NJIA YA REHEMA

NJIA YA REHEMA

NJIA YA REHEMA

Allah ni mwenye huruma

Sura nyingi katika Qur-aan zimeanza kwa kutaja majina mawili ya Allah (Rahmanir Rahiym) katika kila sura, na Mwenyezi Mungu akajiandikia mwenyewe rehema: “…Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema…”(6:54),

Na rehema yake imeenea kila kitu: “…Na rehema yangu imeenea kila kitu….” (7:156),

Na watu wakajipendekeza katika rehema yake na akawabashiria nayo na akawatahadharisha kutokata tamaa: “Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (39:53);

Ni yeye Aliyetakasika ni mwingi wa rehema hupenda kusamehe; amesema (Swala Llahu ‘alayhi wasallam). “Hakika Allah Ta’ala hukunjua mkono wake usiku ili watubie mkosaji wa mchana, na hupanua mkono wake mchana ili watubie waliokosa usiku hadi linyanyuke jua kutoka Magharibi yake.” (Muslim).

Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) akatujulisha kuhusu Mola wake, kasema: “Hakika Allah ameandika kitabu (Qur-aan) kabla hajaumba viumbe kuwa rehema yangu imetangulia ghadhabu yangu.” (Bukhari na Muslim).

Amesema Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) kuhusu rehema ya Mola wake: “Allah amejaalia rehema katika sehemu mia moja, akashusha sehemu tisini na tisa, na akateremsha ardhini sehemu moja, katika sehemu hiyo moja ndio wanayohurumiana viumbe kiasi cha kumfanya farasi akanyanyua mguu wake kwa kuhofia kumkanyaga mwanae.” (Al-Bukhari).

Allah akamtuma Nabii wake (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) kuwa ni rehma (huruma) kwa walimwengu: “Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.”(21:107);

Na akaipendezesha kwa tabia njema za juu; hivyo Allah akasema: “Na hakika wewe una tabia tukufu.” (68:4),

Na hiyo ilikuwa ni katika tabia zake ziliopambanuliwa yeye Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) ni hiyo Rehema; vinginevyo wangetawanyika walio pembizoni mwake na kumuacha peke yake. Allah Ta’ala amesema: “Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia….” (3:159),

Bali yeye Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) ni Mpole, mwenye huruma, hatakii tabu Ummah wake (Swala Llahu ‘alayhi wasallam), Allah Ta’ala amesema: “Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.” (9:128).

Hivyo basi Uislamu uliokuja kutoka kwa mwingi wa Rehema Aliyetakasika na akatumwa nao Mwingi wa rehema kwa Ummah wake (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) na kuwa ni rehema kwa Walimwengu, kuwatoa katika uovu wa udhalimu na chuki, na kuwatoa kwenye aina za huzuni, wasiwasi, woga, katika njia ya kulipiana kisasi, makosa, ukandamizaji na udikteta, akaja kama rehema kwa Walimwengu: “Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.”(21:107).

Ni rehema kwa Waislamu na rehema kwa wasiokuwa Waislamu, ni rehema kwa wanaotii na ni rehema kwa wenye inadi, ni rehema kwa wakubwa, wadogo, wanaume, wanawake, watoto, matajiri kwa masikini, ni rehema kwa Walimwengu.

Uislamu ni rehema kwa walimwengu

Na hivyo Uislamu ukaja kwa kuomba rehema na kutamanisha na kuusiana, Allah amesema: “Tena awe miongoni mwa walio amini na wakausiana kusubiri na wakausiana kuhurumiana.” (90:17)

Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: “Allah hamrehemu asiyehurumia watu.” (Bukhari na Muslim).

Aina za waliohusishwa na rehma

Na akasema (Swala Llahu ‘alayhi wasallam): “Wenye kuhurumia atawahurumia Rahmaan, Wahurumieni waliopo ardhini mtahurumiwa na Aliye mbinguni, Kizazi (udugu) ni huruma kutoka kwa Rahmaan atakayekiunga Allah atamuunga na atakayekikata Allah atamkata.” (Al-Tirmidhi).

Na akasema Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam), “Rehema haiondolewi isipokuwa kwa muovu.” (A-Tirmidhi); Kwa hiyo, Allah akaamrisha Rehma na akahimiza hilo kwa sifa ya ujumla, kama vile tabia na mfumo wa maisha na sheria ikahusisha aina maalumu za huruma miongoni mwa hizo:-

1-Huruma kwa watu wote: Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) akawa ni mwenye huruma kwa Ummah wake, Allah aliwaongoa kupitia Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) kutoka katika kiza kwenda kwenye nuru, na kutoka kwenye uovu hadi kwenye furaha lakini huruma yake Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) ilipita hayo na hadi akahimiza huruma kwa Makafiri ambao bado hawajasilimu, Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) alisema kuhusu watu wa Makkah ambao hawajasilimu: “…Bali natarajia Allah atoe migongoni mwao wenye kumuabudu Allah peke yake wala hatomshirikisha chochote.” (Bukhari na Muslim). Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) alipojeruhiwa katika vita vya Uhud, Maswahaba wake walimwambia, “(waapize) washirikina adhabu; Mtume (akaomba); “Ewe Mola wangu! waongoze watu wangu kwani hawajui”, na katika riwaya: ikasemwa Ewe Mtume wa Allah; “Waombee adhabu Washirikina.” Mtume akasema: “Sijatumwa kulaani, bali nimetumwa kuwa Rehema.” (Muslim).

2-Huruma kwa Wadogo; Mmoja katika Sahaba za Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: Tuliingia pamoja na Mtume wa Allah kwa Ibrahim nae akiwa anaugulia, macho ya Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) yakawa yamelengwa na machozi, AbdurRahman bin Auf akasema, “ Na wewe Mtume wa Allah? Akasema (Mtume), “Ewe Ibn Auf hiyo ni Rehma,” Kisha akasema: “Kwa hakika macho yanatoka machozi, na moyo unahuzunika, wala hatusemi ila lile linalomridhisha Mola wetu, na kwa hakika kuachana nawe Ibrahim tunahuzunika sana.” (Bukhari na Muslim).

Bali Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) alikuwa akimkalisha Usama katika paja lake na Al-Hassan katika paja lake lingine, kisha huwakumbatia na kusema: “Ewe Mola wangu wahurumie kwani mimi ninawahurumia.” Mtu mmoja alipoingia kwa Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) akamuona Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) akimbusu Al-Hassan au Al-Hussein, akamwambia: “Je, mnawabusu watoto wenu?!, Mimi nina watoto kumi sijawahi kumbusu yeyote kati yao, Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) akasema: “Asiyehurumia hatohurumiwa.”

3-Kuwahurumia Wanyonge; Wakati Fulani Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) alimtafuta mwanamke mmoja mweusi aliyekuwa akisimamia msikiti, akamuulizia wakasema: “Amekufa”, akasema: “Kwanini hamkunijulisha? Nielekezeni lilipo kaburi lake.” Wakamuonesha nae akamswalia.” (Al-Bukhari na Muslim). Mtumishi wa Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) Anas bin Malik (r.a.) amesema: “Nimemtumikia Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) kwa muda wa miaka kumi hakuwahi kuniambia Aah, wala kwa nini umefanya, au kwa nini hukufanya.” (Al-Bukhari).

Sahaba Mtukufu Ibn Masuud anasema;”Nilikuwa nikimpiga kijana wangu nikasikia sauti kutoka nyuma yangu ikisema: “Fahamu Ewe Abu Masuud Allah ana uwezo zaidi juu yako kuliko uwezo wako juu yake, nilipogeuka nikamuona Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam), nikasema: “Ewe Mtume wa Allah yeye yupo huru kwa ajili ya Allah, Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) akasema: Kama usingefanya hivyo basi moto ungekubabua au ungekushika.” (Muslim).

4-Huruma kwa Wanyama: Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) alipita akamuona mnyama mgongo wake umekutana na tumbo lake, akasema: “Muogopeni Allah kwa wanyama hawa (wasioweza kuzungumza), wapandeni wakiwa wazima, na waleni wakiwa wazima.” (Abu Dawuud).

$Lauren_Booth.jpg*

Lauren Booth

Mwanaharakati wa haki za Binadamu wa Uingereza.
Amani, Utulivu na Usalama
“Rukuu na Sijida katika Swala ya Waislamu hushibisha nafsi amani, utulivu na usalama. Kila mmoja huanza Swala yake kwa Bismillahir Rahmanir Rahym na humalizia kwa Asalaam Alaykum.”

Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) alipoingia katika nyumba ya Mtu katika Answar alimuona ngamia, Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) alipomuona alianza kunung’unika na machozi kumtoka, Mtume akamuendea na kufuta machozi yake, akanyamaza, (Mtume) akasema: “Ni nani mwenye ngamia huyu?, Ni ngamia wa nani? Akaja kijana wa Kianswari, akasema: Ni wangu Ewe Mtume wa Allah, akasema: “Je, humuogopi Allah kwa mnyama huyu aliyekumilikisha Allah, amenishitakia kuwa unamnyima chakula na unamtelekeza.” (Abu Dawuud).

Hii ni mifano ya kutumwa kwake Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) kuwa ni rehema kwa Walimwengu, vinginevyo ubainifu wa rehema na utekelezaji wake katika Uislamu ni mwingi sana ambao unabainisha njia ya dini hii, lakini rehma hii haina maana ya udhalili bali ni rehma ya utukufu.