Samahani Kidogo

Samahani Kidogo

Samahani Kidogo

Maiko: Tuna dakika kumi hadi hivi sasa hajafika Rashidi…jambo la ajabu.

Rajev: Sahihi, hili litatuathiri katika ahadi zingine.

Baada ya muda si mrefu Rashidi anaingia chumba cha mjadala, na kuanza kuwasalimu rafiki zake wawili, kisha akaanza kusema:

Samahani kwa kuchelewa kufika, kuna baadhi ya majukumu ambayo nilikuwa nayakamilisha, na ilikuwa vigumu kuyaacha au kuyaakhirisha.

Maiko: Bwana Rashidi niruhusu niseme: Hii ni tabia iliyokuwa mashuhuri kwa Waarabu na Waislamu kwa ujumla, wakati hauna hadhi kwenu, samahani kama ukweli huu utakukera.

Rashidi: Mengi uliyoyasema ni sahihi, ukweli ni kuwa tumezikosea nafsi zetu na tumetoa hisia mbaya kwa wengine dhidi yetu… hata hivyo nasahihisha kosa la tabia hizi mbaya mtu kuzinasibisha na Uislamu.

Maiko: Kama sio kutokana na Uislamu basi zitakuwa kutokana na nini? Mimi naona wengi wenye tabia hizi ni watu kutoka katika nchi zenu.

Rashidi: Kuna tofauti mbili muhimu kati ya watu wenu na watu wetu: Utamaduni na mazingira…ukweli ni kuwa ni mazingira na sio Uislamu ndio wenye kuwajibika na tabia kama hizi.

Rajev: Ni vipi hilo, jambo la lazima ni kuwa dini ndio ambayo inatengeneza muongozo muhimu wa utamaduni wenu?!

Rashidi: Hili ni kweli kabisa, lakini ukweli ni kuwa Waislamu wengi leo hii hawafuati mafundisho ya dini yao, ama ni kutokana na ujinga wao kwa mafundisho ya dini yao au ni kwa kupuuzia, na pindi athari ya dini na akida inapopungua kwa mwanadamu basi wakati huo huwa chini ya taathira ya mazingira yanayo mzunguka.

Maiko: Ni nini athari ya mazingira tunayozungumzia?

Rashidi: Nitakubainishia: Kwa mfano katika nchi zenu tokea zamani mlikuwa mkiishi katika hali ya hewa ya baridi sana, na kanuni ya kubaki na kupambana na mazingira imewafanya nyinyi kufanyia mahesabu athari ya hali hii ya hewa, na hivyo mkahifadhi chakula chenu kwa ajili ya nyakati za baridi, na mkakusanya kuni au mafuta ili mjitayarishe kukabiliana na wakati wa baridi….Vivyo hivyo mazingira yamewataka hata kabla ya kufikiria na kupanga kufuata aina fulani za tabia zinazokwenda pamoja na wakati wenyewe.

Ama katika nchi zetu zipo katika nchi zenye hali ya hewa ya wastani au joto la wastani, sifa zake ni kuwa na wastani wa hali ya hewa kwa mwaka mzima, vivyo hivyo kupatikana kwa mavuno yake na utajiri wake, hivyo juhudi za watu wake zikawa ni ndogo na hesabu za watu wake ni chache na mipango yake inatosheleza kuendelea kwa maisha; ikaathiri tabia za watu wa maeneo hayo wakamili katika kudeka (au kwa uchache sema ni: uvivu na uzembe (ambao husaidiwa na hali ya hewa ya joto) na hawakuhisi kuwa kutokuwa makini na kutoweza kusoma alama za nyakati ambazo zinaathiri kubaki kwao na kupambana kwao na mazingira.

Rajev: Hapana shaka kuwa mazingira yana athari kubwa kwa mwanadamu, na kupambana na athari zake huhitajia athari kubwa zaidi yake, Je, Uislamu haukuweza kubadilisha athari hii hasi ya kimazingira kwa kutojali mambo haya, au kwa kutoweza?

Rashidi: Ama kutoweza, hili lina sababu nyingi na hii si sehemu yake ya kulijadili, hata hivyo kwa ujumla tunaweza kusema kuwa Uislamu umeweza kutengeneza jamii zilizorejea kwake, kama ilivyoweza kupanga maisha ya wafuasi wake muda wowote ule, kuna mifano mingi katika eneo hili.

Maiko: Je unaweza kututajia baadhi tu ya mifano hii?

Rashidi: Kuna mifano mingi, miongoni mwayo ni:

Imehadithiwa kuwa ‘Ammarah bin Khuzaimat bin Thabit kuwa alimsikia Khalifa Umar bin Al-Khattwab akimwambia baba yake Khuzaymah: “Nini kinachokuzuia kulima ardhi yako?” Baba yangu akamwambia: “Mimi ni mtu mzima nitakaye kufa kesho.” ‘Umar akamwambia: “Nakulazimisha wewe kuwa utailima.” ‘Ammarah akasema: “Nilimuona ‘Umar akilima kwa mikono yake pamoja na baba yangu.” Sahaba ‘Abdullah bin Mas’ud amesema: “Mimi namchukia mtu ninayemuona ana faragha, hana chochote katika amali za dunia na amali za akhera.” na ‘Abdur-Rahman Ibn AI-Imam Abi Hatim Ar-Razi amesema; (akielezea hali ya baba yake): “Huenda alikuwa akila na ninamsomea, na akitembea na mimi ninamsomea na akiingia maliwatoni na mimi ninamsomea na akiingia nyumbani kutaka kitu na mimi ninamsomea.”

Rajev: Lakini, je, Uislamu umelipa umuhimu suala la matumizi ya wakati katika mafundisho yake, ili tupate maelekezo yake yaliyofuatwa katika zama zozote?

Rashidi: Ndio, Uislamu umetukuza sana suala la wakati na umuhimu wake umo katika kitabu (Qur’an) na Sunnah (mafundisho ya Mtume). Mwenye kupitia Qur’an na uongofu kutoka kwa Nabii wa Uislamu na katika sira ya masahaba (wafuasi wake) na Tabiuun (wafuasi wa wafuasi wa Mtume Muhammad)……Ataona hadhi ya juu iliyopewa matumizi ya wakati na kuheshimu ahadi katika hali zote, na mifano ya miongozo hiyo; ni Kuwa Allah aliyetukuka ameapa ndani ya kitabu chake zaidi ya mara moja kwa nyakati maalumu, amesema: “Naapa kwa alfajiri, Na kwa masiku kumi, Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja, Na kwa usiku unapo pita,”(891-4)

“Naapa kwa usiku unapo funika! Na mchana unapo dhihiri! ” (92:1-2)

“Naapa kwa Zama! Hakika binaadamu bila ya shaka yumo katika khasara, Ila wale walio amini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri. ”(103:1-3)

Na akaashiria kuwa katika ayah zake ni kuumba jua, mwezi, ili tuweze kujua idadi ya miaka na hesabu.

Na hayo yote yamefanyiwa kazi katika ibada nyingi za Kiislamu; ibada zote zimehusishwa na wakati, mwanzo na mwisho, bali wakati ulioainishwa kwa kila ibada zina shuruti katika masharti ya kukubaliwa kwake na kusihi kwake, ndio maana sheria ya Uislamu ikalipa umuhimu sana jambo hili, nao ni kuuheshimu na kujipamba nao kama sharti ya kukubaliwa kwa ibada ile, mathalan Allah Tabaaraka anasema:

“Mkisha sali basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu mkisimama, na mkikaa, na mnapo jinyoosha kwa kulala. Na mtapo tulia basi shikeni Sala kama dasturi. Kwani hakika Sala kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu.”(4:103); kwa hivyo swala ambayo ndio nguzo ya dini huugawa mchana na usiku katika mafungu yenye miadi thabiti na alama zilizo wazi, vivyo hivyo nguzo zingine za Kiislamu zilizobakia: Funga ina muda maalumu katika mwaka, na kwa wakati wake Waislamu wanafuata utaratibu maalumu kila siku, vivyo hivyo Zaka ambayo ni mfumo na utaratibu wa kiuchumi na wa kijamii–ambao upo chini ya muda maalumu na makadirio maalumu, na vivyo hivyo tunaona kwenye ibada ya Hijja.

Wakati katika sunnah ya Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) una ushahidi mwingi ambapo sunnah imetilia umuhimu kama ilivyo Qur’an. Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) ametukuza heshima ya kutekeleza ahadi, nayo inangia katika jumla ya kauli yake: “na Waislamu wapo katika shuruti zao.” Hivyo kuainisha muda maalumu wa mkutano au kikao kunashurutishwa kila mtu mwenyewe kujilazimisha na ahadi hiyo, akihalifu basi atakuwa amekwenda kinyume na alichojishurutisha katika nafsi yake, na Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) amefanya kwenda kinyume na ahadi ni sifa ya unafiki, Mtume amesema: “Alama za mnafiki ni tatu: Anapozungumza husema uongo, anapotoa ahadi huenda kinyume, na akiaminiwa hufanya khiana.” Hivyo mtu huyu aliyechelewa na kwenda kinyume na ahadi basi atakuwa amekwenda kinyume na ahadi ile.

Maiko: Lakini umuhimu wa wakati ni jambo lenye ushirika baina ya jamii, tamaduni na staarabu nyingi, kama ni hivyo Uislamu umeongeza nini?

Rashidi: Uislamu umeongeza thamani ya matumizi ya wakati na kuupangilia katika mapana matatu ya msingi: Kwanza: Huo ni ukomo, kwa hiyo wakati ni kitu kizuri na chenye thamani zaidi anacho miliki mwanadamu, hayo ni maisha yake, wala haiwezekani kuutanguliza au kuuchelewesha au kuuzidisha, na akiupoteza hautarajiwi kurudi kwake, na ndio maana Uislamu ukahimiza kuutumia wakati wake vizuri hadi ukomo wa mwisho, nao ni mwisho wa maisha ya mwanadamu, bali umemhusisha baada ya kifo chake na baada ya kufufuka na kuhesabiwa siku ya kiama, kama ambavyo Uislamu umemhimiza Muislamu kufaidika sana na wakati hata katika mazingira magumu kabisa; Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: “Ikisimama kiama na katika mkono wa mmoja wenu kuna mche na akaweza kuupanda kabla ya kusimama basi na afanye hivyo.”

Pili, nao ni: Kulazimika, Uislamu umefanya thamani ya kuwekeza wakati na kuupangilia ni kufuata na kuzingatia kuwa mpango huu na kuwekeza huku si hiari kwa Muislamu, bali ni lazima kwake, na hii inatokana na kuwa umri wake (ambao ndio kiasi cha muda wa kazi yake) pengine sio miliki yake halisi, bali ni hiba toka kwa Mungu wake ili auwekeze katika lile ambalo Mola wake analiridhia katika njia bora zaidi; na hapa Uislamu umeufanya muda kuwa Rasilimali ambayo mwanadamu atahesabiwa na kuulizwa namna alivyoutumia pale Mtume wa Allah aliposema: “Hauondoki mguu wa mja Siku ya Kiama hadi aulizwe mambo matano; Umri wake namna alivyoutumia….” Na akasema tena Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam): “Neema mbili zimepunjwa ndani yake kuna watu wengi; siha na faragha.” Na akasema: “Wahi matano kabla ya matano: Uhai wako kabla ya mauti yako, afya yako kabla ya maradhi yako na fursa yako kabla ya kushughulika kwako, na ujana wako kabla ya uzee wako, na utajiri wako kabla ya kufukarika kwako.”

Hapana shaka kuwa mtu ataulizwa zaidi pindi rasilimali yake inapozidi; Allah Ta’ala amesema: “Na humo watapiga makelele: Mola wetu Mlezi! Tutoe tufanye mema sio yale tuliyo kuwa tukiyafanya. Kwani hatukukupeni umri wa kutosha kukumbuka mwenye kukumbuka? Na akakujieni Mwonyaji? Basi onjeni! Kwani walio dhulumu hawana wa kuwanusuru.” (Fatir, 35:37) na Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: “Mwenyezi Mungu atachelewesha ajali (kifo) ya mja hadi atakapofikia umri wa miaka sitini.” Na imepokewa kutoka kwa Hassan Al-Basry (Allah Amrehemu) kuwa amesema: “Ewe Mwanadamu, wewe ni masiku, kila siku itakapoondoka basi na baadhi yako huondoka.” Na hii “Baadhi” hufanyika katika masaa, dakika na sekunde…kila dakika au sekunde huondoka na baadhi yako, hivyo basi wakati ni uhai.

Mapana ya tatu: Ni Ufufuo na malipo ya thamani hii, hivyo basi wakati ni katika mabadiliko ya nje, ambayo ni vigumu kwa mtu mwenyewe kuwa na utawala wake, au uwezo wa kuutawala, na kwa ajili hiyo Uislamu umeweka vichocheo vya ndani ya Muislamu ambavyo vitakuwa juu ya vichocheo hivi na misukumo ya kimaada, na hapa unakuja umuhimu wa kuchunguza dhamira kwa mazingatio kuwa ni kipengele cha msingi cha kudhibiti mpaka wa chini kabisa unaokubaliwa katika utoaji. Hivyo basi uchunguzi/ulinzi wa dhati ya mtu katika Uislamu huwa ni khofu ya kuhesabiwa na Muumba, na kutamani thawabu zake na hili ndilo linalomfanya Muislamu kutumia wakati wake katika yenye kumfaa yeye pamoja na ummah wake.

Maiko: Dini hii ni ya ajabu sana, inaingilia kila kitu katika maisha ya mwanadamu, wala haimuachii mwanadamu uchaguzi hata katika maisha yake binafsi.

Rashidi: Hapana, yeye hutoa wasaa kwa mambo anuwai na khiari za kibinadamu, na hauachi nafasi kusongwa na mifumo mingine isipokuwa kwa mfumo wake tu, na hili linawiana na mtazamo wa Uislamu kuhusu mwanadamu, ulimwengu na maisha ambayo mifano yake imetolewa huko nyuma.

Hivyo basi Uislamu unaangalia thamani (wakati) sio tu kwa kuwekeza kwa upande wa kimaada, ambapo unaingia katika upande wa utawala au wa kiuchumi, bali mtazamo wake unakwenda zaidi ya hapo. Mwanadamu kwa mtazamo wa Uislamu kabla ya kuwa mwanazuoni au mzalishaji katika makonde ya kidunia au ya kimaada anakuwa Muislamu anayeongozwa, anayeogopa adhabu ya Allah na kutaraji malipo yake, na humchunga Allah katika matendo na maneno yake yote; hivyo basi matumizi ya wakati wake na kuupangilia katika Uislamu haina maana kuwa ni fikra tupu tu, lengo lake si kutumia wakati kwa lengo la kutumia wakati tu kwa kuzidisha faida yake ya kimaada na uzalishaji pekee, bali ni zaidi ya hapo! Kwa kuwa hilo ni lengo la kiroho ambalo linatokana na khofu ya siku ya kiama, siku ya hesabu na adhabu.

Rajev: Nina maneno mengine yenye kuhusiana na tabia za Waislamu, lakini ni bora niakhirishe hadi kwenye kikao kijacho.