Kikongwe

Kikongwe

Kikongwe

(1)

Baada ya muda mrefu wa huzuni Bwana huyu alichomoa karatasi na akaandika:
“Mpenzi Katarina mimi naondoka na sirejei kamwe! Nitamaliza matatizo yangu ambayo yamenizonga. Nakwambia wazi wazi! Naomba uniwiye radhi nawaomba watoto nao waniwie radhi.”
Na huyo akaondoka pale na kwenda zake.
Alikuwa anasitasita licha ya kuwa alikuwa anajiuliza kimoyomoyo mara nyingi hakuwa na ufumbuzi wa matatizo yake zaidi ya kujitoa uhai. Alikuwa anatembea kwa hatua ndogo ndogo akiwaza rohoni: “Hivi kweli mimi ni mgonjwa.” Daima, Katarina, anasema hivyo, akiwa ananishauri niwe mwenye imani na myakinifu. Hayo karejea mara nyingi.

Pambana na maradhi ya wasiwasi, Joji wala usikate tamaa.

Na hata baba yake alikuwa anamwona kuwa anaumwa, alisema hayo na kumwambia kuwa maradhi hayo ya kurithi yametoka kwa upande wa mama yake. Na Kakhi, mkuu wake wa kazi amempa nasaha mara nyingi ili Joji atulie na ajiweke sawa. Bwana huyo ambaye ni Myahudi akimsemesha kama nduguye akisema mara nyingi huku anatabasamu na kumtania.

Kipenzi changu Joji, nisikilize, wewe unajishughulisha nafsi yako bila faida yo yote ya yale unayoyawaza hayakuongezi kitu cho chote, tatizo kubwa ni kuwa fikra hizo zinakuzuwia na unashindwa kutumia uhai wako vema.

Joji sasa ana miaka thelathini na nane, alimwoa Katarina ambaye ni Mwingereza mwenziwe. Lakini Katarina ana asili ya kutoka India. Ndoa yao imedumu kwa miaka kumi ambayo walipata watoto watatu; wa kwanza Maria (huyo angelikuwa na umri wa miaka kumi, lakini alifariki akiwa na miaka saba); Maiko (ana miaka minane) na Sali (ana miaka sita). Tangu alipofariki mtoto wake wa kwanza – Maria hajatulia. Daima amekuwa mwenye kuwaza tu nini maana ya maisha, nini mauti na sababu gani mpakaapende fikra za falsafa.

Alizidisha maswali sana. Joji alizama katika kusoma falsafa na historia na akawa anasoma dini mbalimbali. Huenda usomaji wake huo mwingi ulimfanya asione ugumu kumwoa KatarinaMkatoliki, mwalimu wa mambo ya dini.

Joji alikuwa anamwona mkewe kuwa ni mtu mwenye imani na aliye makini sana jambo ambalo yeye hakuwa nalo licha ya kuwa yeye alijinaki kuwa ni wa madhehebu ya Kiprotestanti. Na bado aliendelea kuwa anauliza mambo yote. Alikuwa anashangaa kuona bibi huyo alikubali mambo yote na yeye akaendelea kujiona kuwa anauliza maswali kwa sababu ana akili kitu ambacho Katarina mchaMungu hakuwa nacho. Alibishana naye mara nyingi na mijadala mingi ilihusu akili ambayo inawakilishwa naye, na imani na msimamo ambao unawakilishwa na Katarina, au wakati mwingine mjadala unakuwa kati ya ukweli wake yeye Joji na mambo ya kufikirika ya Katarina. Ama ubishi ukianzia kwa Katarina ulikuwa juu ya imani yake na kukubali kwake juu ya dini yake na shaka na maradhi ya Joji. Mwisho mabishano hayo yalikuwa yakiishia ukimya mrefu tu. Na kama isingelikuwa mapenzi baina yao wawili wangeli kuwa wamekwisha achana muda mrefu.
Na kwa mashaka aliyokuwa nayo Joji kuzidi hasa baada ya kifo cha binti yake mijadala ikaongezeka kuwa mikali na tete, maswali yaliyo kuwa yanajirejea yakawa: Kwa nini tuliumbwa? Na kwa nini tunaishi? Na wapi tunako kwenda? Maswali haya yalitawala fikra za Joji. Maswali haya yanaonekana kuwa ni mepesi, lakini ni mazito sana. Na wana falsafa wamepata kuzama katika maswali hayo, wakatumia akili zao na maarifa yao kutokana na uzoefu na mwangalio wao wa maisha na mazingira yaliyopo. Yeye akawa anaona kuwa majibu yake yote hapo ni mwanadamu kuwa huru na kuwa mwenye furaha.
Na pale alipokuwa njiani akielekea kwenda kujiua zilikuja hoja nyingi mbele yake kutokana na maisha yake. Hoja hizo zilipita mbele ya macho yake na kumkumbusha binti yake alivyokuwa anahangaika katika mwisho wa uhai wake akiwa katika gari la wagonjwa. Lakini umauti ulishinda na kumbwaga yule binti maskini–na ukachukua uhai wake na uzuri wake na kuondoka na roho yake na mwishowe yeye mwenyewe. Pia akamkumbuka mtoto wake wa kiume Maiko, ambaye alipata kumwuliza siku moja akiwa amechoka na shughuli nyingi:

“Baba yangu kwa nini unakwenda kazini kila siku?”

Ili nipate ujumbe kwa maisha yangu na pia nawe nikutimizie haja zako.

Una maana gani kusema ujumbe kwa maisha yako?

Kuwahudumia watu na kuleta manufaa kwa wanadamu.

Kwa nini?

Aliguna Joji kwa swali hilo akihisi kuwa lina mgusa kwa undani kisha akamjibu.

Kwa ajili ya jambo kubwa –huenda hulifahamu hilo wewe na hata mimi!

Baba! Wewe mkubwa na hulijui hilo!. Mimi nikiwa mkubwa nitajua kila kitu na sinto acha jambo kubwa lipite vivi hivi nisilijue.

Maiko…sahau hayo kijana wangu mpenzi.

Kisha akacheka na kujisemeza moyoni: Hizi ndizo nasaha nipewazo kila siku: “Sahau haya mambo na faidi maisha yako”. Kisha akamwambia mwanawe:

“Usiogope siku moja nitakujibu hilo.”

Baba! umemaliza masomo yako, na unasoma sana, na hujui!

Ah! mwanangu mpendwa! Je umemaliza kazi zako za masomo ya shuleni?

Ndiyo!

Basi hilo bora. Usiku mwema.

Basi aliendelea kuwaza na kuwazua huku akiwa anasonga mbele na safari yake nzito. Inaonekana kuwa mimi ni mgonjwa kama vile asemavyo Katarina au napoteza muda wa maisha yangu kama vile vile asemavyo Kakhi, au nina wasi wasi kama vile anavyosema baba, au..zuzu kama asemavyo Maiko! Huenda yale ayasemayo Maiko ni kweli, lakini cha kuchekesha ni kuwa majibu yangu kwake yalikuwa kama wanavyonijibu wengine: Sahau, labda nilijifunza kukwepa kwa kukimbilia mbele kama watu wengi wafanyavyo!.
Akiwa njiani akielekea kwenye eneo alitakalo kujiua akakumbuka siku ambayo alishikwa na huzuni nyingi tena ya kutisha, basi alikunywa pombe sana mpaka akalewa chopi! Kisha akatoka anaendesha gari lake na akaenda akalikwamisha ukutani, akatoka huku anayumba na akiwa ameshika kitabu kiitwacho, “Falsafa ya Furaha” Askari wa usalama barabarani akamshika na kumwambia:

“Wewe kitabu chako ni –Falsafa ya furaha au falsafa ya kujiua? Je hufahamu kuwa ni kosa kuendesha gari ukiwa mlevi?

Katarina akaenda kumtolea dhamana kwa polisi wa usalama barabarani, Katarina akamwambia:

Hukupaswa kuendesha gari lako ukiwa umelewa.

Akamjibu kiutani:

Je haukuwa huu ndio usia wako kwangu: Kusahau?

Hapana siyo kwa njia hii.

Kwa nini basi siku zote unakesha ukinywa?

Ah! Mimi nakunywa kweli lakini najumuika kwa kumtumikia masiya kanisani.

Akasema akimkejeli:

Ah! Kikombe kitakatifu na kinywaji chenye baraka! Au unakwepa mambo?

Hivi sasa mabishano nawe tena yanachokesha; wewe unaogopa hata kuwaza, unakimbilia kinywaji na kukesha kwa ajili hiyo kama ninavyo fanya mimi, lakini huo ulevi wako unauvisha vazi la utakatifu.

Maneno ya Joji yalikuwa makali sana, mama yule akaangukiwa na huzuni na kisha akasema:

Lakini mimi sihitaji daktari wa nafsi na akili kama wewe!

Huenda hivyo! lakini nani anajua hilo?

(2)

Akiwa njiani njia aliyoichagua ambayo ni ndefu sana – akafika mahali akatikisa kichwa chake ili ajipange na apange fikra zake vizuri. Akawa amefikia kiwango cha kusita na akaingiwa na hofu; na anaangalia watu wanapita na wengine wanafanya mambo yao. Akaona kama vile watu hao ni chombo tu kinazunguka lakini hakina uhai wala hakuna maana yoyote. Akawa anajiuliza moyoni: Vipi watu wanakubali kuwa kama chombo kisicho na uhai? Na akiwa anaendelea na safari yake hiyo akamwona mzee Kikongwe akicheza kwa furaha na mjukuu wake. Mara akatanabahi, akatabasamu, na akacheka na akamsogelea yule mzee na akasema:

Samahani kukukatisha na mambo yako. Je wewe ni mwenye furaha?

Kikongwe akainua kichwa akamwangalia kwa mshangao na akasema:

Naam! Kisha akarejea kwenye mchezo wake na mjukuu wake.

Joji akamkatisha tena:

Vipi? Yaani kwa nini wewe una furaha! Kwa nini unaishi?

Kikongwe akamwangalia tena kwa jicho la kumchunguza na akasema:

Mwenyewe umejibu swali lako.

Vipi?

Mimi ninafuraha, kwa sababu najua kwa nini naishi, hivyo tu kwa wepesi kabisa.

Mimi kwa nini naishi? Niambie hilo tafadhali.

Hebu jiulize mwenyewe hilo. Mimi siwezi kukujibia swali hilo. Hakuna atakaye kujibia isipokuwa roho yako mwenyewe, na maisha yako.

Nakuangukia tafadhali niambie.

Nimekwambia hili swali anajibu kila mtu aliye na roho yake na uhai wake tena kwa urahisi kabisa. Mimi siwezi kukuambia jambo ambalo nafsi yako haikinaiki nalo na wala maisha yako hayana hajanalo.

Kisha Akamfuatilia Kwa makini:

Hivi wewe ndiyo umeingia katika baleghe hivyo unataka nikupe mafunzo ya jandoni juu ya maisha na ulimwengu, au umeamua kuwa mzigo kwa watu.? Tafadhali sana nipishe niache niendelee mchezo wangu na mjukuu wangu.

Nakuomba mara nyingine tena. Hivi vipi nafsi yangu na maisha yangu vinaweza kunijibia swali hilo.

Nahisi kuwa unasema kwa ukweli wala hunitanii, basi hebu niache nikuambie jambo moja. Kama ukiangalia mkataba wowote utaona kuna mipaka yake, makubaliano hayo yakiwa yamefungwa kwanza vizuri kwa kamba na kufanya makubaliano hayo mazuri tena yako sawa sawa. Vivyo hivyo maisha yako daima yamefungwa na kamba nzuri na hivyo ndivyo sababu ya maisha yako – na ndivyo tunaishi na pia kupata furaha.

Vipi? niambie bwana!

Kama kweli wewe ni mkweli basi ufunguo wa jawabu hilo upo katika utafiti, kudumu katika hilo na kuazimia na kujaribu ufikie huko!

Nifikie wapi?

Ufikie kwenye furaha!

Kwa njia gani?

Tafuta njia ya kuelekea kwenye furaha! Utajisahau na utajikuta unaona kuwa uhai wako na nafsi yako vina maana kwako na utaona ulimwengu una maana kubwa maishani mwako. Ewe bwana! Hebu niache usinipotezee muda wangu. Nataka nicheze na mjukuu wangu.

Vizuri, safi sana! Mimi siijui njia ya kuelekea kwenye furaha, huenda nitaifuata hiyo njia nami nifikie furaha kama unavyosema kama njia hiyo ipo!

Ipo! Vinginevyo maisha yasingelikuwa na maana. Kwa vyo vyote vile naomba uniarifu pale utakapo pata jibu la swali lako. Na jawabu hilo utalipata kama ni mtafutaji. Na utaelewa maana gani roho yako itavyo kujibu na jinsi uhai wako utakavyo kujibu utaikuta hiyo kamba ambayo italeta maana ya kila kitu maishani mwako.

Natamani hilo linitokee –lakini waitwa nani? Na wapi unakoishi?

Kama nitakuwa hai basi utanikuta hapa hapa na wakati kama huu katika siku ya Ijumaa. Nipe anuani yako na nitakutumia anuani yangu baadaye.

Kisha Kikongwe alimgeukia mjukuu wake na akamtupia mpira Joji alishangaa sana na akasema:

Ahsante sana! Hii hapa anuani yangu.

Kisha akaondoka..
Akaondoka huku akihisi dhiki na shida ambayo hajawahi kuipata maishani, hata katika siku ambazo alikuwa ana choka sana na kubanwa na kazi. Akaamua kuwa apate kinywaji kidogo, pombe kidogo ili apate nguvu na kutuliza akili zake. Alikuwa anahisi kama kichwa kitapasuka, lakini akaongeza kinywaji mwisho akapata kizunguzungu na akaishiwa nguvu na akawa anaishiwa fahamu na akaanguka njiani na kuzimia.
Watu walikusanyika wakamzunguka na wakamwinua naye akajikaza kisha akawambia nyumbani kwake wapi.
Hapo mlangoni akamkuta Katarina analia, kilio kizito anamlilia mumewe Joji. Na pale alipomwona Joji alimkimbilia na akajitupa kifuani kwake na kilio kikubwa. Joji akasema akimwambia:

Mimi huyu hapa niko hai kwa bahati mbaya si kufa.

Shukrani zake Mungu kwa kuwa uko salama. Niliogopa sana: Hivi kwa nini ufikirie kujiua?

Ili niondokane na usumbufu wa kelele na ghasia. Niliache lichombo ambalo linaitwa Joji –lichombo ambalo halijui maana ya kuwepo kwake na maisha yake, life roho yake na nafsi iondokane na mashaka ya kila wakati. Leo hii kama si yule Kikongwe ambaye nilikutana naye leo huko njiani na kama siyo ile pombe niliyo kunywa saa hii ningelikuwa nimepumzika saa hii na shida za maisha.

He! Kikongwe gani huyo?

Simjui, lakini alikuwa ni mtu mwenye furaha, ana tabasamu kwa raha na anajua kwa nini anaishi?

Sielewe kile usemacho, lakini namshukuru bwana kuwa hapo ulipo uko salama.

Hata mimi sikumwelewa yote aliyosema, lakini nilielewa kuwa kuelekea kwenye furaha inahitajia mtu aazimie na aamue na aanze kutafuta namna ya kufikia huko kwenye furaha.

Njia ya furaha! Utafikika huko mpenzi wangu. Lililo muhimu usikazie sana mambo kupita kiasi, sisi bado tunakuhitaji.

Hahahaha! Nitajaribu kujidhibiti nisichupe mipaka. Nitajitahidi kuitafuta njia mpaka nipate jibu na nitakuwa na furaha kama yule Kikongwe.

Katarina aliona jinsi Joji anavyohangaika na uso ukionesha mikunjo yake, akamshika mkono na akamsaidia wakaelekea mpaka wakafika chumbani kwao akajinyoosha kitandani akaanza kuwazua yale yaliyompata siku hiyo aliendelea hivyo lakini alizidiwa na usingizi akalala fofofoo.