MISINGI YA DA’WAH YA MITUME

MISINGI YA DA’WAH YA MITUME

MISINGI YA DA’WAH YA MITUME

Misingi yao ni moja

Da’wah ya Mitume yote imewafikiana katika misingi maalumu; msingi wa da’wah ya Mitume ni mmoja, Allah Ta’ala amesema: “Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia wewe, na tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo…” (42:13);

Na ndio maana dini ya Mitume yote ikawa ni moja, Allah amesema, “Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayo yatenda. Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi. ” (23:51-52),

Pamoja na sheria zake kutofautiana, Allah amesema, “Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sharia yake na njia yake” (5:48),

Na lau sheria zingetokea kuwa kinyume na misingi ile basi ingetokea katika hekima, maslahi na huruma, bali ni muhali kuja kinyume na aliyokuja nayo, Allah amesema: “Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani…” (23:71),

Imani na Tawhidi

Na katika kadhia mbalimbali ambazo Mitume wameafikiana na katika ujumbe wake mbali mbali ni:- -Kumuamini Allah, Malaika wake, kitabu chake, Mitume wake, Siku ya Mwisho, na Qadar kheri na shari yake, Allah Mtukuka amesema: “Mtume ameamini yaliyo teremshwa kwake kutoka kwa Mola Mlezi wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumet’ii. Tunakutaka maghfira Mola Mlezi wetu! Na marejeo ni kwako.” (2:285).

Amri ya kumuabudu Allah Peke Yake bila ya kumshirikisha yeye na chochote na kumtakasa na kuwa na mke na mtoto, mfano na kuabudu masanamu, Allah Mtukuka amesema: “Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu” (21:25)

Vivyo hivyo amri ya kufuata njia yake, na kutofuata njia tofauti, na kutekeleza ahadi, na kupima sawa sawa kwa kilo na mizani na wema kwa wazazi wawili na uadilifu baina ya watu na ukweli katika kauli na amali, na kuharamisha maovu yaliyodhihiri na yaliyojificha na uovu na kudhulumu, na kuharamisha kuua watoto, na kuua nafsi pasina haki, na kukataza riba na kula mali ya mayatima, na kukataza ubadhirifu na kiburi na kula mali za watu kwa batili. Imani ya siku ya mwisho; kila mtu ana elimu ya yakini kuwa kuna siku ambayo atakufa, lakini nini baada ya kifo chake? Je, ni mwenye furaha au huzuni? Na kila Mitume na Manabii walifikisha na kuwaambia watu wao kuwa watafufuliwa na kulipwa malipo yao, ikiwa kheri basi atalipwa kheri na ikiwa shari atalipwa shari, na jambo hili la kufufuliwa na kuhesabiwa-akili zilizo salimika zinalikubali, na kuungwa mkono na sheria za Mwenyezi Mungu, kwa hakika Muumba mwenye uwezo, mwenye elimu, mwenye hekima ametakasika kuumba viumbe hivi hivi kwa mchezo na bila ya lengo na kuwaacha hivi hivi tu. Allah amesema, “Na hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yao bure. Hiyo ni dhana ya walio kufuru. Ole wao walio kufuru kwa Moto utao wapata.” (38:27)

Bali amewaumba viumbe wake kwa hekima kubwa, na kwa lengo tukufu zaidi, Allah amesema, “Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi” (51:56)

Si laiki kwa (Mwenyezi) Mungu huyu mwingi wa hekima kuwafanya sawa wenye kutii na waasi na wale wenye kumfuata na kumuasi Allah amesema, “Je! Tuwafanye walio amini na wakatenda mema kama wafanyao uharibifu katika nchi? Au tuwafanye wachamngu kama waovu?” (38:28);

$Debora Botter.jpg*

Deborah Potter

Mwanahabari wa Kimarekani
Misingi Misafi
“Uislamu sio dini mpya kutoka kwa Muhammad, lakini ilipoanza kusambaa ardhini baada ya kupita miaka mia sita ya kupaishwa mbinguni kwa masihi. WAHYI wa pili ulianza kushuka, ulikuwa ni ule ule unaounga dini za mbinguni na kuzirejesha kwenye asili yake safi. Mitume wote waliotumwa na Mwenyezi Mungu walikuwa Waislamu na ujumbe wao ulikuwa ni mmoja daima.”

Hivyo basi ilikuwa ni ukamilifu wa hekima yake na ukubwa wa kudura yake Yeye Allah kuwalipa waja wake kwa matendo yao Siku ya Kiama; hivyo basi mwema atapewa thawabu na atamuadhibu mkosaji, Allah amesema: “…ili awalipe kwa uadilifu wale walio amini na wakatenda mema. Na walio kufuru, wao watapata vinywaji vinavyo chemka, na adhabu chungu kwa sababu ya walivyo kuwa wakikufuru.”(10:4);

Hivyo basi ni wepesi kiasi gani kuhuisha watu kwa ajili ya kuhesabiwa kwao baada ya mauti, si ndio yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) aliyeumba Mbingu na Ardhi?! Na Yeye Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) ameumba viumbe bila mfano uliotangulia, Je, hawezi kurudi kuumba mara nyingine?! Allah amesema: “Je! Hawaoni ya kwamba Mwenyezi Mungu, aliye ziumba mbingu na ardhi, na hakuchoka kwa kuziumba, kuwa ni Muweza wa kuwafufua wafu? Kwani? Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.” (46:33)

Na akasema Mtukuka: “Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi.” (36:81)

Kwa hiyo mwenye kuweza kuanzisha kitu mwanzoni ana uwezo wa kukirejesha tena, Allah amesema: “Na Yeye ndiye anaye anzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara nyengine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.” (30:27);

$Dr._Laura_VecciaVaglieri.jpg*

Laura VecciaVaglieri

Mustashrik wa Kitaliano
Tawhidi halisi
“Mtume wa Waarabu Muhammad kwa sauti kutoka kwa Mola wake, amewaita waabudu masanamu, wafuasi wa Ukristo na Uyahudi yaliyopotoka kwenye dini safi ya Tawhidi, na hivyo kuridhia kuingia katika mgogoro mkubwa pamoja na makundi mengine ya watu ambayo yanampeleka mtu katika kumshirikisha Muumba na miungu mingine.”

Bali ilishatokea kufufuliwa kwa wafu katika maisha haya ya duniani kwa idhini ya Mwenyezi Mungu mbele ya Nabii Ibrahim (‘Alahyi Salaam), “Na alipo sema Ibrahim: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe vipi unavyo fufua wafu. Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue. Akamwambia: Twaa ndege wane na uwazoeshe kwako, kisha uweke juu ya kila kilima sehemu, kisha wete, watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.” (2:260)

Na ilitokea hivyo hivyo kwa Issa (‘Alahyi Salaam) kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Allah amesema, “Na pale Mwenyezi Mungu atapo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipo kutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utuuzimani. Na nilivyo kufunza kuandika na hikima na Taurati na Injili. Na ulipo tengeneza udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ikawa ndege kwa idhini yangu; na ulipo waponesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu; na ulipo wafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipo kukinga na Wana wa Israili ulipo wajia na hoja zilizo wazi, na wakasema walio kufuru miongoni mwao: Haya si lolote ila ni uchawi mtupu!” (5:110).