MAZUNGUMZO YA ROHO

MAZUNGUMZO YA ROHO

MAZUNGUMZO YA ROHO

(1)

Joji alinyanyuka toka kitandani mwake akiwa amechoka sana, alikuwa akihisi uchovu na ni bora kama angebakia chumbani kwake siku nzima asikutane na mtu yeyote, hata hivyo alikuwa katika changamoto na Kakhi na aliazimia amshinde na awe juu yake zaidi katika majukumu yake magumu. Ni bora mambo yake binafsi ayatenge na anayopambana nayo miongoni mwa khofu na kubabaika na uchovu, vinginevyo vitamuharibia kazi yake na mustakabali wake.
Ahadi yake leo hii na Jamali saa nne asubuhi, hivyo basi anao muda wa kutosha kupata staftahi na kuangalia barua pepe, hakutaka kuondoka chumbani, na hivyo basi kuwapigia watu wa Buffet hapo hotelini na kuwaomba wampelekee staftahi yake hapo chumbani, kisha baada ya hapo akaelekea kuoga haraka hadi muda staftahi utakapofika…..
Baada ya dakika chache mhudumu aligonga mlango, na akaingia akiwa na vyakula na kuweka mezani na kutoka. Joji akachukua staftahi yake wakati huo huo akiwa anaangalia barua pepe, akapata barua kutoka kwa Katarina:

“Mpenzi Joji Pamoja na muda mfupi tu wa safari yako, ninahisi nimekutamani sana, nakuhitajia sana, na siwezi kusubiri mwezi mzima hadi urejee, nipo katika mtanziko na sijui lipi la kuamua, nami nina haja kubwa na wewe inatosha kukujulisha kuwa mimi Mkatoliki mtu wa dini nimelia sana nikiwa nasikiliza tarjumi ya kitabu kitakatifu cha Waislamu wanachokiita Qur’an, ninaishi katika hali ya wasiwasi mkubwa sana. Nina haja sana nawe. Mpenzi wako Katarina.”

Joji akajibu:

“Mpenzi Katarina, Nadhani nitarejea hivi karibuni tu, ahadi yangu ya jana ilikuwa mbaya sana, mfano mbaya kwa Waislamu, sijui tatizo lipo kwa Waislamu au lipo kwenye dini yao? Namchukia Mustafa ambae nilikuwa nae kwenye ahadi ya jana, nitajaribu kurejea katika muda wa siku kadhaa zijazo, sali kwa ajili yangu. Sitaki kufeli kwenye changamoto hii pamoja na Kakhi. Mpenzi wako Joji.”

Alipata barua nyingine kutoka kwa John Luke:

“Rafiki yangu Joji, nimepata barua yako, na nimefurahi kuwa rai yangu kuhusu wizi ilikuwa ni sahihi, na ole wako kufanya maamuzi ya haraka haraka, ama kuhusu hali ya mwanamke sina tatizo lolote, tatizo langu lipo kwenye uhuru katika Uislamu! Ikiwa una mtazamo wowote au rai yoyote nijulishe. John Luke.”

Akamjibu,

“John Luke, Huenda ukashangazwa kuwa kwa muda mfupi nimebadilisha rai yangu!! Ndio katika Uislamu hakuna dhulma kwa mwanamke, bali Uislamu umekuja kwa yenye kunasibiana na maumbile yake na tabia yake. Pamoja na kuwa hatujazoea hilo katika jamii zetu mbaya, lakini ni mfumo kamili unaojitegemea kabisa. Nimezungumza katika suala hili na kujadili sana na nimekuwa na hakika kuhusiana nalo, hata hivyo sijasoma wala kujadili kuhusu suala la uhuru. Ikiwa umepata chochote nitumie, nami nitakutumia hali kadhalika nitakayoyapata, nitajaribu kuulizia hilo na kusoma pia. Joji.”

Alipokuwa anafuatilia barua zake simu ya chumbani ililia, mfanyakazi wa mapokezi alimjulisha kuwa kuna mtu anayemsubiri mapokezi, aliangalia saa yake akakuta ni saa tatu na nusu, akashangazwa, je inawezekana Jamali akaja kabla ya ahadi yake kwa muda wa nusu saa.”

Samahani ni nani anayenisubiri?

Kuna msichana anakusubiri.

Ni nani huyo?

Ameniambia kuwa anakufahamu, lakini hakutaja jina lake.

Vizuri nateremka kumuona sasa hivi.

Joji aliteremka katika chumba cha mapumziko ya wageni na kumkuta Diana akimsubiri, alikuwa amevaa mavazi ya kawaida, nywele zake amezitupa kwa nyuma, hakuongeza usoni mwake chochote katika vipodozi, tofauti ilikuwa kubwa baina ya uso wake jana na leo. Pamoja na hayo uso wake ulikuwa wa kawaida na kupendeza zaidi kuliko ile jana, na macho yake makubwa yaliyoficha umakini na akili pevu ndani yake.
Joji alimkaribisha na kumtaka akae katika chumba cha mapumziko.

Utakunywa nini?

Hapana, sitokawia sana, nataka kuzungumza nawe jambo.

Joji alimuashiria mfanyakazi na kumtaka alete glasi mbili za juisi.. kisha akamgeukia Diana akijiuliza sababu ya kumtembelea kwake, aliona machoni mwake machozi yakitaka kumtoka lakini akijaribu kuyaficha…

Karibu…

Mimi niliyetaka kutoroka jana kwa maswali yako ambayo yaliniangamiza na kuniua kwa ndani! Mimi ndie ambaye uliyenidhalilisha jana! Mimi ni Muorthodox niliyetoroka! Mimi ni msomi mkimya kama usemavyo, mimi ndiye yule aliyechoka na maisha..!

Nakukumbuka vizuri, lakini ni nini kinachotakiwa kwangu?

Kwani mimi sio mzuri?!

Bila shaka, wewe ni mzuri sana bali ni uzuri wenye kufitini wa mashariki! Lakini je umekuja tu nikuambie wewe ni mzuri?!

Kama ni hivyo kwa nini basi ulinidhalilisha jana?

Mimi sijakudhalilisha, nilikuwa nakuuliza tu na kujadiliana nawe.

Nimekumbuka kuwa nawe maswali yalikusumbua kama mimi! Na ya kuwa kukimbia hakutotatua matatizo! Je unaweza kunijulisha majibu ya maswali haya magumu yenye kuchosha akili?

Je umekuja kwa ajili hiyo?

Ndio!

Je nikikuambia kuwa sijapata majibu, bali nilikaribia kujiua kwa sababu ya maswali haya!

Ikiwa unachosema ni sahihi basi hili linadhihirisha kuwa una akili nyingi.

Kwa kuwa sijapata majibu ni dalili ya kuwa na akili nyingi.

Bali nina maanisha kutoyakimbia ni dalili ya akili nyingi.

Na wewe Diana kwa nini unakimbia?

Sisi ni wanadamu zinatupitia hali nyingi za udhaifu.

Kwani kweli hakuna majibu ya maswali haya?

Bila ya shaka yapo.

Ni kiasi gani natamani kuyafikia na kuyafahamu.

Ama mimi nayafahamu lakini ni muoga.

Unajua?!

Ndio, lakini mwanadamu hafanikiwi dhati yake, wala hatofurahi katika maisha yake, wala hawezi kubadilisha kitu katika nafsi yake, ila pindi atakapokuwa na ujasiri pamoja na nafsi yake.

Sifahamu unachokisema!

Wakati mwingine fukara anaendelea kubaki fukara; kwa sababu anahofia kupoteza lau akifungua biashara, na wakati mwingine ambae hajaoa anabaki kutooa; kwa sababu anahofia kuoa, na wakati mwingine mjinga huendelea kubaki mjinga; kwa sababu anahofia kujifunza.

Sahihi na jambo lipo wazi, lakini sijui unazungumzia nini?

Mimi najua jibu zuri sana kwa maswali haya, lakini huenda nikauwawa au kufungwa, ndio maana nimebakia nilivyo.

Ama mimi sitoogopa!....niambie ni nini hiyo?

Je una hakika, una ujasiri kiasi hiki?

Huenda ikawa hivyo, niambie bila kutumia falsafa kubwa.

Nilikuwa nasema kama wewe, lakini mwishowe nikaingiwa na woga, na nikarejea kufikiria njia za kutoroka hali hii.

Niache nijaribu ujasiri wangu ikiwa umekinaishwa kwa unachosema! Nitapata wapi majibu ya maswali yetu?

Nimekuja nijue kutoka kwako utawezaje kujibu maswali yako, na sio nikujulishe jinsi ya kujibu maswali yako!

Lakini ombi lipo kinyume, tafadhali nijulishe.

Huenda nitakachokuambia kitakukasirisha, lakini baada ya kufikiri kwa muda mrefu na kufanya utafiti sijaona isipokuwa hilo, ni nini kinakuzuia usiwe Muislamu?

Joji alinyanyua macho yake juu, akatabasamu tabasamu angavu kwa Diana, na akarejea ile misimamo yote iliyokwisha mpitia tokea aanze utafiti kuhusu njia ya furaha, Katarina, Omela, Levi, Habib na John Luke…na Mutwi Rahman na Karimullah na Adam na Sheikh Baasim na Jamali, safari ndefu ameshapita, na akaishi uzoefu mkubwa, ambapo ndani yake amefanya mijadala mingi, amesoma sana na kupata kufikiria kwa kina. Je inawezekana safari yote ngumu hii ikaishia kwenye Uislamu? Je Uislamu ndio njia ya furaha?!
Kisha si yeye ambae mara kwa mara anasema kuwa akiipata njia hiyo mara moja ataifuata, je ni kweli anayosema Adam ya kuwa anahitajia ujasiri? Je ujasiri wake anaouonesha ni maneno matupu.

Samahani inaelekea nimekusumbua, nilikuwa natamani uwe na majibu mengine, ninachotamani isiwe kimya chako ni kuogopa na uoga kama wangu!

Samahani nilikuwa nafikiria tu!

Unafikiria nini?

Kuhusu swali lako.

Ninajua jibu mapema, wewe ni muoga.

Niogope nini?

Unawaogopa wanaokuzunguka, unaiogopea nafsi yako.

Hapana, mimi siogopi, lakini je unaweza kuniambia kwanza: Kwa nini hofu yote hii unayo kuhusu Uislamu?

Siuogopei Uislamu!

Sasa unaogopea nini?

Familia yangu, baba yangu alikufa na nikahamia pamoja na mama yangu kwenda kuishi katika nyumba ya mjomba wangu, nami najua kama nitasilimu, atapata wazimu, na huenda akaniua!

Kwa nini?

Mjomba wangu anaitakidi kuwa Waislamu wanatudanganya.

Huenda ikawa ni kweli!

Mjomba wangu anapenda sana nikae pamoja na Waislamu waliopotoka, kuliko mimi kukaa na Wakristo, kwani nimejadiliana na Wakristo wengi na wanasema kuwa nimetingisha imani ya dini yao katika nafsi zao. Hivyo basi mjomba wangu anataka zaidi nikae na Waislamu waliopotoka na dini yao kwani ni wabaya zaidi kuliko Wakristo.

Mfano Mustafa.

Ndio, bwana huyu namchukia sana.

Lakini huoni kuwa yeye ni mfano wa Waislamu?!

Bali mfano mzuri wa mafisadi waliopotoka, iwe umewaita kuwa ni Wasekula au ni Waliberali au ni shetani, lakini nijibu nini kinachokuzuia kusilimu?

Samahani, napenda tukamilishe kwanza yale ya nyuma, kwanini basi mjomba wako akuuwe utakapokuwa Muislamu?

Ili hali ya kuacha Ukristo zisikariri mara kwa mara!

Hili linapingana kabisa na haki ndogo kabisa ya uhuru wa mtu kuwa na dini!

Uhuru gani! Mimi ni Mkristo kama wewe, je unao uhuru wa kutokuamini siri mbali mbali za kanisa ambazo akili inakataa? Je unao uhuru wa kuamini kuwa Masiya hakuwa Mungu kama ilivyo katika baadhi ya nakala za vitabu vitakatifu?!

Achana na hili kwanza, nina ahadi na mtu sasa hivi, nae ananisubiri kule, hata hivyo ningependa tumalizie mjadala wetu baadae! Ningependa kukutambulisha kwa rafiki yangu Muislamu kama hakuna tatizo kwako.

Unatoroka kujibu swali nililokuuliza kwa hofu na upungufu wa ujasiri kama nilionao, hata hivyo jambo linarejea kwako, ninafurahishwa kumfahamu rafiki yako.

Joji alikwenda kwa Jamali, na akamuomba msamaha kwa kuchelewa, na akamjulisha habari ya Diana na akarudi na Jamali hadi kwa Diana.

Huyu ndie Diana ambae anataka kuingia katika Uislamu.

Karibu Diana, mimi ni Jamali kutoka Alexandria, nimefurahishwa na kutaka kwako kuwa Muislamu.

Nami kadhalika kutoka Alexandria, lakini ni Muorthodoksi, na sijamuambia Joji kuwa nataka kuwa Muislamu, bali nimemwambia kuwa majibu ya maswali yetu mengi yenye kutusumbua yapo kwenye Uislamu.

Vizuri, na hii ina maana kuwa unautaka Uislamu, kwa sababu hakuna yoyote ambae angependa apatwe na wasiwasi, hofu au hapendi kujibu maswali yake.

Sawa kabisa, ndio maana nilikuwa namuuliza Joji kwa nini hasilimu?

Na mimi sikumjibu Diana, lakini nimeshangazwa na ubaya wa unyama wa Wamisri, Diana ananiambia kuwa kama akiingia katika Uislamu basi atafungwa au atauwawa!

Diana alipumua…Akh, Akh, usiwatuhumu Wamisri! Nyie Ulaya na Amerika mmetuzidi sana kwa ukatili, je mmesahau mlichofanya Iraq kule Abu Gharib, unyama na matumizi ya nguvu na kupenda ukatili katika sura yake mbaya kabisa, na haswa zaidi kwa wanawake wenu huko Magharibi. Je unaweza kukataa kuwa mwanamke huko kwenu hupigwa mara sita kuliko mwanamme, je unaweza kukataa kuwa asilimia 33 ya wanawake Marekani hupigwa mara kwa mara, je utakataa kuwa kwenu Uingereza asilimia 77 ya wanaume huwapiga wake zao bila ya kuwepo sababu ya hilo?

Inaelekea umekasirika na kukerwa na mazungumzo yangu!

Hapana, lakini natetea nchi yangu kwa mashambulizi yako.

Ni vizuri kuipenda nchi yako, vizuri sana! Lakini yawe mapenzi ya maadili, pamoja na kukinaishwa kwangu na kuwazidi kwa ukatili katika nchi za Magharibi, bado nashangazwa na mambo haya kuwepo huku kwenu. Hata hivyo sisi ni bora kuliko nyinyi katika uhuru wa kuabudu, kwani unaweza kuwa Mkristo, Myahudi, Muislamu au Mbudha bila matatizo yoyote yale.

Jamali alicheka kisha akasema:

Ha ha ha, ndio maana nikabu ikakatazwa Ufaransa!! Na ndio maana wakakataza adhana na kujenga minara huko Uswisi!! Unazungumzia uhuru gani?

Swadakta, ewe Jamali, lakini hatumuui au kumfunga mtu yeyote anayetaka kusilimu?!

Hata sisi hatumuui mwenye kutaka kusilimu!

Umesema kweli Jamali, nadhani hii ni kasumba ya Wakristo hapa kwetu, lakini hata Uislamu ulienea kwa nguvu na kwa upanga?

Ni Komando yupi wa majeshi ambae kwa upanga wake watu wa Indonesia, Nigeria, Ethiopia au Tanzania au mfano wake wamesilimu? Nchi nyingi za Kiislamu zimesilimu kwa da’wah bila ya upanga na historia inathibitisha hilo, bali hakuna aliyelazimishwa kusilimu..samahani, je wakristo katika nchi hii si walikuwa chini ya hukumu ya Waislamu kwa miaka 1400 je ni nani aliyewalazimisha Uislamu? Je wahindi waliokuwa chini ya hukumu ya Waislamu kwa muda wa miaka 1000 je walilazimishwa Uislamu? Je Wakristo wa Hispania walilazimishwa kusilimu au hao Wakristo ndio ambao waliowalazimisha Waislamu kuwa Wakristo au kuwauwa katika mahakama na kuwindwa baada ya hapo (ili wafutike Hispania)?!

Joji alihisi majadiliano yamekuwa makubwa na yametoka katika utawala wake, hivyo akataka ayamalize ili asije kuchelewa katika ahadi yake.

Tumechelewa sana, nilitaka tu kuwatambulisha, Diana hiki ni kitambulisho changu, na nataka unipe namba yako ya simu.

Pokea tafadhali, hii ni kadi yangu, na hii ni ya kwako Jamali.

Nitakupigia kama si tatizo ili tukamilishe mjadala wetu, huenda ukawa leo au kesho.

La msingi ni kuwa mjomba wangu asijue, akawa kama vile mfano wa Wafaa wa Constantinople au Christine Mmisri au Mirna Adil au mfano wao, kisha kumbuka kuwa hukujibu swali langu hadi sasa!

Nitakupigia leo au kesho, na nitakujibu maswali yako pamoja na ugumu wake! Haya kwa kheri.

(2)

Joji alipopanda gari pamoja na Jamali, alimgeukia Jamali na kumuuliza kwa mshangao:

Majina haya ya mwisho aliyoyataja Diana ni ya nini?

Unakusudia watu wa Constantinople na Christine na Mirna na wengineo? Hawa ni wanawake wa Kikristo waliosilimu wakatekwa kisha wakaadhibiwa na baadhi yao kuuwawa! Hivyo basi anaogopea kuwa kama wao.

Unyama kabisa huu, la msingi ni kuwa nataka kumaliza kazi zangu kesho hapa Cairo; ili nirudi Uingereza kwa masiku kadhaa kisha nirejee tena Cairo, kwani mke wangu yupo katika hali mbaya angependa niwe naye karibu.

Vizuri, leo hii ni ahadi na shirika la mwisho, kisha chukua maamuzi yako walau kwa kipaumbele katika utaratibu uutakao.

Hili ndilo litakalokuwa, lakini nataka kuuweka utaratibu wa ufuatiliaji na kuendelea kwa kazi baada ya safari yangu.

Baada ya usaili katika shirika hili la mwisho tutajua ni nani watakaofaa kwa hilo…tumekaribia, unataka nirejee saa ngapi?

Tuingie sote na tutoe maamuzi baada ya hapo.

Waliingia katika shirika lile, na wakamuomba sekretari waonane na mkurugenzi, naye akampigia mkurugenzi kumjulisha kufika kwa wenye ahadi nae.

Karibuni, Dr. Khalid anawasubiri.

Dr. Khalid aliwakaribisha na kuingia nao katika chumba cha mikutano.

Kulingana na mawasiliano yetu nataraji kuwa kuna wataalamu ambao unaweza kuonana nao leo?

Ndio kuna watu wanne leo hii, na wengine unaweza kuonana nao kesho ukipenda. Nimewagawanya makundi mawili kati ya watu wenye fani ya teknolojia na wataalamu wengine katika menejimenti ya 1.T.

Vizuri sana, vipi kuhusu wataalamu katika menejimenti ya I.T.?

Kama nilivyokutajia wapo wanne ambao utaonana nao leo, ninaamini kuwa kuna uwezekano wakutane na na watu wa teknolojia kwa niaba yako ikiwa utaridhishwa nao, kwa ujumla wao ni watu wa teknolojia na wataalamu wa programu vile vile lakini wao walisoma na kufanya kazi katika menejimenti ya teknolojia na programu.

Muda gani naweza kuonana nao?

Baada ya kunywa chai unaweza kuonana nao, wakiwa ni mmoja mmoja au kwa pamoja ukipenda.

Ningependa kuonana nao wote wanne kwa pamoja.

Kama utakavyo, nitahakikisha kuwa wameshajitayarisha wakati utakapokuwa unakunywa chai chukua hii ni CV zao ni vizuri kuwafahamu kwanza kabla ya kuanza usaili, samahani baada ya dakika chache nitarudi.

Joji alizipitia CV zao upesi upesi, alivutiwa sana na uwezo wao, hata hivyo hakufanya haraka hadi aonane nao: alifupisha maelezo yao katika karatasi ndogo:
Muhammad AliMuislamu miaka 38 alisimamia menejimenti ya miradi ya Serikali ya Kielektroni Misri lakini haijakamilika.
Amir Ishaq miaka 37 Mkristo. Alisimamia menejimenti ya miradi ya teknolojia ya Umoja wa Mataifa pamoja na Serikali ya Misri pamoja na Egyptian Information Centre.
Salwa Hassan miaka 39 Muislamu. Alisimamia menejimenti ya miradi ya Shirika linalofanya kazi katika Smart Device.
Maazin Kamal miaka 39 Muislamu anasimamia mashirika mawili ya Programu na Web Designing.
Pindi alipomaliza kuandika tu Dr.Khalid aliingia….

Ikiwa umemaliza, nitawaita kuingia katika chumba cha mikutano.

Nipo tayari.

Vizuri Joji, Mimi ninakwenda, nije kukuchukua saa ngapi?

Asante Jamali, sidhani kama maudhui haya yatachukuwa muda mrefu sio zaidi ya saa nzima, nitakusubiri kuna sehemu nataka twende sote.

Vizuri, kwa heri.

Dr. Khalid aliwaita wale wenye CV zile kuingia kwenye chumba cha mikutano, ambapo Joji alikuwa akiwasubiri.

Sitaki kuwarefushia kikao nyie wala mhandisi Joji nilishawaeleza anachokitaka, na ameshaangalia CV zenu na kuandika muhtasari wake, kwa kupunguza wakati kikao hiki kitakuwa cha pamoja, karibu Joji.

Nimefurahishwa na CV zenu wote, na nimezisoma na ninazo hapa, kila mmoja anieleze anaweza kulifanyia nini shirika letu, na kwa nini amelikubali?

Aliwasikiliza wote na kujadiliana nao, alivutiwa na wote na akawajulisha kinachotakiwa, na akaamua kuwachagua watatu miongoni mwao aliwaainisha vizuri (Amir, Salwa na Maazin), kwani Muhammad kazi hii haimfai, aliwataka wamchague mkuu wao na wote walikubaliana kuwa Amir ndie atakayewafaa.

Hamna tatizo mkuu wenu awe Mkristo?

Kuna tatizo gani, mbona hata wewe ni Mkristo?

Amir ni rafiki yangu tokea tulipokuwa sekondari na nitasema mbele yake kuwa ni mwenye haki zaidi ya kuongoza, na namtamania Uislamu, hata kama hakusilimu bado ataendelea kuwa rafiki yangu.

Hatuna tatizo kama lenu huko Magharibi pamoja na Waislamu, na nilikuwa naamini kuwa Maazin ni mwenye uwezo kuliko mimi katika uongozi na menejimenti.

Nina ahadi baada ya muda mfupi, nawataka mumalizie kikao chenu na muweke muhtasari wa mpango jumuishi kwa ajili ya uanzwishaji na usimamizi wa kazi kwa mwaka wa kwanza, na sisi tutaonana kesho asubuhi kwa ajili ya mapitio na kupitisha mpango wa kwanza na kuanza kazi. Hali kadhalika nawapeni habari nzuri kuwa nimekutana na kundi zuri la wafanyakazi wa teknolojia wenye uwezo mzuri katika ofisi ya International Employment Bureau.

Ambayo inaongozwa na Dr. Gerjes?

Ndio, Amir je unamfahamu?

Dr. Gerjes ni rafiki yetu mimi na Maazin, na ana kundi zuri la wafanyakazi.

Kadhalika nimempata mtaalamu mzuri wa programu ambaye nimekutana nae katika ofisi nyingine jina lake Diana Saamih.

Ha ha ha, Diana Saamih Programmer?

Je, unamfahamu?

Ni mtoto wa dada yangu.

Je wewe ni mjomba wake?

Ndio.

Haiwezekani!

Kitu gani hakiwezekani?!

Lazima nionane nawe jioni ya leo, je unakubali nikualike chakula cha usiku, saa moja usiku?

Sisi sote?

Hapana, nakuhitaji wewe tu katika jambo maalum lisilo na uhusiano na kazi.

Vizuri, wapi?

Katika hoteli ambayo nipo, chukua hii hapa anuani yake.

(3)

Nataka uende nami sehemu wala usinipinge.

Hamna neno, wapi?

Nataka nikae na mafukara na watu wa chini kabisa kisha nizungumze nao.

Ombi la ajabu kabisa, sitopinga, lakini je naweza kujua ni kwa nini?

Nataka kuwasikiliza wao katika mambo fulani na kujua mtazamo wao kuhusu maisha.

Sababu nzuri kabisa.

Kwa mnasaba: Nimefahamiana na mjomba wake Diana ambaye atamuuwa Diana kama atasilimu, nimepata fikra vile vile.

Umefahamiana nae wapi?

Ni ambae nimempendekeza awe Mkurugenzi wa Shirika!

Bila shaka mtu kama huyu hafai, kwa nini kasumba kiasi hicho Joji?

Sikujua kama ni mjomba wake ila baada ya maamuzi, na nikakubaliana nae awe Mkuu.

Hii ni aibu na upungufu wa maadili, anaweza kukufanya ukabadilisha rai yako.

Swadakta, na hili ndilo litakalokuwa, lakini baada ya kufanya zoezi fulani utakaloliona jioni; nakualika nawe kwenye chakula cha usiku, hotelini kwangu.

Unakusudia nini?

Utaona mwenyewe jioni.

Vizuri, tumeshafika katika mtaa wa mafukara…

Nataka kumtembelea mtu nyumbani kwake!

Hamna neno mimi namjua mtu lakini yupo upande wa pili wa barabara, wacha nimpigie kwanza ili nihakikishe kama yupo na kama atakubali ziara yetu.

Vizuri, na mimi nitawasiliana na Diana.

Joji aliwasiliana na Diana na kukubaliana wakutane nae saa moja usiku hotelini, Jamali nae akampigia Amo Said akimjulisha ziara yake pamoja na Joji.

Lazima tununue chakula cha mchana na tuchukue pamoja nasi.

Kwa nini?

Kwa sababu haifai ifike wakati wa chakula cha mchana wala asitukaribishe Amo Said, nami najua kuwa hawezi kutukaribisha, sasa kwa nini nimfedheheshe?

Sawa, tununue chakula kizuri kabisa pamoja na tamutamu na yote yenye kufaa.

Walifika katika nyumba ya Amo Said, ilikuwa ni nyumba ya zamani sana, katika mtaa mchafu wenye barabara nyembamba sana, Jamali aligonga mlango. Amo Saidi alifungua mlango akiwa anatabasamu huku akiwakaribisha, wakaingia wakiwa na chakula, matunda na tamutamu….Aliwaingiza katika chumba cha zamani sana lakini kikiwa kisafi sana, ndani yake kulikua na sofa za chini kwenye ardhi chakavu. Katikati yake alitandika chano ndani yake kulikuwa na mikate pamoja na mboga mboga na sahani ya wali.

Karibuni.

Chukua tumekuja na hiki chakula.

Nawashukuruni, lakini hakukuwa na haja hivyo; mimi nimewatayarishia chakula, dakika niingize ndani watayarishe.

Amo Said aliingia ndani na Joji akamtaka Jamali amjulishe walichozungumza, na kumtaka amfasirie neno kwa neno alichosema Amo Said, na asiache neno alilosema ila amjulishe. Baada ya dakika chache Amo Saidi alirejea akiwa na sahani kubwa ambayo ndani yake aliweka vyakula vyote vilivyoletwa na Joji pamoja na Jamali.

Karibuni, mmetutukuza.

Jamali, muulize anatamani nini katika dunia hii?

Stara na afya ewe mwanangu.

Je yeye ni mwenye furaha katika maisha yake?

Ewe mwanangu fadhila za Mola wangu ni kubwa sana, mimi nipo katika nyumba na nina watoto, na kila siku ninapata mlo wangu, ninataka nini zaidi ya hapo.

Je hutamani mali au utajiri?

Ewe Mola wangu tupe riziki na utuzidishie, lakini sio mali peke yake, Mola wetu hutuzidishia katika mali na siha na utulivu

Muulize anataka nini katika utulivu na anakusudia nini?

Ewe Jamali muulize swahibu yako anaishi vipi? Asiyefahamu utulivu maisha yake ni ya tabu.

Samahani narejea swali langu, wakati gani anahisi tumaini na utulivu?

Napata tumaini ninapokunywa chai wakati wa alasiri pamoja na wanangu, na ninapoweka ubavu wangu kitandani usiku nami sikuwa nimemuasi Mola wangu na wakati ambao nimeshasimamia haki nilizo nazo, na sijamuudhi yeyote, ewe mwanangu mwambie: Je hahisi tumaini baada ya kuswali?

Jamali alipofasiri yale maneno kwa Joji, alikaa kimya kwa muda mrefu huku akiangalia chini.

Samahani sana nadhani nimepetuka mipaka katika mazungumzo nanyi ni wageni wangu, na haki zenu ni kukirimiwa.

Sio lazima kwake aombe msamaha, bali mimi ndie wa kuomba msamaha kwa majibu, naomba udhuru kwa majibu na naomba nimuulize swali la mwisho, muulize kwa nini anaishi?

Maswali yenu ya ajabu sana! Je kuna ambae hajui kwa nini tunaishi?! Ewe mwanangu sisi tumeumbwa ili tufanye ibada, naye Mola wetu ndie ambae anaturuzuku na kwa mikono yake kuna fadhila nyingi na ukarimu wote, lakini sijajua kwa nini mmenitukuza kwa kunitembelea.

Mwambie ili tumfahamu na tufaidike nae.

Mola wetu awabariki.

Joji alimuona Amo Saidi akiwa anakula chakula chake mwenyewe zaidi kuliko kile walichokileta wao cha gharama kubwa.

Jamali muulize kwa nini hali katika chakula tulichokileta?

Ili niwaachieni nyie wageni wangu, pamoja na kuwa nyie ndie mliyekileta, ukweli ni kuwa naona ladha nzuri ya chakula changu cha kawaida, kama muonavyo katika chakula chenu, ikiwa mwanadamu ni mwenye furaha ameepushwa na kila ovu, kila atakachokula kitakuwa ni kizuri na kitamu na maisha yote kwake ni ya furaha, Mwenyezi Mungu ashukuriwe.

Walimaliza chakula chao, akamuaga Amo Saidi na kumshukuru kwa kuwakaribisha, kisha wakatoka.

Inaelekea nimekuchosha, lakini ningependa kutembelea Kanisa au makazi ya Mkristo wa hali ya chini na ya kawaida kabisa.

Kama ni hivyo tushuke tena chini kwani jirani yake Amo Saidi ni Mkristo, je unataka nimwambie atuombee ruhusa?

Vizuri.

Jamali alimpigia Amo Said na kumjulisha, dakika chache tu Amo Said akatoka hali ya kuwa anatabasamu.

Karibuni.

Wapi?

Nina jirani yangu… nimeongea nae na kumjulisha kuwa mpo mlangoni anawakaribisha.

Amo Said aligonga mlango akafungua ajuza akiwa amejifunika kichwani mwake haonekani isipokuwa uso wake tu.

Karibuni, Sabri anaosha uso wake, nimemwamsha usingizini na anakuja sasa hivi.

Dakika hivi, nakwenda nyumbani kuleta chochote.

Jamali una hakika kuwa hii ni nyumba ya Mkristo?

Ndio, kulingana na maneno yao.

Kwanini basi anafunika mwanamke kichwa chake?

Pamoja na ujuzi wangu wa majibu lakini ni bora kusikia kutoka kwao.

Amo Said alirejea akiwa na kahawa, pamoja na baadhi ya vyakula na akaviweka mbele yao.

Nimemwambia jirani yangu asitayarishe chochote kwani kila kitu nilishakiandaa, kwani sisi tumemshtukizia ziara, na wageni wangu ndio wageni wake.

Ahsante kwa chakula na kahawa pamoja na kuleta wageni.

Jamali, waulize wao ni majirani kwa muda gani?

Said ni swahibu wangu tokea akiwa na umri wa miaka kumi na mbili (12), pindi baba yangu na baba yake walipokuwa jirani.

Lakini nyie hamko katika dini moja!

Kweli, lakini sisi ni majirani na ni marafiki, kila siku Said ananinasihi na ananitaka niwe Muislamu.

Muulize: Ni nini rai yake kuhusu Uislamu na Ukristo na mahusiano baina yao?

Ewe mwanangu Yesu na Muhammad wote ni Mitume kutoka kwa Mungu, na mimi na baba yangu ni Wakristo na Said na babu yake ni Waislamu tokea zamani na mahusiano ni mazuri tokea zamani.

Muulize kwa nini hakusilimu? Pamoja na kuamini kuwa Muhammad ni Mtume kutoka kwa Allah?

Ha ha ha, Said vile vile anaamini kuwa Yesu ni Mtume kutoka kwa Allah sasa kwa nini na yeye hawi Mkristo?!

Kwa sababu Muislamu anaamini kuwa Yesu ni Mtume wa Allah, lakini Mkristo haamini kuwa Muhammad ni Mtume wa Allah.

Ni maneno yale yale ya Said, je unataka ukweli mwanangu? Mimi ninaogopea kuyaacha yale waliyokuwa wakifanya baba na babu zangu, vinginevyo mimi ni mwenye kukinaishwa na anachosema Said, naye ni mpendwa wangu zaidi kuliko hata watoto wa ami yangu, lakini nina swali. Je wewe ni Mkristo au Muislamu?

Nitalihifadhi jibu la swali hili kwa ajili ya wakati, nina swali lingine, kwa nini mke wako amevaa kama Waislamu?

Mke wangu amevaa kama wavaavyo wanawake wote wa Kimisri wawe ni Wakristo au Waislamu!!

Wakristo kwetu Ulaya hawafuniki vichwa vyao.

Ninacho kifahamu ni kuwa kwenu Ulaya wanawake wanafunika vichwa vyao na wakati mwingine hata nyuso zao, na hakukutokea mabadiliko ila katika karne za hivi karibuni tu vinginevyo angalia bibi zako au mama zao! Na sisi hali kadhalika. Ama wasichana wadogo na haswa Wakristo hupenda kuwaigeni na laiti basi ingekuwa katika jambo zuri.

Kwa nini basi iwe zaidi ni Wakristo?

Kwa sababu dini kwa Waislamu hupaka na hubadilisha maisha ya mtu, na maasi na makosa hayaondoki ila kwa toba, wakati ambapo kwetu sisi Wakristo maisha hubadilika tukiwa Kanisani tu, na inatosha kwetu sisi kuwa Yesu ametukomboa na madhambi yetu wote, hivyo masuala kwetu ni mepesi zaidi.

Nawashukuru sana, lazima tuondoke ili tusije kuchelewa kwani tuna ahadi hotelini.

Kwaherini Amo Said na Amo Sabri, kisha wakaondoka kwenda kwenye gari lao.

Je, umefanikiwa ulichokitaka?

Ndio, akili yangu inataka kupasuka sasa, sijui lakini nahisi kuwa ndani yangu kuna volkano inataka kupasuka, lau kama sio ahadi na Diana na mjomba wake basi ningejaribu kurefusha kikao changu na wale watu wa kawaida wa hali ya chini akina Amo Said na Sabri; wao wanaelezea maisha kwa njia nyepesi na kwa kina, Jamali tafadhali nahisi kutokutaka mazungumzo yoyote kwa sasa.

Vizuri.

Kichwa cha Joji kilikaribia kupasuka kwa swali moja tu “Kitu gani kinachokuzuia na njia ya furaha?”, Je wewe ni muoga? Au ni kwa sababu ni kuwa njia haiko wazi?! Au ni kuwa wewe unajua usiyoyataka wala hujui unayoyataka! Alitamani lau maswali haya yangepungua.

(4)

Tumekaribia hotelini, nimemuita Diana pamoja na mjomba wake katika chakula cha usiku.

Unataka kufanya nini?

Nitamfanya yule msichana aingie katika Uislamu na kuondoa tatizo la mjomba wake.

Vizuri, umekuwa ni mlinganiaji mzuri wa Uislamu, lakini wewe utaingia lini katika Uislamu?

Kama nilivyomwambia Amo Sabri… Mimi nitahifadhi jibu langu mwenyewe. Kichwa changu kinataka kupasuka kwa swali, au huenda nataka kulitoroka, sijui.

Utamlingania vipi katika Uislamu ewe mlinganiaji?!

Asante kwa dharau yako kwangu! Yeye anataka kuingia katika Uislamu lakini anamuogopa mjomba wake, hivyo basi nitaondosha woga huu.

Vipi?

Utaona, kwani tumefika.

La msingi ni kuwa tusilete matatizo kati ya Diana na mjomba wake.

Tumefika katika wakati wenyewe, nitapanda juu niweke mkoba wangu, kisha nitawafuata mara moja mgahawani.

Jamali alifika Mgahawani, akamkuta Diana amekaa na Mjomba wake katika meza moja wakimsubiri Joji, hivyo akakaa pamoja nao.

Joji amepanda juu kuweka mkoba wake na atateremka sasa hivi.

Mimi sijui anataka nini, alipojua tu kuwa mimi ni mjomba wake Diana alisisitiza nile nae chakula cha usiku, je unajua anataka nini?

Huenda Diana akajua….!

Mimi sijui chochote, aliniambia asubuhi kuwa atawasiliana nami anijibu swali langu kwa nini hakuwa Muislamu? Nikakuta kuwa ananiita kwenye chakula cha usiku!

Joji alifika mgahawani, Diana alimuona na kumuashiria kwa mbali, akasogea mezani walipokuwa wamekaa.

Niwatambulisheni, Amir ni Mkurugenzi wa jimbo la Shirika letu hapa Misri na huyu Diana ni Programmer wa Shirika letu na huyu sahiba yangu Muislamu si programmer lakini fani yake ni baba wa Programmer, yaani mwana mahesabu.

Mjomba wangu ndie Mkurugenzi wa shirika lenu?!

Yeye ndie mkurugenzi wa shirika kulingana na fani yake na uwezo wake, na kwa uthibitisho wa wenzake wote, pamoja na kuwa ni Waislamu.

Nakushukuru kwa dhana nzuri kwangu.

Lakini bado nashangazwa kuwa wenzake ni Waislamu pamoja na hayo wamempendekeza!

Diana alitabasamu na kusema:

Nini la ajabu katika hilo?!

La kushangaza ni kuwa baadhi ya Wakristo wanawakataza watu kusilimu.

Amir kwa mshangao.

Kwa sababu hawakuufahamu Uislamu vizuri!

Ewe Amiri una maana kuwa wewe huoni tatizo kwa Mkristo kusilimu?!

Nitakujulisha ninachokiamini, na huenda usipende kusikia nitakachokisema. Mimi sioni tatizo la Mkristo yeyote kuingia katika Uislamu bali huenda usichokijua kutoka kwangu ni kuwa tokea wiki tatu zilizopita nami nakwenda katika moja ya vituo kuujua Uislamu, nani anajua huenda nikasilimu hivi karibuni!

Mjomba wako anaweza kuingia katika Uislamu kinachokuzuia wewe ni nini?

Ha ha ha, sasa nimefahamu, ha ha ha.

Umefahamu nini? Una nini?

Mjomba wangu Amir sie mjomba wangu niliekuelezea.

Vipi? basi huyu ni nduguye mjomba wako uliyenielezea?

Hapana, huenda ukashangazwa ninachokisema, lakini babu yangu ameoa zaidi ya mke mmoja.

Mkristo ameoa zaidi ya mke mmoja?! Simjui Mkristo anayesema kuhusu wake wengi!

Nani amesema hilo? Tuna ambao waliokuwa wakisema kuwa Injili haikatazi wake wengi, bali Papa Markos wa Tano (V) alifungwa; kwa sababu alikataza ndoa ya wanawake wengi na watu walikuwa wanaitaka na wakaungwa mkono na baadhi ya viongozi wa kanisa wanaounga mkono wake wengi. Au inaweza kuwa wake wengi ni bora kuliko mtu kuwa na hawara wengi kama wasemavyo wanawake walioolewa. Kwa hali yoyote ile ni kuwa alipofariki mke wa mjomba wangu akaoa mke mwingine, hivyo basi Amir ni mjomba wangu lakini sie ndugu kwa baba na mama na mjomba wangu Markos niliyekujulisha, lakini ni nduguye kwa baba yake.

Ajabu sana! watu wanataka wake wengi?!

Sasa nimefahamu kwanini umeniita peke yangu ukidhania kuwa mimi ndie niliyemkataza kuingia katika Uislamu.

Ndio.

Diana alibana midomo yake na akasema kwa msisitizo:

Lakini nimefahamu kuwa mwito ni kwa ajili ya kunijulisha ni kwa nini wewe hukusilimu?

JamalI kwa mshangao:

Niruhusuni niingilie, kweli kwa mnasaba ikiwa huku ndiko kujali kwako Diana apate kusilimu; kwa nini wewe basi hukusilimu?

Nimemuuliza swali hili akawa anakimbia majibu na nikadhani kuwa ameniita anijulishe, je unaweza kujibu sasa hivi?

Nitajibu kwa kulazimishwa, mkiniruhusu kuniachia nitawashukuru.

Amir alitabasamu huku akisema:

Kwa nini hujibu, tunataka jibu lakini hatutaki ujihisi vibaya.

Diana akaangalia juu:

Mimi najua jibu lakini nalihifadhi kwa ajili yangu binafsi madamu hutaki kulisema.

Asanteni nyote, lakini sidhani kuna anayefahamu yaliyomo nafsini mwangu!

Wewe ni mwanadamu na unahitaji furaha, na mimi pamoja na mjomba wangu Amir hali kadhalika na kinachokukataza wewe ndicho kinachotukataza sisi wote, iwe ni majasiri au ni waoga, au hata tutakapoficha majibu yetu hata kwa nafsi zetu, chukulia mimi kwa mfano najidanganya na natoa sababu mbali mbali ninaposema mjomba wangu Markos ndie sababu? Lau ningekuwa namiliki ujasiri na uhuru kamili ningechukua maamuzi.

Umenifanya nitahayari, sasa ni nini kinachokuzuia?

Diana alifuta nywele zake kwa mkono wake na akasema:

Kinachonikataza ni ukweli ambao unakukataza wewe na Amir hali kadhalika, kama tulivyo kuruhusu usitujulishe ili usioneshe migongano uliyo nayo mbele ya nafsi yako ndani mwako, kwa nini basi usituruhusu sisi vile vile? Kila mtu ndani ya nafsi yake kuna migongano na matarajio na matamanio yake. Mtu kuwa mkweli wa nafsi yake ni jambo gumu, haswa ikiwa katika maana yake ndio chanzo cha maisha ya mwanadamu na maana ya uwepo wake na maisha yake, na ndio maana mtu anatoroka hayo yote kwa kunywa pombe na kufanya upuuzi…kama nilivyofanya mimi kwa udhaifu wangu wa uwoga!!!!!

Amir alivutiwa na maneno ya Diana na kuathirika nayo, kisha akaangalia chini na kusema:

Ninafahamu vizuri unachosema, ni lazima mtu aishi hali ya kuwa na furaha na kuivumbua nafsi yake, ili amjue Mola wake na aneemeke kwa maisha yake, lakini maamuzi yanahitaji kiasi kikubwa cha uhuru na ujasiri, na wewe Diana umetupa ujasiri na ndio maana ukasema ulichosema.

Jamali akiwa anawaangalia wala hafahamu kitu.

Mimi sijafahamu chochote, ujasiri gani?!

Diana kwa msisitizo pamoja na kuwa sauti yake tulivu ya kina;

Ujasiri wa kuondokana na maradhi ya nafsi, na kuwa juu ya mazingira ya maisha na matamanio yake na mambo yake tata, ujanja na vitimbi vyake. Uhuru wa kuchukua maamuzi ambayo unavuka mipaka ya ulichokizoea na utata wote ambao unaenezwa na vitimbi ambavyo vinaendeshwa. Ujasiri wa kuamini yale yanayofanyiwa juhudi na ulinzi wako hata kama moyo wako unaujua vizuri.

Bado najitahidi kufahamu!

Huenda ikawa vigumu kwako kufahamu kwa sababu umezaliwa Muislamu, ama mimi nimefahamu anachokusudia Diana na nafikiri Joji hali kadhalika.

Diana alitokwa na machozi, alipokuwa akisema:

Ila kama hataki kufahamu, au hataki kudhihirisha kuwa ana fahamu, watu wengi wanazitoroka nafsi zao kwa kudhania kuwa wako katika furaha.

Ilipita akilini mwa Joji hatua zote alizopitia katika msafara wake wa utafiti mbele machoni mwake kama vile mtu anavyoangalia filamu ya haraka haraka, kisha akakumbuka aya zote alizosoma kwenye Qur’an, na mazingira yote aliyopitia. Kadhalika migongano yote ambayo alijaribu kutafutia ufumbuzi na majibu yake. Muangalio wa Joji usiojua pa kushika ulikuwa unatabiri volkano iliyokuwa inatingishika ndani mwake, alijaribu kuficha kwa njia zote lakini hakuweza, hivyo akaamua kuzungumza…

Ndio, nimefahamu.

Nimefahamu pamoja na kuzungumza kwenu kwa mafumbo, ninachowatakia katika jambo la kheri nikuwa msilimu ili mpate furaha ya duniani na huko akhera, na mpate kheri zote zilizo kwenye dini na amesema kweli Mwenyezi Mungu aliposema: “Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini.” (5:3). Kwa hivyo neema imekamilika na dini imekamilishwa kwa Uislamu huu.

Nadhani nimefahamu vizuri nilichokuwa nikikitafuta kwa muda mrefu.

Nini ulichokuwa ukikitafuta?

Nilikuwa naitafuta nafsi yangu, na maana ya maisha yangu na kuwepo kwangu… natafuta nuru ya Tawhidi na uzuri wa maisha… natafuta starehe ya roho, akili na nafsi.

Diana alifuta machozi yake huku akisema:

Hilo hilo nililokuwa nikitafuta!

Nimepata uzi mrefu ambao unaweza kushona na kusuka shanga za maisha yangu ili uwe mkufu mzuri, sasa nimefahamu vizuri kabisa kwa nini nimeumbwa?! Kwa nini ninaishi?!

Mimi sijafahamu chochote? Je unaweza kuniambia ulichofahamu?!

Uso wa Diana uling’aa kwa tabasamu pana kisha akasema:

Kiasi gani napata hisia zako! Wewe ndie mwenye uhuru zaidi yetu na ujasiri, ni uzuri ulioje wa mtu kuwa mkweli wa nafsi yake.

Nimefahamu ninachotaka, na nimemfahamu Adam na Mutwi Rahman na kadhalika nimemfahamu Levi vile vile. Tom, Katarina, Habib, Maiko na John Luke na Kakhi wote nimewafahamu, lakini lililo muhimu zaidi ni kuwa Joji sasa amefahamu maana ya maisha!

Sijafahamu chochote!!! Majina gani haya uliyoyataja?

Macho ya Amir yalijaa machozi na kusema:

Nami sasa nimefahamu Joji, ni uzuri ulioje kutoka kwako!

Kadhalika nimefahamu maneno ya Kikongwe kuhusu njia ya furaha.

Kikongwe? Je unaweza kutuelekeza njia ya furaha?!

Roho yangu imenijibu, nimeisikia sasa hivi, wote nyinyi mnanidai (kwa wema huu mlionifanyia)

Roho yako imekujibu?!

Ndio, nilijitenga na roho yangu, akili yangu, elimu yangu ilishajua njia lakini roho yangu ilikuwa mbali kabisa.

Amir alikodoa macho yake kwa mshangao, kisha akasema:

Inaelekea unanieleza nilivyo, roho yako imekuambia nini?

Imeniambia; iweje dunia ikanyooka pamoja na akhera, na vipi nafsi itanyooka na tawhidi ambayo ndio inaipa uhai maana yake.

Taathira ile ilifikia kikomo kwa Diana akiwa anafuta machozi yake…

Dunia imenyooka na akhera?!

Na roho inakutana na elimu na akili na nafsi na hivyo vikakumbatiana badili ya kuangushana na kupigana mieleka, ni kiasi gani migongano yao ikinipa tabu kubwa!

Vizuri, ni uzuri ulioje mambo yanapokuwa wazi! Vipi roho yako iliokutana pamoja nawe sasa hivi?

Uso wa Joji uling’aa akiwa anasema:

Zilikutana raha ya kiwiliwili pamoja na roho, ukawaida ukakutana na kina cha mambo, dunia ikakutana na akhera na maadili yakakutana na maslahi….

Vizuri, vizuri.

Mimi kesho jioni nasafiri kwenda London; ili nimpe habari nzuri kuwa nimefahamu na nimepata njia ya furaha, ni kiasi gani nilidhulumu nafsi yangu na kupoteza umri wangu.

Ni nani ambae utamjulisha?

Yule kikongwe aliyenihakikishia kuwa roho yangu ndiyo ambayo itapata njia ya furaha.

Na vipi kuhusu shirika ambalo utalifungua hapa?

Nitamalizia matayarisho yake kesho asubuhi, na ndege yangu ipo saa mbili usiku, kesho kutwa Ijumaa. Ninataka kumjulisha kikongwe kuwa nimeisikia roho yangu na maisha yangu na nimefahamu; hivyo basi maisha yangu na roho yangu yameratibika natamani kuwasiliana na kila mmoja katika marafiki zangu sasa hivi, ni mwenye furaha sasa, mimi ni mwenye furaha kwa sasa nimeipata njia.

Nakupongeza Joji.

Naombeni ruhusa na nisameheni, ningependa kwenda chumbani kwangu hivi sasa mara moja.

Joji alipanda chumbani kwake na kuwaandika marafiki zake email ya pamoja:

“Enyi Rafiki zangu, enyi mliosafiri nami kutafuta njia ya furaha, kwa hakika nimeipata, nimeipata, nimeipata. Nina furaha sana, nimejua majibu ya maswali yangu yaliyokuwa yakinitatiza na kunipa woga. Nyote mnastahiki kupanua vifua vyenu na nuru ya nyoyo zenu. Nyote mnastahiki raha ya dhamira zenu na mng’ao wa Tawhidi. Nyote mnastahiki raha ya roho na shauku zake. Nyote mnastahiki mnyooshe (Istiqama) dunia na mazuri ya maisha. Nyote mnastahiki mpate furaha ya dunia na akhera. Nawapendeleeni kheri na njia ya furaha ambayo nimeipata, naam nimeipata, roho yangu imekutana na akili na nafsi yangu, kadhalika dunia imekutana na akhera, raha za kiwiliwili zimekutana na roho. Kwa hakika nafsi yangu iliyokuwa imeparaganyika sasa imekutana, kwa hakika imejibu maswali yangu yote…Ni njia ya furaha! Uhimidiwe wewe Rahimu ewe Mkarimu. Ndugu yenu awapendae Joji Neson.”