwa aliyelipua ni Mpakistani, je hawakusema mwanzo kuwa kamera zilichukua picha yake?!

Huenda Karimullah akawa ni mkweli, je walimkamata mtuhumiwa huyo mwanaharakati wa SIITA?

Ndio, na wanasema kuwa ni tukio la kisiasa na sio la kigaidi.

Kuwabadilisha watuhumiwa tumefahamu hilo, ama kubadilisha tukio kutoka ugaidi kwenda jinai hapo hatujafahamu?!!

Anakuwa ni gaidi ikiwa mtekelezaji wa tukio ni Muislamu.

Ha ha ha, haya ndio maneno hasa aliyosema Karimullah mwenyewe, cha msingi ni kuwa London imekuwa ya salama baada ya kukamatwa kwa majambazi.

Simu ya Joji ililia, akaipokea haraka, alitamani mpigaji awe ni Adam, na kweli alikuwa yeye Adam, alipokea kwa hamu.

Mwishowe Adam, nimeingiwa sana na hofu kwa ajili yako.

Ha ha ha, nilikuwa katika jukumu fulani dogo na nimemaliza sasa hivi.

Je umemaliza utafiti wako?

Bali imekuwa ya kina zaidi, achana na hilo vipi hali yako?

Katika hali nzuri, nataka kukuona, je nije kwako sasa hivi?

Nimechoka katika kazi niliyoimalizia, unaonaje ukaja ninapomaliza kazi zangu kesho?

Sawa, tumekubaliana, nitafika kwako kabla ya saa kumi na moja, nitakualika katika chakula cha jioni, katika hoteli ya furaha.

Sawa, nitakusubiri kesho.

Joji alikata simu, na hisia za furaha zikamrejea tena..

Unaelekea una furaha baada ya kuongea na mhudumu!

Ndio, sijui kwa nini hivyo, katika mazungumzo yake napata hisia za ukweli katika mazungumzo yake, upole na umakini wake.

Je, ni Myahudi au Mkiristo? Au ni Mkatoliki au Mprotestanti?

Sijawahi kumuuliza hilo, nikikutana nae nitamuuliza swali hilo.

Katika ahadi waliyowafikiana Joji alimsubiri kwa gari lake mbele ya mgahawa kwa dakika kadhaa kisha Adam akatokea na kupanda gari pamoja nae..

Ulikuwa wapi, umenitia hofu?

Asante kwa wema wako, samahani sana, sikuweza kujibu barua zake kwa mazingira yaliyojitokeza, nipe habari nzuri ya njia ya furaha? Na majibu ya maswali yako? Na safari yako ya India..

Safari ya India ilikuwa na faida nyingi sana, nimefurahishwa sana, tutamalizia mazungumzo yetu tukifika hotelini.

Hamna neno, tumekaribia.

Walipofika hotelini Joji na Adam walikaa katika meza ndogo iliyotayarishwa kwa ajili ya watu wawili, na mhudumu akafika na orodha ya chakula. Adam akawa anaangalia huku akizungumza na Joji.

Hoteli hii ni nzuri..

Inaelekea kuwa ni hoteli unayoipenda sana..

Jina lake linanivutia, kwani napenda furaha, na ninahisi kuwa ni mahitaji ya kila mwenye akili katika dunia hii, hata mwenye hoteli ni mgeni, sijui ni wa nchi gani?

Hoteli za Wamalaysia ni chache hapa Uingereza, hii ni hoteli ya Mmalesia, je ulipata kwenda Malaysia?

Hapana..

Malaysia ni nchi ambayo nataraji kuzitembelea, sikuwahi kwenda huko, wanasema kuwa tabia nchi ni nzuri kama watu wake walivyo, watu hawa ni watu wa kawaida sana hawana makuu na tabia zao ni nzuri.

Upole, ukawaida wakati mwingine ni dalili ya umakini na wakati mwingine ni dalili ya kutokujua.

Hapana, hii ni dalili ya umakini, Malaysia ni nchi inayoendelea kwa kasi haswa katika mawanda yetu ya teknolojia.

Napenda ukawaida wenye umakini, kisha akatabasamu na akasema: Au umakini wa upole, kamilisha mazungumzo yako kuhusu safari yako ya India..

Tuagize chakula kwanza..

Joji alimuita mhudumu na wakaagiza chakula chao, na mhudumu akawakaribisha na akaondoka.

Safari yangu ya India imejibu maswali yangu kwa uwazi, na ninaamini kuwa ninapita katika njia ya furaha.

Vizuri sana!

Safari yangu iliingiwa dosari na matatizo ya Katarina na Tom ambayo nimekuelezea, nami nakushukuru sana kwa ushauri wako; nilikuwa katika hali mbaya ya kinafsi, na inaelekea kuwa maneno yako yalikuwa sahihi.

Maneno gani?

Uliniambia: Huenda shaka nilizokuwa nazo zikawa si sahihi, kwani Tom aliniambia kisa chenyewe kwa usahihi wake, na sijui kwa nini mara hii nimemwamini, na ninahisi kuwa amekuwa tofauti na kubadilika.

Kila mtu anaweza kubadilika na kuwa katika hali nzuri zaidi madamu tu wamepata fursa ya hilo..kisha akatabasamu na akasema: Na vipi kuhusu ubora wa dini kati ya dini za wanadamu na za mbinguni?

Bila shaka ya kuwa dini za mbinguni ni bora kuliko za wanadamu.

Inaelekea kuwa una hakika na hilo.

Ndio, nami nimeona mkanganyiko uliopo katika dini za ardhi, dini za wanadamu ambayo hata akili haiwezi kufikiria, kisha akacheka na kusema: hebu fikiria kuna watu wanaoabudu panya, na kuna wanaoabudu mende, na wanaoabudu mawe, ulimwengu wa ajabu kabisa. Bila ya shaka kuwa Mungu ambae atajibu maswali yangu hawezi kuwa panya, mende au sanamu au mnyama.

Kwa maana hiyo una hakika kuwa ni dini za mbinguni ndio sahihi?

Hapana, bila ya shaka, itakuwa ima ni Uyahudi au Ukristu au Uislamu…

Ni hatua ipi ifuatayo utaifuata?

Ni kuanza utafiti wa kujua dini hizi za mbinguni moja baada ya nyingine, na nitaanza na Uyahudi…kwa mnasaba ni ipi dini yako rafiki yangu?

Unatarajia itakuwa ipi? Jina langu ni Adam kwa jina la baba wa wanadamu wote, na jina la baba yangu ni jina la baba wa Mitume yote na dini zote za mbinguni (Ibrahim).

Vipi hilo?

Adam ni jina la baba wa wanadamu wote, na Ibrahim ni jina la baba wa Mitume yote, na katika kizazi chake ni Musa, Isa (Yesu) na Muhammad.

Na wewe unamfuata yupi katika mitume hiyo?

Unaonaje tuipitie dini moja hadi nyingine katika dini hizo tatu, huenda nikabadilisha dini yangu!

Inaelekea wewe ni Mkatoliki kama mke wangu…Ha ha ha, chakula kimeshafika..Unajua? inaelekea umeniathiri katika hilo, nimejiona kuwa nakariri maneno yako kuhusu ukawaida, pamoja na kuwa tabia ya falsafa siku zote ni kuyafanya maneno kuwa magumu na sio kuyawepesisha..na tabia zetu sisi Waingereza wakati mwingine kwa bahati mbayatunafanya mambo kuwa magumu badala ya kuyarahisisha.

Ukawaida, upole, tabasamu, furaha ni maneno yenye kuungana na kuingiliana daima.

Na katika mtiririko huo huo, ni kuwa ugumu, migongano, huzuni na uovu ni maneno yenye kulingana, sijakuambia kuwa daktari amependekeza nisafiri kwenda Tel Aviv ili nipate fursa ya kuusoma Uyahudi na kuufahamu vizuri, nini rai yako?

Vizuri, utasafiri kuelekea miji mitakatifu!

Je, sijakuambia kuwa wewe ni Mkatoliki?

Huenda safari yako ikawa na manufaa makubwa kufahamu kuhusu dini hizi tatu, na sio kuhusu Uyahudi peke yake.

Ni sawa na aliyoniambia Katarina vivyo hivyo pindi nilipomjulisha kuhusu safari yangu ya Tel Aviv

Sio lazima niwe Mkatoliki ili nikuambie hayo, hili ndilo linaloafikiana na dini zote za mbinguni..Hii ni ardhi ya mapambano, na ninaamini kuwa safari yako itakuwa yenye faida kubwa ili kujua zaidi kuhusu Uyahudi na dini nyinginezo, pamoja na kuwa hilo halitoshelezi na kusoma.

Unakusudia nini?

Umebakia muda gani wa safari yako?

Siku nne.

Napendekeza usome, tusome kwa pamoja kuhusu Uyahudi, dini kubwa, tukufu.

“Uyahudi dini kubwa tukufu”! je wewe ni Myahudi?

Wafuasi wote wa dini tatu kubwa wanaamini kuhusu Musa, hii haiwezi kuwa ni dalili, kwa nini tusizungumze bila kuwa na hisia za nyuma, achana na dini yangu, huenda nikawa Myahudi, Mkristo au Muislamu!

Kwa mnasaba wa kunitajia Uislamu nimekumbuka udi ulioniagiza.

Bei gani?

Ha ha ha, ni bure, nilipewa zawadi na Muislamu, na sihusiki ikiwa ni bomu au kuna sumu ndani yake, kama alivyonitahadharisha mke wangu, Katarina.

Ha ha ha, kwa maana hiyo nikijipaka nitakuwa gaidi?

Tulikuwa katika hali ya hofu ya ugaidi kwa sababu ya milipuko hapa London, ikiwa ni bomu basi itakuwa ni hali ya jinai na sio ugaidi.

Kwa nini ni Jinai na sio kigaidi?

Ni jambo lenye kuchekesha, sijui kwanini, inaelekea kuwa sisi kama alivyoniambia Muislamu mmoja India kuwa: “Ugaidi ni pale mnapokuwa hamuwafikiani wala hampendezwi.”

Ugaidi ni ugaidi tu, haina dini wala nchi yoyote inaweza kusifiwa kwa ugaidi, hudhani kuwa hata sisi katika miamala yetu ya kawaida pamoja na wake zetu na watoto wetu tunakuwa magaidi, na kadhalika nchi zinaweza kupiga vita ugaidi lakini hapo hapo nao wakawa ni magaidi kwa miamala yao. Nguvu, mauaji ya kutisha yanagongana na Abc za akili na dini, hata ikifanywa na mtu yeyote!

Inaelekea unazungumzia kufungwa na kukamatwa kwa baadhi ya Waislamu bila dhambi yoyote kwa milipuko hii ya karibuni.

Sawa sawa, hadi sasa hivi pamoja na uhakika wao wa kuwa hawahusiki lakini bado idadi ya waislamu ipo jela, je huu nao sio ugaidi?!

Bila ya shaka ndio, lakini sijui kwa nini naamini kuwa Waislamu wengi ni magaidi?

Hiyo ni hali ya kawaida kabisa kuwa na mtazamo huu, nami vile vile ni muhanga wa tamalaki ya vyombo vya habari na siasa za kigaidi.

Kwa vipi? Unakusudia nini?!

Ufalme huu wa vyombo vya habari unatengeneza namna ya kufikiri kwetu na mtazamo wetu kwa wengine, na hiyo inafanyika kwa utambuzi wetu na hata bila ya utambuzi wetu hali kadhalika. Je huoni ya kuwa nchi nyingi za kikoloni huziona nchi zilizozitawala kuwa ni nchi za watu waberiberi wanaostahiki kuuwawa! Je huo ni mtazamo wa watu kuwaangalia watu wa mataifa mengine kuwa ni wauaji na watu wabaya majambazi, na mtazamo wa dini moja kwa nyingine ni mtazamo wa kuwa wao ni wauaji na magaidi.

Swadakta, lakini unaelekea mwenye hamasa sana, kisha akatabasamu na kusema: Je wewe ni Muislamu?

Ha ha ha, chunga sana nisije kukulipua sasa hivi pamoja na hoteli yako hii.

Usijali nilikuwa nakutania, rafiki yangu.

Nami hali kadhalika, tumechelewa, tuondoke unipitishe nyumbani.

Haya twende.