Tarekh ya mitume:Musa

Tarekh ya mitume:Musa

Tarekh ya mitume:Musa

Kuuliwa kwa watoto wa kaumu ya Musa

Bani Israil walikuwa wakisomeshana wenyewe kuhusiana na Mtume Ibrahim (‘Alahyi Salaam) kuwa katika kizazi chake atatoka kijana ambae mfalme wa Misri ataangamia kwa mikono yake, utabiri huu ulikuwa ni maarufu kwa Bani Israil. Habari zile zikafika kwa Firauni na maamiri wake walimueleza habari hiyo, hivyo kuamuru kuuwawa kwa wavulana wa Bani Israil kwa kutahadhari na kuwepo kwa kijana huyo. Zama hizo Bani Israil walikuwa wanaishi kwa kuonewa shida na dhuluma kubwa kutoka kwa Firauni: “Hakika Firauni alitakabari katika nchi, na akawagawa wananchi makundi mbali mbali. Akalidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na akiwaacha watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa katika mafisadi.” (28:4)

Allah akataka kuwaneemesha waliodhoofishwa miongoni mwa Bani Israil: “Na tukataka kuwafadhili walio dhoofishwa katika nchi hiyo na kuwafanya wawe waongozi na kuwafanya ni warithi. Na kuwapa nguvu katika nchi, na kutokana na wao kuwaonyesha kina Firauni na Hamana na majeshi yao mambo yale waliyo kuwa wakiyaogopa.” (28:5-6).

Kisa cha kuzaliwa na kukua kwake

Pamoja na Firauni kujihadhari na kukwepa kutopatikana Musa, kiasi cha kuwafanya askari wake wakiwazungukia wenye mimba na wakijua tarehe za kuzaa kwao, hivyo basi alikuwa hazai mwanamke yoyote mtoto wa kiume isipokuwa watamchinja wachinjaji hao muda ule ule, Lakini Allah alitaka kumuoneshe Firauni, Hamana na majeshi yake walichokua wakitahadhari. Pindi mama yake Musa alipozaa: “Tulimfunulia mama yake Musa kwa kumwambia: Mnyonyeshe. Na utakapo mkhofia basi mtie mtoni, na usikhofu wala usihuzunike. Hakika Sisi tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa Mitume.” (28:7)

Hivyo akawa na khofu juu yake, akamuweka katika sanduku la mbao na kumtupa mtoni:“Basi wakamwokota watu wa Firauni, aje kuwa adui kwao na huzuni. Hakika Firauni na Hamana na majeshi yao walikuwa wenye makosa.” (28:8).

Mapenzi ya Musa yakaingizwa moyoni mwa mke wa Firauni: “Na mkewe Firauni alisema: Atakuwa kiburudisho cha macho kwangu na kwako. Msimuuwe! Huenda akatufaa, au tumpange kuwa mwenetu. Wala wao hawakutambua.” (28:9)

Ama mama yake Musa: “Na moyo wa mama yake Musa ukawa mtupu. Alikuwa karibu kumdhihirisha, ingeli kuwa hatukumtia nguvu moyo wake ili awe miongoni mwa Waumini. Naye akamwambia dada yake Musa: Mfuatie. Basi naye akawa anamuangalia kwa mbali bila ya wao kujua.” (28:10-11) “Na tukamjaalia awakatae wanyonyeshaji wote tangu mwanzo, mpaka dada yake akasema: Je! Nikuonyesheni watu wa nyumba watakao mlea kwa ajili yenu, nao pia watakuwa wema kwake? Basi tukamrudisha kwa mama yake ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike. Na ajue ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, lakini wengi wao hawajui.” (28:12-13).

Musa akakulia katika nyumba ya dhalimu muovu Firauni: “Na Musa alipo fika utu-uzima baraabara, tulimpa akili na ilimu. Na hivi ndivyo tunavyo walipa walio wema. Na akaingia mjini wakati wa kughafilika wenyeji wake, na akakuta humo watu wawili wanapigana - mmoja ni katika wenzake, na mwengine katika maadui zake. Yule mwenzake alimtaka msaada kumpiga adui yake. Musa akampiga ngumi, akamuuwa. Akasema: Hiki ni kitendo cha Shet’ani; hakika yeye ni adui, mpotezaji dhaahiri. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu; basi nisamehe. Akamsamehe; hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. Akasema: Mola wangu Mlezi! Kwa ulivyo nineemesha, basi mimi sitakuwa kabisa msaidizi wa wakosefu.” (28:14-17).

Pamoja na Nabii wa Allah Shu'aib

Lakini baada ya kuua adui yake na adui wa Bani Israil: “Akapambazukiwa mjini asubuhi naye ana khofu, akiangalia huku na huku. Mara yule yule aliye mtaka msaada jana akawa anampigia kelele amsaidie. Musa akamwambia: Hakika wewe ni mgomvi kweli kweli. Basi alipo taka kumshika kwa nguvu yule aliye adui wao wote wawili, akasema: Ewe Musa! Unataka kuniuwa kama ulivyo muuwa mtu jana? Wewe hutaki ila kuwa jabari katika nchi, wala hutaki kuwa miongoni mwa wenye maslaha.. Na akaja mtu kutoka mwisho wa mji akipiga mbio, akasema: Ewe Musa! Wakubwa wanashauriana kukuuwa. Basi toka! Hakika mimi ni katika wanao kupa nasaha. Basi akatoka, naye ana khofu, akiangalia huku na huku. Akasema: Mola wangu Mlezi! Niokoe na watu madhaalimu.” (28:18-21),

Aliondoka Misri na kuelekea Madyan: “Na alipo elekea upande wa Madyana alisema: Asaa Mola wangu Mlezi akaniongoa njia iliyo sawa. Na alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao wanawake wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachunga. Na baba yetu ni mzee sana. Basi Musa akawanyweshea; kisha akarudi kivulini, na akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mhitaji wa kheri utakayo niteremshia.” (28:22-24).

Wale wasichana wawili wakamwambia baba yao –Nabii wa Allah Shu’ayb –alichokuwa nacho, Nabii wa Allah Shu’ayb (‘Alahyi Salaam), akamtuma mmoja wa binti zake kwa Musa (‘Alahyi Salaam): “Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea….” (28:25).

Musa akafika kwa Shu’ayb (‘Alayhima salaam): “…Basi alipo mjia na akamsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwisha okoka kwenye watu madhaalimu.” (28:25),

Binti yake mmoja alipoona uaminifu wa Musa (‘Alahyi Salaam): “Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu.” (28:26)

Shu’ayb akamtaka Musa (‘Alayhima salaam): “Akasema: Mimi nataka kukuoza mmojawapo katika binti zangu hawa wawili kwa kunitumikia miaka minane. Ukitimiza kumi, khiari yako; lakini mimi sitaki kukutaabisha. Inshallah utanikuta miongoni mwa watu wema. Musa akasema: Hayo yamekwisha kuwa baina yangu na wewe. Muda mmojapo nikiumaliza sitiwi ubayani. Na Mwenyezi Mungu ni Mlinzi juu ya haya tunayo yasema. ” (28:27-28).

Kumlingania Firauni

Musa alipomaliza muda wake alisafiri kwenda kwa watu wake: “Basi alipo timiza muda wake na akasafiri na ahali zake, aliona moto upande wa Mlima T’uri. Akawaambia ahali zake: Ngojeni! Mimi nimeona moto, labda nitakuleteeni kutoka huko khabari au kijinga cha moto ili mpate kuota moto.” (28:29),

Hapo ndipo Allah alipomteremshia Wahyi: “Basi alipo ufikia aliitwa kutoka ng’ambo ya bonde la kuliani katika eneo lilio barikiwa kutoka kwenye mti: Ewe Musa! Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote. Na tupa chini fimbo yako. Basi alipo iona ikitikisika kama nyoka, akarudi nyuma wala hakutazama. (Akaambiwa): Ewe Musa! Njoo mbele wala usiogope. Hakika wewe ni miongoni mwa walio salimika. Ingiza mkono wako kwenye mfuko wako, utatoka mweupe pasipo na ubaya. Na jiambatishe mkono wako ukihisi khofu. Basi hizi ni dalili mbili zitokazo kwa Mola wako Mlezi kumpelekea Firauni na wakuu wa umma wake. Hakika hao walikuwa watu mafaasiki.” (28:30-32),

Lakini Musa alimuogopa Firauni kwa sababu alimuua adui yake hapo kabla, na kwa sababu ya fundo lililo kwenye ulimi wake: “Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nilimuuwa mtu katika wao, kwa hivyo naogopa wataniuwa. Na ndugu yangu Harun ni fasihi zaidi ulimi wake kuliko mimi. Basi mtume ende nami kunisaidia, ili anisadikishe. Hakika mimi nina khofu watanikadhibisha.” (28:33-34).

Akamuomba Allah amfanye ndugu yake Harun, Waziri: “Na nipe waziri katika watu wangu, Harun, ndugu yangu. Kwake yeye niongeze nguvu zangu. Na umshirikishe katika kazi yangu. Ili tukutakase sana. Na tukukumbuke sana. Hakika Wewe unatuona. Akasema: Hakika Umepewa maombi yako, ewe Musa! ” (20:29-36).

Walipokwenda kwa Firauni na kumfikishia waliyotumwa katika kumlingania yeye kumuabudu Allah Ta’ala peke yake bila kumshirikisha na chochote na kufungua mateka wa Bani Israil na kuacha kuwakamata, kuwatenza nguvu na kuwanyanyasa na awaache wamuabudu Mola wao watakavyo, na wajishughulishe na kumpwekesha Allah peke yake na kunyenyekea kwake. Firauni akatakabari na kupetuka mipaka na akamuangalia Musa kwa jicho la dharau na kebehi akimwambia: “(Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi? Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani? ” (26:18-19).

Musa akamjibu: “(Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea.” (26:20);

Yaani kabla sijateremshiwa Wahyi na kupewa utume: “Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume.” (26:21),

Kisha akasema akimjibu Firauni alivyojisifu kumlea na kumfanyia wema: “Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili?” (26:22);

Yaani neema hii uliyoitaja ya kwamba ulinifanyia mema na mimi ni mtu mmoja katika Bani Israil na kwa upande wa pili umewatumikisha watu hawa wa Bani Israil kwa ukamilifu na kuwafanya kuwa watumwa katika kukutumikia na kukuhudumia katika shughuli zako. Kisha Firauni akamuulizia Mola ambae Musa anamlingania: “Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote?” (26:23),

Likaja jibu linalo kinaisha: “Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.” (26:24),

Firauni akaanza kebehi: “(Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi?” (26:25),

Musa akaendelea na kulingania watu wote: “(Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza.” (26:26),

Firauni akazidisha uovu wake: “(Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu.” (26:27),

Hata hivyo, Mtume wa Allah Musa hakuacha kadhia yake: “(Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini.” (26:28),

Dikteta mkubwa mwenye kiburi na kujikweza Firauni aliyekosa hoja na akili na mantiki alianza vitisho: “(Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani.” (26:29),

Kama ambavyo kebehi na dharau za Firauni hazikumuondosha Musa katika da’wah yake, hata vitisho vya Firauni havikumfanya kuacha da’wah yake; hivyo alimjibu: “Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi? Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli. Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri. Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao.” (26:30-33),

Firauni akaogopea watu wasije kumuamini (Musa), hivyo akawaambia watu wake: “(Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu. Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani? Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo. Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu. ” (26:34-37)

Kisa cha wachawi wa Firauni

Baada ya Firauni kuona hoja zote alifanya jeuri na kukana na kukataa: “Na hakika tulimwonyesha ishara zetu zote. Lakini alikadhibisha na akakataa. Akasema: Ewe Musa! Hivyo umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako? Basi sisi hakika tutakueletea uchawi kama huo. Basi weka miadi baina yetu na wewe, ambayo tusiivunje sisi wala wewe, mahali patapo kuwa sawa. Akasema: Miadi yenu ni siku ya Sikukuu; na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri. Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha akaja. ”(20:56-60),

Musa akawaogopea kupata adhabu ya Allah: “Musa akamwambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akakufutilieni mbali kwa adhabu. Na mwenye kuzua lazima ashindwe!” (20:61);

Hivyo wakatofautiana, baadhi yao wakasema: haya si maneno ya mchawi: “Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe, na wakanong’ona kwa siri.” (20:62).

Lakini wao wakarejea, wengi wao wakasema: “Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wao, na waondoe mila zenu zilizo bora kabisa. Kwa hivyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa yakini atafuzu kweli kweli leo atakaye shinda.” (20:63-64) “Akasema: Bali tupeni nyinyi! Tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinapiga mbio. ” (20:66)

Musa akaogopea wale wachawi wasije wakawafitinisha: “Basi Musa akaingia khofu nafsi yake.” (20:67),

Allah akamteremshia Wahyi; Musa: “Tukasema: Usikhofu! Hakika wewe ndiye utakaye shinda. Na kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia; kitavimeza walivyo viunda. Hakika walivyo unda ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo.” (20:68-69), “Nasi tukamfunulia Musa kumwambia: Tupa fimbo yako. Mara ikavimeza vyote vile walivyo vibuni. Kweli ikathibiti na yakabat’ilika waliyo kuwa wakiyatenda.” (7:117-118),

Kwa ghafla (likatokea jambo lisilotarajiwa): “Kwa hivyo walishindwa hapo, na wakageuka kuwa wadogo. Na wachawi wakapoomoka wakisujudu. Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa viumbe vyote, Mola Mlezi wa Musa na Haarun.” (7:119-122), “Basi wachawi wakaangushwa wanasujudu. Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa Harun na Musa! ” (20:70),

Vitisho vya Firauni vikaonekana kama upumbavu: “(Firauni) akasema: Oh! Mnamuamini kabla sijakupeni ruhusa? Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliye kufundisheni uchawi. Basi kwa yakini nitakukateni mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakutundikeni misalabani katika vigogo vya mitende…. ” (20:71),

Jibu lao halikutarajiwa kwa Firauni, na huu ni uthibitisho wa wazi jinsi Imani inavyomfanya aliyeamini: “Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi. Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini.” (26:50-51).

Kuangamia na kuzama kwa Firauni

Firauni akaendelea kuwaudhi waumini; Allah akamuadhibu pamoja na walio nae: “Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa miyaka (ya ukame) na kwa upungufu wa mazao, ili wapate kukumbuka. Likiwafika jema wakisema: Haya ni haki yetu. Na likiwafika ovu husema: Musa na walio pamoja naye ni wakorofi. Hakika ukorofi wao huo unao wafikia unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui. ” (7:130-131),

Hawakuamini wala kutubia: “Na wakisema: Hata ukituletea Ishara yoyote kutuzuga hatuto kuamini. Basi tukawapelekea tufani, na nzige, na chawa, na vyura, na damu, kuwa ni Ishara mbali mbali. Nao wakapanda kiburi, na wakawa watu wakosefu.” (7:132-133),

Walipochoka: “Na ilipo waangukia adhabu wakasema: Ewe Musa! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa aliyo kuahidi. Ukituondolea adhabu hii hapana shaka tutakuamini, na tutawaachilia Wana wa Israili wende nawe. Lakini tukiwaondolea adhabu mpaka muda fulani wao waufikie, mara wakivunja ahadi yao.” (7:134-135),

Hawakutekeleza waliyoyaahidi, bali walitengua waliyoyasema: “Basi tuliwapatiliza, tuka-wazamisha baharini kwa sababu walizikanusha Ishara zetu, na wakaghafilika nazo.” (7:136).

Watu wa Misri walipozama katika ukaidi, ukafiri na inadi yao na kumfuata mfalme wao, na kwenda kinyume na Nabii wao na Mtume wao Musa bin Imran (‘Alahyi Salaam), na baada ya Allah kuwasimamishia hoja kubwa na kuwaonesha miujiza, lakini pamoja na yote hayo hawakuacha wala hawakurudi nyuma, na hawakuamini isipokuwa wachache miongoni mwa kaumu ya Firauni.

Ama wachawi wote, na Bani Israil wote, Imami zao zilikuwa za kificho kwa kumuogopa Firauni na dhuluma zake, ujeuri na ubabe wa utawala wake. Mwenyezi Mungu alimteremshia wahyi Musa pamoja na nduguye Harun (‘Alahyi Salaam) wajiwekee majumba maalumu miongoni mwao tofauti na nyumba za watu wa Firauni; ili wawe katika matayarisho ya kuhama pindi watakapoamrishwa ili waweze kufahamiana nyumba zao, na ili wamuabudu Allah huko: “Na tukampelekea Musa na ndugu yake wahyi huu: Watengenezeeni majumba watu wenu katika Misri na zifanyeni nyumba zenu ndio mwahali mwa ibada, na

Kisha Allah akamteremshia Wahyi mja wake Musa: “Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa. ” (26:52),

Jibu la Firauni likawa: “Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo. (Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo. Nao wanatuudhi. Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari.” (26:53-56),

Na Allah akataka: “Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem, Na makhazina, na vyeo vya hishima, Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili.” (26:57-59)

Wakawafuata Bani Israil: “Basi wakawafuata lilipo chomoza jua. ” (26:60),

Walipofika kwa Bani Israil:“Na yalipo onana majeshi mawili haya, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana! ” (26:61),

Lakini jibu la Musa lilikuwa limejaa tumaini la Allah, kumjua na kumtegemea yeye Allah Ta’ala:“(Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa!” (26:62),

Baada ya hapo hidaya ya Allah na rehma zake zikateremka: “Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa. Na tukawajongeza hapo wale wengine. Tukawaokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote. Kisha tukawazamisha hao wengine. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini. Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.” (26:63-68).

Katika wakati huu mgumu wenye kutisha: “Tukawavusha bahari Wana wa Israili, na Firauni na askari wake wakawafuatia kwa dhulma na uadui!...” (10:90),

Hapa ndipo Firauni alipoyakinisha mauti na kuangamia: “…Hata Firauni alipo kuwa anataka kuzama akasema: Naamini kuwa hapana mungu ila yule waliye muamini Wana wa Israili, na mimi ni miongoni mwa walio nyenyekea” (10:90),

Lakini alishachelewa; kwani mauti yalishamdiriki: “Ala! Sasa? Na hali uliasi kabla yake na ukawa miongoni mwa mafisadi! ” (10:91),

Katika agano na Mola wake na Bani Israil kuabudu ndama

Mwenyezi Mungu akatimiza neema yake kwa Bani Israil kwa kumuangamiza adui yao na walipovuka bahari: “Na tukawavusha bahari Wana wa Israili, wakafika kwa watu wanao abudu masanamu yao. Wakasema: Ewe Musa! Hebu tufanyie na sisi miungu kama hawa walivyo kuwa na miungu….” (7:138);

Yaani ombi la mjinga baada ya neema ya kuokolewa na Allah dhidi ya Firauni na majeshi yake: “…Musa akasema: Hakika nyinyi ni watu msio jua kitu. Hakika haya waliyo nayo watu hawa yatakuja angamia, na hayo waliyo kuwa wakiyafanya yamepotea bure.” (7:138-139),

Kisha Musa akaenda katika kiaga na Mola wake: “Tulimuahidi Musa masiku thalathini na tukayatimiza kwa kumi; ikatimia miadi ya Mola wake Mlezi masiku arubaini. Na Musa akamwambia nduguye Haarun: Shika mahala pangu kwa watu wangu na utengeneze wala usifuate njia ya waharibifu. ” (7:142),

Allah akazungumza na Musa na akamfanya mahsusi kwa maneno yake na ujumbe wake: “(Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteuwa wende kwa watu na Ujumbe wangu na maneno yangu. Basi chukua niliyo kupa na uwe katika wanao shukuru.” (7:144)

Na akamneemesha kwa mawaidha na Taurati ambayo ndani yake kuna hukumu za Allah: “Na tukamuandikia katika mbao kila kitu, mawaidha na maelezo ya mambo yote. (Tukamwambia): Basi yashike kwa nguvu na uwaamrishe watu wako wayashike kwa ubora wake. Nami nitakuonyesheni makaazi ya wapotofu.” (7:145),

Kiaga ilipotimia, na Mola wake akampa Musa Taurati, Musa alirudi kwa watu wake na akawakuta: “Na baada yake watu wa Musa walimfanya ndama kutokana na mapambo yao (kumuabudu), kiwiliwili tu kilicho kuwa na sauti. Hivyo, hawakuona kuwa hawasemezi wala hawaongoi njia? Wakamuabudu, na wakawa wenye kudhulumu. Na walipo juta na wakaona ya kwamba wamekwisha potea, walisema: Ikiwa Mola wetu Mlezi hakuturehemu na akatusamehe, bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa walio khasiri.” (7:148-149),

Ikawa ni habari yenye kuumiza sana kwa Musa: “Na alipo rudi Musa kwa watu wake, naye amekasirika na kuhuzunika, alisema: Ni maovu yalioje mlio nifanyia nyuma yangu! Je, mmeitangulia amri ya Mola wenu Mlezi? Na akaziweka chini zile mbao, na akamkamata kichwa ndugu yake akimvutia kwake. (Haarun) akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Hakika hawa watu wamenidharau, na wakakaribia kuniuwa. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu, wala usinifanye pamoja na watu madhaalimu. (Musa) akasema: Mola Mlezi wangu! Nisamehe mimi na ndugu yangu, na ututie katika rehema yako. Nawe ni Mwenye kurehemu kushinda wote wenye kurehemu.” (7:150-151),

Kisha akaongea na Saamiriy aliyetengeneza ndama yule, akasema: “(Musa) akasema: Ewe Msamaria! Unataka nini?” (20:95)

Akamjibu: “Akasema: Niliona wasiyo yaona wao, nikashika gao katika unyao wa Mtume. Kisha nikalitupa. Na hivi ndivyo ilivyo nielekeza nafsi yangu.” (20:96);

Jibu la Musa likawa jibu lenye nguvu lenye kukata hoja zote za kumshirikisha Allah: “(Musa) akasema: Basi ondoka! Na kwa yakini utakuwa katika maisha ukisema: Usiniguse. Na hakika una ahadi kwako isiyo vunjwa. Na mtazame huyo mungu wako uliye endelea kumuabudu - Sisi kwa hakika tutamchoma moto, kisha tutamtawanya baharini atawanyike. Hakika Mungu wenu ni Allah, Mwenyezi Mungu, tu. Hapana Mungu isipo kuwa Yeye. Ujuzi wake umeenea kila kitu. ” (20:97-98),

Kisha Musa akaenda nao kuelekea ardhi tukufu, baada ya kuchukua mbao (za maandiko): “Na Musa ilipo mtulia ghadhabu aliziokota zile mbao. Na katika maandiko yake mna uwongofu na rehema kwa wanao mwogopa Mola wao Mlezi.” (7:154),

Baadhi ya Bani Israil walikuwa hawakubali yaliyomo katika Taurati; Allah akanyanyua Jabali juu yao: “Na pale tulipo unyanyua mlima juu yao ukawa kama kwamba ni kiwingu kilicho wafunika, na wakadhani kuwa utawaangukia, (tukawaambia): Kamateni kwa nguvu tuliyo kupeni, na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kumcha Mungu.” (7:171),

Ng'ombe wa Bani Israil

Hivyo wakachukua pamoja na kuwa kuna uongofu kwao na rehema kwa kuogopea jabali lisije kuwaangukia, wakaendelea kuwafanyia maudhi Bani Israil pamoja na Mtume wao Musa (‘Alahyi Salaam). Basi mara moja wakauwa mtu, na mtu yule alikuwa ni Bani Israil tajiri, mtoto wa nduguye alimpitia usiku na akamchinja! Wakatofuatiana na kutuhumiana na kila mmoja akajitetea, wakamfuata Mtume wao Musa (‘Alayhi salaam), na kumwambia kwa jeuri na adabu mbovu; ikiwa wewe Musa ni nabii basi muulize Mola wako! Allah akamuamrisha Musa: Ewe Musa waamrishe Bani Israil wachinje ng’ombe, kisha wachukue kiungo chake wampige nacho maiti; nami nitamuhuisha kwa idhini yangu; hivyo maiti Yule atazungumza na kumtaja aliyemuua, Allah amesema: “Na mlipo muuwa mtu, kisha mkakhitalifiana kwayo, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyatoa hayo mliyo kuwa mkiyaficha. Tukasema: Mpigeni kwa kipande chake (huyo ng’ombe). Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anakuonyesheni Ishara zake ili mpate kufahamu.” (2:72-73),

%%

As-Samiry – Mtengeneza Ndama wa Sanamu.
Haiwezekani Mtume wa Allah Harun kuwa ndie aliyetengeneza ndama na kulingania ushirikina: Mitume wote walikuwa ni walinganizi wa Tawhid. Atakayenukuu yasiyokuwa hayo amepotoka, mfano wa hayo yaliyokuja: “Harun akawaambia: Zivunjeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mkaniletee. Watu wote wakazivunja pete za dhahabu zilizo katika masikio yao, wakamletea Haruni. Akaipokea mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha; na wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyo kutoka katika nchi ya Misri.” (Kutoka: 32/2-4). Agano la kale.

Musa akasema: Chinjeni ng’ombe, na wangemchukua ng’ombe yeyote ingetosha lakini kutokana na maudhi yao Allah akasema kwa ulimi wa Musa: “Na Musa alipo waambia watu wake: Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mchinje ng’ombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha? Akasema: Audhubil lahi! Najikinga kwa Mwenyezi Mungu nisiwe miongoni mwa wajinga. ” (2:67)

Watu wakajibu: “Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni ng’ombe gani?...” (2:68)

Walikazania nae Allah akawakazania: “…Akasema: Hakika Yeye anasema kwamba ng’ombe huyo si mpevu, wala si kinda….” (2:68)

Sio mkubwa mzee wala mdogo: “…Akasema: Hakika Yeye anasema kwamba ng’ombe huyo si mpevu, wala si kinda, bali ni wa katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyo amrishwa.” (2:68)

Wakajifunga zaidi: “Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie nini rangi yake?...” (2:69),

Allah hakuwauliza rangi na hakuwawekea sharti maalumu: “…Akasema: Yeye anasema, kuwa ng’ombe huyo ni wa manjano, na rangi yake imekoza, huwapendeza wanao mtazama.” (2:69),

Wakakusanyika katika baraza maalum, kisha wakarudia maneno yao: “Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni yupi? Hakika tunaona ng’ombe wamefanana. Na kwa yakini, Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda, tutaongoka. ” (2:70),

Allah akawajibu: “Akasema: Yeye anasema: Kuwa huyo ni ng’ombe asiye tiwa kazini kulima ardhi wala kumwagia maji mimea, mzima, hana baka. Wakasema: Sasa umeleta haki. Basi wakamchinja, na walikaribia kuwa wasifanye hayo.” (2:71),

Wakatafuta katika miji na vijiji vya Bani Israil, kijiji hadi kijiji; wakampata ng’ombe huyu kwa tabu na taklifu kubwa na kwa thamani ghali mno; wakamchinja na hawakuwa wakitaka hilo, wakampiga maiti ambaye wametofautiana ni nani aliyemuua kwa sehemu ya kiungo cha ng’ombe yule; maiti Yule akaamka kwa kutetema na hasira; akaamka akiwa hai kutoka kaburini kwake kwa idhini ya Allah akiwa amesimama, Musa akamuuliza: Ni nani aliyekuuwa? Akasema: Huyu hapa: “Tukasema: Mpigeni kwa kipande chake (huyo ng’ombe). Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anakuonyesheni Ishara zake ili mpate kufahamu.” (2:73).

Walipofika katika ardhi tukufu, waliwakuta watu wenye nguvu (majabari): “Na pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, alipo wateuwa Manabii kati yenu, na akakufanyeni watawala, na akakupeni ambayo hakuwapa wowote katika walimwengu. Enyi watu wangu! Ingieni katika nchi takatifu ambayo Mwenyezi Mungu amekuandikieni. Wala msirudi nyuma, msije mkawa wenye kukhasirika. Wakasema: Ewe Musa! Huko wako watu majabari. Nasi hatutaingia huko mpaka wao watoke humo. Wakitoka humo hapo tutaingia.” (5:20-22), “Wakasema: Ewe Musa! Sisi hatutaingia humo kamwe maadamu wao wamo humo. Basi nenda wewe na Mola wako Mlezi mkapigane. Sisi tutakaa hapa hapa.” (5:24);

Allah akawakosoa kwa udhaifu wao, na akawaadhibu kwa upotofu na kuacha kwao jihadi na kwenda kinyume na Mtume wao, Musa akasema: “Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi similiki ila nafsi yangu na ndugu yangu. Basi tutenge na hawa watu wapotovu. ” (5:25),

Allah Mtukuka akamuitikia: “(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi nchi hiyo wameharimishiwa muda wa miaka arubaini, watakuwa wakitanga-tanga katika ardhi. Basi wewe usiwasikitikie watu wapotovu. ” (5:26),

Wakawa wanatembea katika ardhi bila malengo usiku na mchana, asubuhi na jioni.