Sitara ya Kimaadili

Sitara ya Kimaadili

Sitara ya Kimaadili

Rashidi alikutana na Maiko kulingana na ahadi waliyowekeana kati yao pembeni ya stesheni ya treni inayosafiri Paris kupitia English Channel… walitafuta kiti wakakaa wakisubiri muda wa kuondoka treni.

Maiko: Nadhani wakati unatutosha kubadilishana mazungumzo kuhusu mtazamo wenu juu ya mavazi ya mwanamke… utanieleza kuhusu Hijabu …….au sivyo?I

Rashidi: Watu wengi wanaamini kuwa Hijabu ni vazi la kufunika kichwa tu, wala watu hawajui kuwa Hijabu ni fikra na mfumo wa kijamii… yatupasa kuangalia jambo hili kwa mtazamo huu.

Maiko: Nimekuona umeandaa maudhui haya na umeyapa uzito mkubwa zaidi usiostahiki!

Rashidi: Sisi tunaona watu wakitofautiana katika kuweka vigezo vya kuisitiri miili yao, na kila kundi linaona kuwa, vigezo vyake ndio maendeleo na ustarabu, wakati ambapo kundi moja linaliona kundi lingine kuwa halijaendelea, na hawa huwaangalia kundi lingine kwa mtazamo wake wa kimaadili na kifikra tu. Hivyo basi hapana budi kuwepo na maafikiano ya marejeo ya mipaka ya sifa za jumla kwa upande wa sitara yake ya mwili.

Jambo hili ni kama nilivyokuambia kwa upana wake, ukiniruhusu kwanza nikuoneshe baadhi ya misingi ambayo itaweka karibu mitazamo yetu.

Maiko: Haya karibu.

Rashidi: Nadhani kuwa sisi tunakubaliana kuwa haiwezekani kupata suluhisho katika masuala ya maisha ya msingi ya mwanadamu isipokuwa baada ya kufahamu undani wa mwanadamu na kufahamu ukweli wa maarifa yake kamili.

Maiko: Hii ni hali ya kawaida.

Rashidi: Nadhani maendeleo makubwa ya kielimu yaliyofikiwa na tunayoendelea kuyaona, ni dalili ya mipaka ya elimu ya mwanadamu, yale yaliyokuwa yamejificha kwake jana, leo hii yapo wazi, na yale ambayo ulikuwa ukiyaamini jana, husahihishwa leo hii, na hivi ndivyo vile vile mwanadamu anavyovumbua-kesho na ya kuwa leo hii alikuwa ni mjinga au kwa uchache wa elimu yake ilikuwa na mipaka. Jambo hili limetajwa katika Qur’an, “Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu.” (17:85).

Maiko: Naafikiana nawe, lakini kuna uhusiano gani wa yote hayo na maudhui yetu?!

Rashidi: Hebu nisubirie rafiki yangu sijakamilisha bado, kwani tutakapo kubaliana kuhusu hilo baadae tutajua kuwa kuna sehemu zilizojificha katika masuala haya ambazo hatuwezi kuziingia katika kina chake, na hii ni kutegemea na kujitenga na matamanio yetu binafsi na taathira za mazingira, na hili ni gumu kulikwepa. Na hata kama tutashughulikia masuala haya katika njia hii basi tutakutana na pingamizi, na mipango ambayo tutaichukua katika msingi huu itakuwa ni pungufu au potofu, si hivyo tu, bali inaweza kuwa ni njia iliyo kinyume na njia sahihi ya kutatua tatizo na kuleta suluhisho.

Maiko: Bila shaka haya ni matokeo ya kimantiki, lakini kwa upande mwingine hakuna mbele yetu isipokuwa kutumia akili zetu zenye kutufikisha kwenye fikra na maarifa, na kuzama ndani ya utafiti, makosa na masahihisho ni bora kuliko kuacha mambo bila uvumbuzi na utatuzi na kusubiri mtu kufikia kwenye nukta ya kulingana ambapo mambo yake yatanyooka.

Rashidi: Kama ni hivyo wewe unakubaliana nami kuwa suluhisho ni lazima liwe na sifa ima ya kuzidisha au kupunguza, lakini wewe unaona kuwa tunalazimika katika hilo, na ya kuwa hakuna mbele yetu uchaguzi mwingine zaidi ya huo.

Maiko: Naam, ninaona hivyo.

Rashidi: Ama sisi tuna uchaguzi mwingine pembeni ya mambo haya.

Maiko: Unakusudia nini kusema: “Sisi!? Na lipi hilo suluhisho?

Rashidi: Ninachokusudia: Sisi Waislamu tuna uchaguzi ambao tunauona ni uokozi (ukombozi) wa ulimwengu na uchaguzi huu unahitimisha kuwa aliyeumba watu ndio anaowafahamu zaidi, kama alivyosema Allah: “Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari?” (67:14), na yeye Allah peke yake ndie ajuaye wasifu wa mwanadamu na kile anachokihitaji na kinachomfaa na kile kisichomfaa, na wakati huo huo Allah ametakasika dhidi ya matamanio ya mwanadamu, hisia na mwelekeo wake, kwa hivyo basi Allah pekee ndie mwenye uwezo wa kuweka mfumo mzuri kwa mwanadamu kwa hekima na ulinganifu, na hili linaonekana wazi katika Qur’ani.

Maiko (Akimkatisha): Maneno yako yameshikamana vizuri bwana Rashidi, hata hivyo usisahau kuwa mimi siamini dini yako, hivyo usinilazimishe kwa jambo ambalo siliamini…..niambie lile ambalo tumeafikiana kama tulivyokuwa tukijadiliana.

Rashidi: Pamoja na kuwa kanuni hii ni msingi ambao kila Muislamu amejisalimisha nao, ninaamini inampasa kila mwanadamu, isipokuwa sioni tatizo kuwa tukamilishe mjadala wetu kama utakavyo, lakini bila shaka katika mwanga wa kujitosha mwenyewe, yaani: Katika mipaka ya mfumo wa kijamii ambao nimekutajia hapo kabla kuwa hijabu ni sehemu katika mfumo huo…

Maiko: Hakuna neno.

Rashidi: Nilikuambia katika kikao kilichopita: Sisi hatuwezi kusahau nafasi ya kiwiliwili kwa mwanadamu, bali hata ule uhayawani wake, mwanamume kwa tabia ya maumbile yake anavutika na mwanamke na cha mwanzo anachokitamani ni kiwiliwili chake; katika hilo basi mavazi ambayo yataonesha kiwiliwili chake yatamletea matamanio mwanamume na kumshawishi mwanamume kumshambulia au kumtongoza mwanamke.

Maiko: Mimi naona katika mtazamo huo kuna kumdhalilisha mwanamke na mwanamume pamoja, kumdhalilisha mwanamke ni kumuangalia kuwa mwanamke ni kiwiliwili tu na kupuuza akili yake, maarifa na maadili yake, na kumuangalia kama vile ni mtu mpungufu ambaye hawezi kujihifadhi mwenyewe, na kwa upande mwingine ni kumdhalilisha mwanamume kwa mtazamo kuwa mwanamme anaonekana kama mnyama mkali mwenye kushambulia muhanga wake (mwanamke).

Rashidi: Je, rafiki yangu unaona mwanamke anaposimama mbele ya kioo ili ajipambe na kuchagua nguo zake zenye kuvutia huwa anafanya hivyo ili aridhishe akili ya mwanamme au maadili yake? Au kwa uchache hufanya hivyo ili amvutie mwanamume, na kama sio kwa kumfanya avutike kwake na kumuwinda? Na je unaona kuwa mwanamume anapomuangalia mwanamke mzuri aliyejipamba na kupendeza atavutika kwa upeo wa akili yake na hulainika kwa mapenzi katika upana wa utamaduni wake pindi anapomuangalia mara ya kwanza?

Sote tunajua kuwa mwanadamu yupo katika hatua tofauti katika silika, matamanio na matayarisho ya kuvuka vigingi, kama walivyo katika viwango tofauti vya fadhila na adabu, na mwanamke mwenye kuvaa hijabu huonekana kuwa ni mwenye heshima na hapendi kuwavutia wanaume ili wamtongoze, na hivyo hawi kivutio kwa watu wenye nafsi dhaifu na maadili mabaya. Qur’an imelitaja hilo kwa uwazi kuwa hijabu humkinga mwanamke dhidi ya ufasiki.

Maiko: Hata hivyo bwana Rashidi mimi ninaona kuwa tabia za baadhi ya wavaa hijabu hazilingani na maadili mema, na hili linathibitisha kuwa jambo hili linarejea kwenye dondoo zingine zisozokuwa uvaaji wa hijabu; kama vile malezi na kushikamana na maadili mema.

Rashidi: Maneno yako yana sehemu ya ukweli, mtu asidai kuwa kwa kuvaa kwake kipande cha kitambaa basi atabadilika kuwa mwanamke mwema, lakini hili halimaanishi kuwa asivae hijabu, hata kama mtu atasifika na tabia njema, au ya kuwa daktari aliyekosea au kutumia vibaya utaalamu wake hiyo haina maana kuwa kasoro ipo katika utaalamu huu, lakini humaanisha kuwa mtu huyu mwenye makosa anahitaji kunyooshwa, hivyo basi daktari huyu au mwanamke huyu aliyevaa hijabu au wengineo mfano wao, ni wanadamu, hutokewa na udhaifu wa kibinadamu.

Kwa upande mwingine Uislamu ulipoweka sheria ya hijabu kwa wasifu wake ukaiwekea kanuni ya kutoangukia kwenye machafu au katika hatua zake haujaishia kwake tu, bali umehusisha mfumo kamili kama vile maadili mbali mbali, na ukawekea mipango; ili kudhamini kufika katika viwango vya juu vya maadili mema katika maisha ya mwanadamu, na kwa ufupi: Mwanamke mwenye maadili mema huvaa hijabu, na sio lazima kuwa kila mwanamke mwenye kuvaa hijabu ndio mwanamke mwema.

Maiko: Lakini hilo halimaanishi mtazamo hasi kuwa kiwiliwili cha mwanamke kinafanana na ushetani? Je, yatupasa sisi kuchukizwa na kiwiliwili hiki?!

Rashidi: Uislamu ulipoweka wajibu wa hijabu haikuwa hivyo kuwa kiwiliwili cha mwanamke ni kiovu, inabidi kifunikwe, bali umewajibisha hilo ili hisia za mwanamme za kijinsia (za kimaumbile) zisihamasishwe, na haswa zaidi kwa wale wenye nyoyo dhaifu na tabia mbovu. Hivyo Uislamu ukaweka sheria ya hijabu kumlinda mwanamke na kuvamiwa na kubakwa na wanaume, na kadhalika kumlinda mwanamme na kutofanya zinaa–kama ambavyo sheria ya Kiislamu ilivyojali kubakisha hisia za mapenzi na hamasa za kijinsia katika mipaka ya mahusiano ya ndoa pekee, na hilo hupelekea kwenye mshikamano wa kijamii.

Maiko: Lakini ewe bwana Rashidi, ikiwa hijabu ni kinga dhidi ya mvuto wa mwanamume kwa mwanamke, kwanini basi wanaume nao wasivae hijabu vile vile ili iwe ni kinga dhidi ya wanawake kwa wanaume, kwani mwanamke hana matamanio kama alivyo mwanamume?

Rashidi (Huku akicheka): Swali zuri…Kwa hakika Uislamu umewajibisha nguo kwa mwanamume kwa uchache kuliko ilivyo kwa mwanamke, na huenda hekima katika hilo ikawa inaonekana kwa zaida ya maarifa ya wasifu wa kila mmoja. Utafiti uliofanywa na Dr. Benjamin Hayden huko Marekani hivi karibuni umethibiisha kuwa mwanamume hufurahishwa na kuona ladha kwa kumuangalia mwanamke, kwani katika akili yake kuna sehemu ambayo humsukuma mwanaume kufanya jitihada ya kumtazama mwanamke mzuri kwa matamanio, wakati ambapo mwanamke hafanyi juhudi hizo kumuangalia mwanamume mwenye kuvutia. Dr. Benjamini Hayden ni mtaalamu wa vichwa na ubongo wa wanadamu katika chuo kikuu cha Duke. Maelezo haya yameandikwa katika jarida la “Berlin Morgon Post la Ujerumani.

Kupitia utafiti huo waliangalia na kutafuta sababu ambazo zinamsukuma mwanaume kutumia juhudi hizo ili kujistarehesha kwa kumtazama mwanamke mzuri mwenye kuvutia, na kinyume chake ni sahihi kulingana na mwanamke, na ikabainika kuwa tofauti iliyo wazi kati ya mwanamke na mwanamume, ipo kwenye ubongo ambapo katika ubongo wa mwanamume kuna sehemu ambazo zinakuwa na nishati zaidi, pindi anapomuona mwanamke mzuri, na hilo ndilo linalomfanya kuhisi raha na kustarehe, ama mwanamke hali yake ni tofauti, kwani yeye haathiriki kwa hali yoyote ile anapomuona mwanamume mwenye kuvutia.

Matokeo ambayo utafiti huo umeyatoa ni: jambo la kwanza lenye kuvuta mtazamo wa wanaume katika sura za wanawake wazuri ni uso, (wa mwanamke) wakati ambapo mwanamke huangalia sura haraka haraka bila kuangalia sehemu maalum.

Nukta nyingine: Ni kuwa, mwanamume ni jasiri zaidi na mwenye kuthubutu katika kushambulia kuliko mwanamke; ambapo utafiti umedhihirisha kuwa, ujambazi kwa mwanamume huzidi mara tano ya mwanamke, hivyo basi kama mwanamke ataamua kufunga mlango katika kuhamasisha na kutochukua hatua ya kwanza, basi atafunga milango ya mwanamume kuthubutu na kuvuka mipaka yake au kumshambulia.

Maiko (Akifanya haraka): Nadhani wakati umefika kupanda treni….haya twende.!!